Na Mashaka Mgeta, Afrika Kusini

Takwimu za Shirika la Afya (WHO) zinaonesha kuwa takribani watu milioni 7 wanakufa kila mwaka ulimwenguni hasa katika nchi masikini ikiwamo Tanzania na zenye uchumi wa kati kwa sababu ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku kama sigara.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu milioni wanakufa kutokana na matumizi ya moja kwa moja ya bidhaa zinazotenegenzwa na tumbaku wakati takribani 890 000 wanakufa kwa kufikiwa na moshi unaotokana na sigara na bidhaa nyingine za tumbaku.

Nchini Tanzania, jarida la Tobacco Atlas linalochapishwa na asasi ya Vital Strategies linaripoti kuwa tumbaku imekuwa miongoni mwa vyanzo vinavyoathiri afya za watu.

Kwa mujibu wa jarida hilo, zaidi ya watu 17200 wanakufa kwa mwaka kutokana na magonjwa yanayohusiana na matumizi ya sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku.

Pia jarida hilo linaeleza kuwa zaidi ya watoto 17,000 wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 14 na watu wazima 247,3000 wa umri wa kuanzia miaka 15 wanaendelea kutumia sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku kila siku.

Takwimu za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) zinaonesha kuwa asilimia 32 ya saratani zilizoripotiwa kwenye taasisi hizo zilihusiana na masuala ya uvutaji sigara.

Pia utafiti uliofanywa mwaka 2013 na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na WHO ulionesha kuwa asilimia 17.5 ya watu katika ngazi ya familia wasiovuta sigara, wanaathirika kwa moshi unaotokana na wavutaji wa sigara.

Utafiti huo ukazidi kubaini kuwa asilimia 24.9 ya watu wasiovuta sigara wanaathirika kutokana na moshi kutoka kwenye sigara zinazovutwa mahali pa kazi.

Tanzania ina Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 ya mwaka 2003 ambayo hata hivyo inahitajika kufanyiwa maboresho ili iendane na Mkataba wa Kudhibiti Tumbaku wa Shirika la Afya Duniani (WHO-FCTC) ulioridhiwa na Tanzania mwaka 2007.

Katikati ya hali hiyo, wadau mbalimbali wanakutana jijini Cape Town, Afrika katika Mkutano wa 17 wa Dunia wa Udhibiti wa Tumbaku (WCTCOH2018) ukiwa na kauli mbiu ya “Kuiunganisha dunia yenye kizazi kisichokuwa na tumbaku”.

Takribanji watu 2000 wakiwa wawakilishi wa Serikali za nchi tofauti hususani wizara za afya kutoka mataifa 100 wamehudhuria mkutano huo uliofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Gebreyesus, amesema Serikali za mataifa zinapaswa kutekeleza mikakati madhubuti itakayofanikisha udhibiti wa tumbaku kwa maslahi ya watu wao na dunia.

Dk Ghebreyesus amesema kampuni za tumbaku na sigara zimezilenga nchi masikini na zenye uchumi wa kati kuwa soko lao, hivyo ipo haja ya kuwekeza zaidi katika utekelezaji wa WHO-FCTC.

“Ni wakati sasa kwa nchi zote kutekeleza ahadi zao (za udhibiti wa tumbaku) kwa sababu tumbaku inaathiri afya, uchumi na mazingira,” amesema.

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Dr Aaron Motsolaedi, amesema walengwa wakuu wa tumbaku na bidhaa zinazotokana na tumbaku ni vijana katika nchi masikini na zenye uchumi wa kati.

“Kampuni za tumbaku na sigara zinatafuta faida kwa gharama ya watu wanaoathirika, mapambano yetu sasa si dhidi ya tumbaku bali kutetea utu wa mtu,” amesema.

Balozi wa WHO wa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa, Michael Bloomberg amesema kampuni za tumbaku na sigara zinafanya jitihada kubwa kukwamisha mipango ya udhibiti wa tumbaku na kutumia taarifa potofu kuhalalisha biashara zao.

Amesema ongezeko kodi kwa tumbaku na bidhaa zinazotokana na zao hilo ni njia muafaka ya kupunguza kiwango cha uvutaji sigara na matumizi ya zao hilo hasa kwa vijana

Naye Mwenyekiti wa WCTOH 2018, Dk Flavia Senkubuge, amesema mafanikio katika udhibiti wa tumbaku yanaonekana ikiwamo utekelezaji wa WHO-FCTC, lakini changamoto zinazohusiana na zao hilo bado zinaongezeka ikiwamo hujuma zinazofanywa na kampuni za tumbaku na sigara.

Mkurugenzi wa Jukwaa la Udhibiti wa Tumbaku Tanzania (TTCF), Mama Luthgard Kagaruki amesema Tanzania imepiga hatua katika udhibiti wa tumbaku, ingawa matukio ya karibuni yanaashiria dalili za kurudi nyuma katika utekelezaji wa WHO-FCTC.

Mama Kagaruki ameshiriki mkutano huo na kuwasilisha mada inayohusu mazao mbadala yalivyobadilisha wakulima kutoka kilimo cha tumbaku mkoani Ruvuma.

Amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku barani Afrika ikitanguliwa na Malawi, na kwamba hali hiyo haijawezesha kuondokana na umasikini kama inavyoelezwa na watetezi wa tumbaku hususani kampuni zinazofanya biashara ya zao hilo.

Kwa mujibu wa Mama Kagaruki, takwimu za Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kwa mwaka 2006-2014 zilidhihirisha ongezeko la uzalishaji wa mazao mbadala na kushuka kwa tumbaku.

Mama Kagaruki amesema uhamasishaji wakulima wa tumbaku kujihusisha na kilimo cha mazao mbadala utafanikiwa zaidi ikiwa watapata soko la uhakika na bei nzuri kwa mazao yao.

By Jamhuri