Taasisi ya fedha, Diamond Trust Bank (T) Ltd (DTBT), imetangaza rasmi huduma ya Xpress Money inayohamisha fedha kimataifa kwa kutumia mtandao kwa ada nafuu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam wiki iliyopita, Mkuu wa Uzalishaji na Masoko katika DTBT, Sylvester Bahati (pichani), amesema taasisi hiyo imekuwa ya kwanza kuleta huduma hiyo nchini.


“Huduma ya Xpress Money inawapa wateja njia rahisi, ya haraka na salama ya kutuma na kupokea fedha popote duniani kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” amesema.


Huduma ya Xpress Money sasa inapatikana katika matawi 16 ya benki hiyo hapa nchini, kati ya hao, manane yako Dar es Salaam na mengine manane yako mikoa ya Arusha, Mwanza, Tanga, Mbeya, Moshi, Dodoma na Zanzibar.


Meneja Uhusiano wa DTB – Ukanda wa Comesa – kitengo cha Xpress Money, Aaditya Vankatesh amesema benki hiyo ina mpango wa kufungua matawi mapya manne katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Mtwara na Mwanza, mwaka huu.


“Xpress Money inatarajia kueneza huduma zake kwa kuongeza idadi ya mawakala hadi kufikia 50 Tanzania Bara na Zanzibar, ifikapo mwishoni mwa mwaka 2013.


“Xpress Money itazindua huduma za kuchukua na kuweka fedha, na ada ya kuhamisha fedha kimataifa ni Sh 7,000, na ndani ya Afrika Mashariki ada ni Sh 5,000,” ameongeza.


DTB ni kampuni tanzu ya Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi ya Aga Khan, na huduma ya Xpress Money imeenea katika nchi zaidi ya 150, ikiwa na vituo 170,000 duniani.

1269 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!