Haki, ukweli ni nguzo za amani

Tanzania inaelekea kupoteza sifa ya upendo, ukarimu na uzalendo kutokana na hulka ya baadhi ya viongozi hapa nchini kupuuza na kutupa uadilifu. Sababu za kufanya hivyo ni kuweka mbele nafsi, kujilimbikizia mali, kudhulumu na kupenda mno anasa.

Viongozi ninaowazungumzia ni wa dini, siasa na serikali. Mwenyezi Mungu amewatunuku uongozi na kuwajaza sifa za heshima, upendo na ukarimu. Lakini tunu hiyo kwao ni bure aghali. Si vibaya kutamka Mwenyezi Mungu amewashushia adhabu. Ewe Mwenyezi Mungu, wasamehe na kuwanusuru viongozi hao warudi kwenye njia ya haki. Amen!

 

Kwani adhabu hiyo inawatafuna vibaya kiasi cha kuwafanya kama mazuzu na kushindwa kuwaongoza Watanzania walio nyuma yao. Matokeo yake wamekuwa wazandiki na wanafiki hadi kuwafanya wafuzu kuwateka baadhi ya Watanzania kuwa vibaraka wao.

 

Hali na matendo hayo yamefanya nchi kupoteza sifa za utulivu na usalama, ambazo hukuza na kuneemesha amani. Amani inayotokana na misingi miwili madhubuti ambayo ni HAKI na UKWELI.

 

Mwenyezi Mungu, katika vitabu vyake vinne vitukufu na vitakatifu vya dini – Torati, Zaburi, Injili na Quran – maneno haki na ukweli yamepewa ubora wa asilimia 100. Mitume waliopewa vitabu hivyo walihubiri ukweli na haki kwa maana ya ikhlasi, unyofu, uaminifu, upendo na ukarimu.

 

Mahubiri hayo yalijazwa kwa waumini na viongozi mbalimbali wa dini, siasa na serikali ili wawe vichocheo kwa waumini na wafuasi wao katika jamiii. Lakini viongozi hao kwa kujaa tadi na inda wameshindwa kuhubiri haki na ukweli.

 

Kuwako rushwa, dhuluma, uonevu na udini hapa nchini kumesababishwa na viongozi hao kuacha kuhubiri ukweli na haki kuutenga uadilifu na kukaribisha udhalimu na ufisadi kuwa sehemu ya maisha yao.

 

Kabla ya kuzama kueleza ukweli, haki, utulivu na amani, nakumbusha mambo mawili – katika toleo la kwanza la Gazeti la JAMHURI, Desemba 6-12, 2012 kulichapishwa ahadi za chombo hiki cha habari kwa Watanzania na nukuu ya kijitabu TUJISAHIHISHE cha Mwalimu Julius K. Nyerere.

 

Nia na madhumuni ya mhariri wa gazeti hilo, mosi kuwajulisha wananchi dhamira na msimamo wa gazeti kuwa “Tupo tayari kuitumikia jamii yetu kwa utulivu, uadilifu, na waledi wa hali ya juu”. Kwa maana ya kusema kweli na kutenda haki.

 

Pili, kukumbusha na kuweka msisitizo kuhusu umoja, unafsi, dhuluma, woga, haki na ukweli ambayo kwa hayo yote yameelezwa kisanifu na kinagaubaga ndani ya kijitabu hicho, ili viongozi na wananchi wazingatie na kufuata njia za haki na amani.

 

Nimetoa maelezo hayo kutaka kuelewana na wewe msomaji wa makala haya, katika safari ya kutafakari uvunjifu wa amani unaofanywa na baadhi ya Watanzania wenzetu.

 

Naanze kusema nyondenyonde za kutaka kuvunja amani ya Tanzania kulianza tangu Awamu ya Kwanza ya Utawala wa Mwalimu Nyerere. Haki hiyo iliendelea kupata mwendo kasi katika Awamu ya Pili ya Utawala wa Alhaj Ali Hassani Mwinyi, na kupata mserereko katika Awamu ya Tatu ya Utawala wa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Marais wote hao wameonja joto ya jiwe.

 

Joto hiyo imejitokeza katika sura mbalimbali ikiwamo ya ubinafsi na madaraka, uhujumu uchumi, rushwa na dhuluma, haki na uonevu, na mwisho usawa na udini. Yote hayo yamefanyika ndani ya majahazi matatu makubwa ambayo ni dini, siasa na Serikali.

 

Majaribio ya kuangusha utawala wa Awamu ya Kwanza kwa madai ya utawala bora na demokrasia ya kweli yalijichomoza si chini ya mara mbili. Vurugu za kisiasa na uchafuzi wa hali ya hewa Bara na Visiwani ulijitokeza, na baadhi ya viongozi kuvuliwa uongozi. Uchumi ulianza kuhujumiwa na udini ulikuwa ukifukuta kwa chini.

 

Katika Awamu ya Pili ya utawala, maadili ya uongozi yalianza kumomonyolewa kwa miiko ya uongozi kutupwa na kuanzishwa biashara za watu binafsi. Kashfa, matusi na kejeli vilichipuka mithili ya uyoga. Viongozi walivunjiana heshima na vikundi vya dini mbalimbali vilijichomoza na kupata usajili.

 

Awamu ya Tatu ya utawala iliridhi mambo yote hayo na kuongeza upendeleo wa kutoa haki katika baadhi ya vikundi vya maendeleo ya jamii, kuuza mashirika ya umma, viwanda na benki za wananchi kwa bei mchekeya chini ya sera ya uwekezaji na uwezeshaji kwa wageni.

 

Misimamo ya siasa mbalimbali iliminywa, uhuru wa habari kwa kiasi fulani ulifutikwa kwapani na vyombo vya mabavu vya dola vilianza kuwasulubu baadhi ya wananchi waliotuhumiwa au kuonekana na dalili za kuhatarisha amani ya nchi. Udini na ubinafsi ulianza kushika kasi.

 

Itaendelea

1286 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!