FikRA YA HEKIMA

Ulinzi wa wanyamapori  liwe jukumu la kila mtu

Sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kuendelea kuinua uchumi wa taifa letu, ikiwa kila Mtanzania atawajibika kulinda rasilimali za wanyamapori na mazingira hai.

Wanyamapori na mazingira hai ni miongoni mwa vivutio vikuu vya utalii vinavyowashawishi wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali kuzuru hapa nchini siku zote. Wazawa nao huzuru hifadhi mbalimbali kujionea vivutio vilivyomo na kujhifunza mambo mbalimbali.

Shughuli za utalii katika Hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na tengefu huwezesha upatikanaji wa fedha nyingi za kigeni zinazochangia ukuaji wa uchumi wa taifa letu.

 

Umefika wakati kila Mtanzania kutambua kuwa ana wajibu wa kushiriki katika uhifadhi endelevu na ulinzi imara wa rasilimali za wanyamapori na mazingira hai. Dhana hiyo ndiyo itanusuru kutoweka kwa rasilimali hizo nchini.

 

Nchi yetu hivi sasa inakabiliwa na tatizo la ujangili wa kutumia silaha za kivita, linalotishia kutowesha kabisa wanyamapori wakiwamo tembo ambao ni kivutio kikuu cha utalii.

 

Athari nyingine za ujangili huo ni pamoja na kutishia amani na usalama katika hifadhi husika na kudhoofisha pato la taifa linalotokana na shughuli za utalii. Sekta ya utalii huchangia asilimia 17 ya pato hilo.

 

Tanzania ni nchi ya pili katika Bara la Afrika kwa kumiliki tembo wengi baada ya nchi ya Botswana.

 

Hata hivyo, takwimu zinazopatikana katika Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) zinaonesha kuwa idadi ya tembo imeendelea kupungua kwa kasi ya kutisha kutokana na kuuawa na majangili ndani na nje ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

 

Kwa mfano, inaelezwa kwamba idadi ya tembo hapa nchini imepungua kutoka 300,000 mwaka ya 1960 hadi 110,000 mwaka 2009. Hali hii inaashiria kuwa wanyama hao wako katika hatari ya kupotea kabisa katika uso wa Tanzania ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa haraka kukomesha ujangili.

 

Juhudi za TANAPA na serikali zinahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi wengine vijijini na mijini kufanikisha mapambano dhidi ya ujangili. Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kushiriki katika kutoa taarifa zinazofichua vitendo vya ujangili na wahusika.

 

Ni dhahiri kuwa majangili wengi hata kama wanatoka nje ya Tanzania wanajulikana miongoni mwa Watanzania kwa sababu hawawezi kwenda moja kwa moja hifadhini bila kupata mwongozo wa wenyeji.

 

Umefika wakati wa kutowafumbia macho wananchi wasio na uzalendo wala uchungu wa rasilimali za nchi yetu. Tusisite kuwafichua wasaliti hao na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

 

Inaelezwa kuwa baadhi ya watumishi wa TANAPA na serikali wasio waadilifu wanashirikiana na majangili kuhujumu rasilimali za wanyamapori na mazingira. Hao wanastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kutaka kutenda uhalifu huo.

 

Lakini kwa upande mwingine, ni vizuri TANAPA na serikali vifikirie uwezekano wa kuwamotisha raia wema wanaotoa taarifa za vitendo vya ujangili katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Ninatoa angalizo hili kwa sababu baadhi ya watu wanaofichua vitendo vya ujangili wamekuwa wakilalamika kutopata msaada wowote kutoka TANAPA na serikalini pindi majangili wanapowatishia maisha.

 

Utamaduni wa kuandaa zawadi mbalimbali na kuhakikisha usalama kwa watu wanaojitolea kuwafichua majangili utasaidia kuongeza msukumo wa wananchi wengi kuchukia ujangili na kushirikiana na mamlaka husika kulinda rasilimali za wanyamapori na mazingira hai.

 

Watanzania wote, kila mmoja kwa nafasi yake, tukidhamiria kwa dhati ya moyo chini ya mwongozo wa TANAPA na serikali yetu tutashinda vita dhidi ya ujangili ndani na nje ya hifadhi zetu. Tanzania bila ujangili inawezekana.