Epuka kuishi maisha ya majivuno (3)

Fumbua macho yako utazame. Tazama upya uhusiano wako na Mungu wako. Tazama upya uhusiano wako na mke/mume wako. Tazama upya uhusiano wako na watoto wako. Tazama upya uhusiano wako na majirani zako. Tazama upya uhusiano wako na kazi yako. Tazama upya uhusiano wako na wafanyakazi wenzako.

Baada ya kutazama umebaini nini? Je, umebaini kasoro za kiuhusiano? Jifunze kumwomba msamaha aliyekukosea na uliyemkosea pasipo kusita. Siku yako ya ushindi ni siku ile unayomwomba msamaha aliyekukosea na uliyemkosea. Kumbuka: Mungu anakutafuta ili urekebishe mambo ambayo hayaendi sawa. Usikate tamaa bado unayo nafasi ya kuboresha uhusiano na Mungu wako, mke wako, watoto wako, jirani zako na wafanyakazi wenzako. Oren Arnold [1900-1980] mhariri na mwandishi wa kujitegemea aliyezaliwa Texas, Marekani alikuwa na haya ya kusema juu ya zawadi za kutoa wakati wa Krisimasi. Alisema: “Kwa adui yako, msamaha. Kwa mpinzani wako, uvumilivu. Kwa rafiki yako, moyo wako. Kwa wateja wako, huduma nzuri. Kwa watu wote, upendo. Kwa kila mtoto, mfano mzuri. Kwako wewe, heshima.”

Mungu akiwa dereva wa maisha yako, shetani haombi lifti. Anaogopa sana, lakini kama Mungu si dereva wa maisha yako lazima shetani atakuomba lifti. Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kukupa mafanikio unayoyataka kwa sekunde moja, lakini anakutaka kwanza uonyeshe juhudi za kuyataka mafanikio unayoyataka.

Mwandishi Henrieta C. Mears anasema hivi: “Mungu anatuacha tushindwe katika jambo ambalo si la msingi ili tuweze kufanikiwa katika jambo ambalo ni la msingi.” Kuna nyakati fulani, mtu anahisi kuwa hawezi kuona njia kwa urahisi. Anawahi kuhitimisha kwa kusema: “Hapa siwezi.” Kumbuka: Pale unaposema, hapa nimefika mwisho, Mungu anasema “Huu ni mwanzo mpya.” Mwandishi na mshairi wa Marekani, Albert Laighton, anatutia moyo kwa ujumbe huu: “Pale mwanadamu anapoona majani yamekauka. Mungu anaona maua mazuri yamechanua.”

Niseme kwamba; inawezekana kabisa ukafanikiwa kuishi maisha unayoyapenda, lakini pia inawezekana kabisa ukafanikiwa kuishi maisha usiyoyapenda. Uchaguzi wa maisha yako unao wewe mwenyewe. Nakusihi: Chagua mtazamo sahihi ili uishi maisha sahihi. Maisha ni swali linalojibiwa kwa jibu la ‘Uthubutu’. Ukiamua kuthubutu utaweza, usipoamua hautaweza kamwe. Mwanamuziki Bob Dylan siku moja  aliulizwa swali  na mtoto wake.  Mtoto wake  alimuuliza hivi: “Baba unapenda  sana  kuimba, je, siku  ukilewa sifa za watu halafu ukawa unaimba vibaya vibaya utafanyaje?” Baba  yake  alimjibu  hivi: “Nitaacha  kuimba.”

Ndugu msomaji, siku hizi binadamu amekuwa na utamaduni wa kupenda kwa muda, kwa sababu ya kitu flani. Huu ni ule utamaduni unaojinasibu kwa falsafa ya “Nipe – nikupe, tuachane kiroho safi.” Itoshe kusema kwamba, upendo si kitu kinachowahusu watu wawili tu, bali ni kitu kinachohusu jamii nzima anayoishi mwanadamu. Kwa ufasaha kabisa mwanateolojia wa Kanisa la Anglikana, William Backlay, anasema: “Msingi mkubwa wa furaha ya mtu duniani inatoka katika uhusiano wake na wengine.”

Upendo ni nguvu ya Kimungu inayomwezesha kila mmoja wetu kushinda hofu yake ya upweke na kujiunga na wengine, lakini wakati huohuo bila kupoteza hadhi yake au ya wengine na kubaki hivyo daima. Upendo kwa hiyo unaonekana kama sharti la kibinadamu ambalo linamwokoa mtu kutoka katika maisha ya janga la kujitenga na wengine na kumwongoza katika maisha ya kuunganika na wengine. Hebu tuone kinyume cha neno ‘upendo’ yaani ‘chuki’.

Tujiulize maswali haya kwa usikivu mwanana: Hivi ni nani kati yetu binadamu tulio hai  anaweza kuishi maisha ya chuki halafu akawa na amani katika nafsi yake? Ni nani  kati yetu binadamu tulio hai  anaweza kuishi maisha ya chuki  halafu akawa mpatanishi wa amani katika taifa lake au familia yake? Nani anafahamu mzigo wa chuki? Pengine unaweza ukawa haufahamu mzigo wa chuki. Niulize nikwambie. Chuki ni sumu isiyo na tiba ya kisayansi wala tiba ya kiasili. Tiba ya chuki ni upendo. Njia rahisi ya kuepuka chuki ni kuishi maisha ya upendo.

Mwanaharakati Martin Luther King Jr anasema: “Nimeamua kujishughulisha na upendo. Chuki ni mzingo mzito sana  ambao haubebeki.” Upendo ni mzigo mwepesi ambao unabebeka. Chuki ni mzigo mzito ambao haubebeki. Mtawa wa Kanisa Katoliki. Mt. Francisco wa Asizi alipata kutunga sala ya kusali kila siku. Sala hii ilimfaa yeye kwa wakati wake, inakufaa wewe kwa wakati wako na inanifaa mimi pia kila wakati. Alisali hivi:

Bwana nifanye niwe chombo cha amani.

Mahali palipo na chuki nilete upendo.

Mahali palipo na ghadhabu nilete msamaha.

Mahali palipo na utengano nilete umoja.

Mahali palipo na wasiwasi nilete amani.

Mahali palipo na uongo nilete ukweli.

Mahali palipo na kukata tama nilete tumaini.

Mahali palipo na huzuni nilete furaha.

Mahali palipo na giza nilete mwanga.