Haki, ukweli ni nguzo za amani (2)

Juma lililopita nilisema baadhi ya viongozi wa dini, siasa na Serikali pamoja na wananchi vibaraka ni vyanzo vya kuhatarisha uvunjifu wa amani nchini, kutokana na kuweka kando maadili na miiko ya uongozi na  kutozingatia kauli ya Mwenyezi Mungu kuhusu haki, ukweli, uongo, upendo na ukarimu.

Nilikumbusha kwa muhtasari baadhi ya matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotikisa nchi katika nyanja za uongozi serikalini, misimamo ya kisiasa na mahubiri ya neno la Mwenyezi Mungu.

 

Nia ya makala haya si kufurahia matukio hayo yanayoendelea kutokea tangu kupata Uhuru wa bendera mwaka 1961 hadi leo. Nia, sababu na madhumuni ni kukemea na kulaani matendo hayo ya kauli hasi zinazotolewa na vishawishi vya uvunjifu wa amani.

 

Kimsingi amani hustawi na kutawala mahali ambapo kuna mambo mawili makuu. Mosi, upo ukweli ambao unaelezwa, unazingatiwa na unafuatwa bila mashaka wala woga. Pili, ipo haki ambayo inaelezwa, inazingatiwa na inatekelezwa na jamii husika.

 

Mambo hayo mawili yana miiko yake hasi na chanya. Kwa mfano ukijua na kuamini kusema ukweli kwa maana ya kuwa muwazi, mtenda mema, ingawa haki sawa iliyojaa upendo na ukarimu. Utendaji wako daima utakuwa murua na utulivu na amani utatawala.

 

Lakini ukijua, kutoamini na kusema uongo, kuwa msiri, msharti, mdhulumati, mzandiki, mnafiki, mwizi, mwovu, mchoyo na mwenye inda n.k. utendaji wako daima utakuwa na kasoro na hapo utulivu na amani hauna nafasi ya kutawala.

 

Katika kile kijitabu chake ‘TUJISAHIHISHE’, Mwalimu Nyerere anasema “Ukimwi una tabia moja nzuri sana, haujali mkubwa wala mdogo, haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa, ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa”.

 

Maneno hayo nimeyanukuu kutaka kuonesha uzito na umuhimu wa ukweli. Unapoubana au kuufunika ukweli, tambua iko siku utajitokeza na kujibainisha kwa sababu haujapata jibu halali.

 

Leo kila pembe ya Tanzania kunazuka vurugu na ghasia kwa sababu wananchi hawakubali tena kauli za viongozi wao, hawasemi ukweli. Ahadi wanazotoa hazina mjamala, maelezo yao hayana sanifu adilifu. Maumivu ya kauli hizo yamewakifu wananchi.

 

Wananchi wanalalama kuporwa mali na rasilimali zao. Umaskini unazidi badala ya kupungua. Imani ya kuabudu haipewi uzito unaostahili, unatabaka ya upendeleo na ahadi za kujenga nchi kesho ndizo zinazotamalaki.

 

Vipi wananchi hawa watadumisha amani wakati viongozi wao hawataki kurudisha na kufuata maadili na miiko ya uongozi, ambayo ndani yake yamo mambo ya ukweli na haki? Hapa napenda kuainisha busara moja muhimu.

 

Viongozi wasiwe wepesi kunyoosha kidole kwa wananchi na wageni kutoka nchi za nje, kuwa ndiyo wahusika na chanzo cha kuvunja amani iliyoko Tanzania. Sawa, inawezekana ikawa ndiyo hivyo, lakini busara inawasuta.

 

Ni kidole kimoja tu kimeelekea kwa wananchi na wageni wao. Vidole vitatu vimeelekea kwa viongozi wenyewe kuonesha athari ya hayo makusudio. Wananchi na wageni hawawezi kufuzu bila hasa viongozi kuhusika, je, hiyo si  dosari ya wazi na ukweli?

 

Si hayo tu. Mara kadhaa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, amewasihi wananchi kuacha kupalilia vurugu, ghasia au maasi, na kuwasikiliza na kuwafuata baadhi ya viongozi wanaotaka kuangamiza nchi yetu.

 

Kwa mfano, viongozi, wananchi na wageni wanashiriki katika kutorosha madini, fedha ya wananchi na wanyamapori hai kwenda ughaibuni, kuingia mikataba kiujanjaujanja katika miradi ya maendeleo ya nchi, kupora ardhi ya wananchi na kupewa wawekezaji wa nje, na kuruhusu dini zenye misimamo ya kujenga chuki miongoni mwa wananchi.

 

Huu ni ukweli kwamba viongozi ni washiriki wakuu kutaka  kuangamiza nchi kwa sababu tu za ubinafsi, utajiri na ubarakala wa madaraka. Je, tufanye nini kunusuru Tanzania isipoteze sifa zake za upendo, ukarimu na uzalendo?

 

Mwalimu Nyerere anasema “Sitaki mtu yeyote afikiri kuwa mimi niliyeandika maneno hayo sina makosa hayo. Hivyo si kweli, kosa moja kubwa sana ambalo linatokana na unafsi ni kutaja makosa ambayo sisi wenyewe hatunayo, na kuficha makosa ambayo sisi wenyewe tunayo.”

 

Mwalimu anaendelea kusema: “Hili ni kosa lile lile linalotufanya tulaumu tusiowapenda na kutolaumu tunaowapenda bila ya kujali ukweli. Nimetaja makosa haya ili yatusaidie siyo katika kuwahukumu wenzetu tu ambalo ni jambo rahisi, lakini katika kujihukumu sisi wenyewe ambalo ni jambo gumu na la maana zaidi.”

 

Kuhusu ukweli leo yatosha. Penye majaaliwa yake Mwenyezi Mungu, wiki ijayo tunaangalia nguzo ya pili ya amani ambayo ni HAKI.

 

Inaendelea

By Jamhuri