Ndugu Rais, wapo wanaosema kuna maneno ambayo ni makali. Ni yapi hayo maneno makali? Ukali wake upo kwa namna yanavyotamkwa kwa ukali au ukali wake uko katika maneno yenyewe kuwa hata ukiyatamka kwa upole yanabaki kuwa makali?

Kwamba, hata yakiwa yenyewe kama ni kitabuni au wapi yanakuwa makali. Maneno makali ni yapi? Ukimwambia timamu ambaye si dhaifu kuwa ni dhaifu, atakuangalia kwanza, atacheka, mwishoni atakupuuza na kukuona wewe ndiye dhaifu.

Kwake hapo yamekwisha.

Kwa asiye dhaifu kumwita dhaifu, hayo maneno si makali kwake. Atakudharau tu. Nenda sasa kwa aliye dhaifu wa kweli ukamwambie kuwa ni dhaifu, wee! Atachemka huyo kama maji ndani ya sufuria na matusi yake utayaoga. Atakwenda kila mahali anapopajua yeye akipayuka ovyo huku akisahau kuwa waliotutangulia walisema ni busara ukae kimya wakudhanie tu kama hauna akili kuliko ukisema na kuthibitisha hilo. Unajua makabila yetu hayakosi watani wa jadi.

Watani zake wakimsikia watamwambia kwa utani: “Ah! Mtani kumbe hata wewe hamnazo!’’ Kwa aliye dhaifu kumwita dhaifu kwake ni maneno makali sana. Ala! Kumbe maneno makali ni maneno yanayoliita koleo kwa jina lake, koleo! Kwa maneno mengine maneno makali ni yale yanayoisema kweli.

Watanzania tuna bahati kuwa na rais anayependa kuambiwa ukweli. Baba anapenda sana ukweli. Yeyote aisemayo kweli baba humchukulia kama mwanaye aliye mwema. Na sisi tunajinyenyekeza kwake baba na kumuahidi kuwa tutadumu katika kuisema kweli daima.

Tuikubali kweli kuwa malumbano kati ya Job Ndugai, Spika wa Bunge na CAG Mussa Assad yanayoendelea hadharani yamelifedhehesha Bunge.

Katika mabunge yote yaliyopita hakuna kumbukumbu inayoonyesha Bunge kuwahi kutumbukizwa katika aibu kubwa kama ilivyo sasa. Ni kweli katika hali yetu ya kibinadamu hatukubali kuitwa wezi hata kama kuku tunayeambiwa tumemuiba bado tunaye mkononi.

Lakini neno dhaifu alilolitumia CAG Mussa Assad ni sawa na tone moja tu la maji ambalo katika akili ya kawaida lisingeweza kuleta gharika kubwa katika nchi kama hivi. Tujitafakari! Ni njia ipi tulipitia mpaka kufika hapa tulipo? Kama tuliwadhuru wengine, basi hiki ni kiashiria kuwa huko tuendako mwisho wetu hauwezi kuwa mwema kwa sababu imeandikwa, kilichoingia kwa hila kitaondoka kwa hila. Kama mpaka kufika hapa tulipo tulitumia rungu au gongo, tutaondoka kwa rungu au gongo.

Neno dhaifu si tusi, hivyo kuita dhaifu si kutukana.

Ni dhahiri sasa mwingine akinasa anajaribu kujinasua kwa kushika kila kitu hata kama ni makali ambayo mwisho wake hujikata mwenyewe kama ilivyo pale kiongozi mmoja alipodai maneno ya CAG yamemchafua hadi rais. Timamu gani atakubali rais wetu atukanwe?

Unayesema ametukanwa wakati hakutukanwa unamdhalilisha baba yetu. Kutokeza kwa watu wenye fikra kama hizi

ndio wanaozidisha umuhimu wa kuwa na katiba mpya. Kwa hili mtu mzima nguo zimemvuka, achutame, atupishe! Tunajua kuwa katiba mpya haiwezi kuwa ndiyo mwarobaini wa kutatua matatizo yote katika nchi bali udhaifu

kama huu wa Rais kuwa sehemu ya Bunge lazima urekebishwe.

Wako baadhi ya watu linapotajwa suala la nchi la kuwa na katiba mpya wanajawa mawazo makubwa kupita uwezo wao. Tuliona matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi wa nchi hii katika mchakato wa katiba mpya.

Lakini hii haiwezi kutosha kuwa ni sababu sahihi ya kusema katiba mpya sasa basi. Hata hivyo baba Joseph Sinde Warioba si ametupa pa kuanzia?

Walioivuruga rasimu yake kwa tamaa ya mali na madaraka wengine si wamekwisha tangulia? Ije mvua, lije jua katiba mpya lazima itapatikana. Kama leo haitoshi itapatikana kesho. Busara ni kukubaliana na ukweli huu sasa kuliko kungojea shutuma, masimango na laana za baadaye kwa kuonekana kuwa sisi ndio tulikuwa kizingiti.

Yanaweza kuwa ni maneno makali lakini huo ndio ukweli wenyewe.

Udhaifu wa katiba iliyopo ulionekana tangu zamani hata kabla vyama vingi vya siasa havijakomaa. Miaka zaidi ya 15 iliyopita katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa: “Kutakuwa na mihimili mitatu ya uongozi katika nchi, Serikali, Bunge na Mahakama.

Bunge litawekwa moja kwa moja na wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu ambamo watu wenye sifa watasimama kuchaguliwa kuwa wabunge.

Rais atachaguliwa moja kwa moja na wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu kwa kupata asilimia zaidi ya hamsini ya kura zote.

Jaji Mkuu atatokana na mhimili wenyewe wa Mahakama kwa utaratibu utakaokubaliwa lakini si kuteuliwa na mhimili mwingine.

Rais ataunda serikali kwa kuteua watu ambao ataona wanafaa kuwa mawaziri, nao hawatafanya kazi zao mpaka baada ya kupata ridhaa ya Bunge.

Mbunge mwenye jimbo la uchaguzi hataruhusiwa kuwa waziri, maana kwa kufanya hivyo, jimbo lake litakosa uwakilishi bungeni, pia itakuwa ni kugonganisha mihimili miwili, yaani Serikali kwa maana ya waziri na Bunge kwa maana ya mbunge kwa mtu mmoja.

Hakutakuwa na mbunge wa kuteuliwa, maana bungeni ni mahali pa uwakilishi wa wananchi, yeye atakuwa anawakilisha wananchi wa wapi?

Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Tume ya Uchaguzi watateuliwa na rais, lakini hawatafanya kazi zao mpaka wapate ridhaa ya Bunge. Aidha, hawataweza kuachishwa nyadhifa zao, ila kwa ridhaa ya Bunge.

Rais atakuwa na haki ya kushtakiwa kwa makosa atakayofanya katika kipindi chake cha urais.

Mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha urais atakuwa mbunge moja kwa moja, kwa sababu ndiye atakuwa amechaguliwa na wananchi wengi kuliko mbunge yeyote. Naye ndiye atakuwa mkuu wa upinzani bungeni.

Spika wa Bunge hatakuwa na jimbo la uchaguzi, na wala hatakuwa wa chama chochote cha siasa.

Hakutakuwa na wakuu wa wilaya wala mikoa wa kuteuliwa na rais.

Viongozi wa wananchi watachaguliwa na wananchi wa mkoa, wilaya au ‘lokesheni’ husika katika Uchaguzi Mkuu. Wataunda serikali zao ambazo zitakuwa chini ya serikali kuu.”

Wanawema ni wakati sasa wa kuyatafakari haya!

Please follow and like us:
Pin Share