*Ni baada ya kudhibiti uchakachuaji kwa kuweka vinasaba

*Wabunge waliotemeshwa ulaji wanaanza harakati ivunjwe

 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeliwezesha taifa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 170 kwa mwaka, lakini hatua hiyo imewakera baadhi ya wabunge waliokuwa wakichakachua na sasa wanafanya mbinu ivunjwe.

Habari za uhakika kutoka katika ofisi nyeti za Serikali, zinaonyesha harakati hizi zinaendeshwa na Mbunge mmoja kutoka Mkoa wa Kagera aliye na uhusiano na wa moja kwa moja na kampuni moja ya kuuza mafuta nchini.

Kampuni hiyo iliyokuwa na ubia na Serikali na ambayo imebinafsishwa kwa njia za kutatanisha kwa kampuni ya Brazil, inaelezwa imempa hisa mbunge huyo na hivyo kwa sasa anafanya kazi ya kuipigia debe kwa kiwango kikubwa.

“Kimsingi ilichofanya EWURA ni kudhibiti uchakachuaji kwa njia ya kitaalamu kabisa ya kuweka vinasaba kwenye mafuta. Hili limewafanya baadhi ya maafisa ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wabunge waliokuwa wananufaika na uchakachuaji, waumie kimapato na sasa wanafanya harakati wakisema EWURA ivunjwe,” kilisema chanzo chetu.

Mmoja wa wabunge aliyeomba asitajwe aliliambia Gazeti la JAMHURI kuwa Mbunge huyo anafanya harakati za wazi kwenye Kamati za Kisekta.

“Lakini kinachosikitisha ni kuwa hatangazi bayana kuwa ana masilahi binafsi. Tungemuelewa kama angetuonyesha faida ya kuondoa mpango huu. Huyu na wengine walishirikiana kupandisha bei ya mafuta kwa nia ya kuonyesha kuwa hakuna umuhimu wa kutumia vinasaba, lakini hawatafanikiwa,” alisema Mbunge huyo.

Utafiti uliofanywa na EWURA kwa kushirikiana na TRA hadi Mei mwaka huu, unaonyesha kuwa kabla ya kuanza programu ya kuweka vinasaba kwa mwezi matumizi ya petroli yanaonyesha ni wastani wa lita 34,589,906, lakini baada ya kuanzia program ya vinasaba, petroli inayotumika hadi Aprili iliongezeka na kufikia lita 44,010,360. Hili ni ongezeko la lita 9,422,454 sawa na asilimia 27.

Ongezeko hili la kodi ukizidisha kodi inayotozwa kwa lita Sh 539 x 9,422,454 = 5,078,702,706. Hii inamaanisha wastani wa ongezeko la kodi za Serikali kwa mwaka kuwa 60,944,432,472 kwa petroli pekee.

Mafuta ya dizeli nayo baada ya kuweka vinasaba vya kuzuia uchakachuaji yamepata mabadiliko makubwa ajabu. Wastani kwa mwezi kabla ya kuanza programu ya kuweka vinasaba ilikuwa lita 69,221,971.73, lakini baada ya kuweka vinasaba zimeongezeka hadi lita 87,065,810. Hapa kuna ongezeko la lita 17,843,838 sawa na asilimia 26.

Ongezeko hilo likizidishwa kwa wastani wa Sh 514 x 17,843,838= 9,171,732,732. Hii ni sawa na Sh 110,061,000,000. Ukijumlisha kodi inayopatikana kutoka petroli na mafuta ya taa ni zaidi ya ongezeko la Sh bilioni 170 kwa mwaka. Kiasi hiki kilikuwa kinaingia mifukoni mwa wajanja wachache kabla ya EWURA kuanzisha utaratibu wa vinasaba.

Kuthibitisha kuwa uchakachuaji ulikuwapo kwa upande wa mafuta ya taa, baada ya mpango huu kuanza, uingizaji wa mafuta hayo nchini umeshuka kutoka wastani wa lita 30,025,977.11 kwa mwezi hadi lita 19,005,580. Hapa kuna upunguaji wa lita 11,020,397 sawa na asilimia 37.

Hapa kilichokuwa kinatendeka ni kwamba wakubwa hawa walikuwa wanachanganya mafuta ya taa na dizeli na petroli kisha mambo yanasonga mbele.

Kwa sasa wakubwa hawa wanapiga ndogo ndogo EWURA iache kuweka vinasaba kwa maana kwamba mafuta yanayopelekwa nje ya nchi hayawekewi vinasaba, hivyo yanapoingizwa kwenye soko la nchini kwa EWURA kutumia mitambo ya kompyuta wanayabaini haraka na hivyo kuwapiga faini wahusika. Hii inawakosesha ulaji na wanasema iachwe nchi irejee kama zamani.

By Jamhuri