Miaka 50 hakuna maendeleo! – 2

Wiki iliyopita katika makala haya nilikumbusha vitu vinne: Ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora jinsi vilivyoweza kuleta maendeleo ya nchi na watu katika elimu, afya, siasa na uchumi, pamoja na kujenga umoja na mshikamano wa Watanzania.

Leo naendelea na sehemu ya pili. Umoja wetu ulisaidia sana kuondoa tofauti zetu za rangi, dini na ukabila, na kujenga umoja wa kitaifa. Umoja huo ulichanua chini ya kaulimbinu za Uhuru ni Kazi, na Mtu ni Afya. Si hivyo tu, watoto na wakubwa – wake kwa waume – walikariri na kuimba kaulimbiu nyingine za chakula bora, mazao bora shambani na kazi ni kipimo cha utu.

Tabia ya choyo, inda na ufisadi wa baadhi ya viongozi wetu nchini ilisababisha maendeleo yetu kufifia, Siasa ya Ujamaa kufa, dhuluma kufunika haki ya Mtanzania na nchi kukosa dira na kupoteza mwelekeo.

Waliofanya vituko hivyo ni ndugu zetu tuliowaheshimu, tuliowaamini na tuliowapa madaraka ya kushauri na kuongoza. Walichofanya ni kutusaliti na kuzika siasa safi na uongozi bora. Wametuachia watu na ardhi.

Vitu hivyo [watu na ardhi] kwao ni mtaji wa kujipatia maendeleo, na kwetu wananchi ni kufuli ya mlango wa maendeleo yetu. Leo wanaimba na kutamba eti miaka 50 hakuna maendeleo.

Wanajifanya kusahau na kujifanya hapajatokea maendeleo ya aina yoyote, ilhali nyoyo zao kwa ndani zinawasuta na sura zao kwa nje zinaona haya na kuinama. Ndiyo maana hawaitangazi kaulimbiu hii hadharani kwa vinywa vyao, bali huwaelekeza watoto wao, vibaraka vyao, mashemeji na wakwe zao kupiga mbiu hiyo.

Ni vizuri kuwashtua viongozi hao hata kama hawapendi, bado watambue ukweli ni ukweli kamwe hauwi uongo. Ni vema kuwafahamisha watoto na wakwe zao, hasa vijana wanaodandia jukwaa la siasa, ambao hawakupata kuona maendeleo yaliyopatikana. Hapa nataja mifano michache tu:

Kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962 kulisereresha elimu, mila na utamaduni kutolewa kwa vijana. Lugha ya Kiswahili, mavazi ya heshima, mambo ya jadi, kazi za mikono, ufundi, kilimo na vielelezo vya utamaduni vilizingatiwa na vijana.

Shule za msingi na sekondari zilipanuliwa na nyingine mpya zilijengwa na kutoa nafasi nyingi kwa watoto wa wakulima na wafanyakazi kupatiwa elimu bure na bora. Vyuo vya walimu vilijengwa zaidi na kutoa walimu wahitimu wengi waadilifu.

Sekondari na vyuo vya ufundi vilivyoanzishwa viliwezesha viwanda vidogo vidogo kutoa ajira kwa vijana. Wataalamu na mafundi stadi wazawa na wale wa nchi za nje walitoa mafunzo na kuanzisha karakana za kufua na kusana vipuri mbalimbali kwa mahitaji ya mitambo yetu nchini.

Chuo kikuu cha kwanza kilijengwa nchini chini ya hamasa ya wananchi wenyewe kuchangia fedha ya ujenzi. Chuo kilitupatia wasomi waaminifu na waadilifu katika taaluma ya sheria na baadaye katika taaluma za uhandisi, elimu, uganga, biashara, utawala, mipango na uchumi.

Watu wazima na wazee nao hawakuachwa nyuma kupata elimu chini ya kaulimbiu ‘Kisomo Chenye Manufaa’, walijifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Mafunzo ya siasa, ulinzi na ufundi yaliyotolewa kwa lengo la kufuta ujinga.

Kilimo cha kutumia plau na ufugaji wa kisasa ulishika kasi kupitia mafunzo yaliyotolewa na vyombo vya habari na vyuo vya kilimo ndani na nje ya nchi. Mabwana na mabibi shamba, maafisa kilimo na mifugo walistawisha sekta hizo na kuondoa njaa na kuwezesha kupata fedha za kigeni kutokana na mazao ya chakula na biashara.

Wagonjwa wa maradhi mbalimbali walipatiwa tiba bure kuanzia zahanati, vituo vya afya hadi hospitali. Vyuo vya uganga na utabibu vilipokea vijana wengi wenye sifa za fani hizo. Aidha, chuo cha maji kilianzishwa na kutoa wataalamu, mafundi na wahandisi wa maji. Visima na mabwawa vilichimbwa na baadhi ya vijiji na miji vilianza kupata maji safi na salama.

Maendeleo yetu yalituwezesha kuwa na viwanda vya kusindika nyama za makopo, samaki na maziwa, kutengeneza zana za kilimo na mbolea. Viwanda vya ngozi, viatu, mikanda, mabegi, tumbaku na sigara. Madebe, mabati na chupa tulizalisha wenyewe, sindano, nyembe na visu tulisana wenyewe.

Viwanda vya nyuzi na nguo vilipigana vikumbo mbele ya wananchi kutafuta soko. Viwanda vya sabuni na manukato hakika vilirembesha na kutia rihi nzuri kwenye nguo na miili ya wakulima na wafanyakazi. Watu walipendeza.

Shughuli zote hizo na nyingine nisizozitaja tangu mashambani hadi viwandani zilijenga uchumi, na kuwa na hazina kubwa ya fedha ndani na nje ya nchi na kutufanya kuwa jeuri wa kutokuwa ombaomba na dhalili mbele ya mataifa tajiri na maskini.

Mataifa tajiri hayakupendezwa na kiburi chetu chini ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Hapa suala si Ujamaa hasa kwani hatukuwa na Ujamaa wa Kikomunisti ambao ulihofiwa! Ujamaa wetu ni wa Kiafrika. Suala hapa ni kujitegemea.

1476 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!