Tusizikwe tungali hai -1

Tusizikwe tungali hai. Nimeanza na kaulimbiu hiyo iliyobuniwa na kutumiwa na wastaafu wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam-(RTD)  sasa TBC.

Wastaafu hao wameanzisha chama kitakachowawezesha kutumia ujuzi mwingi walionao kuinua sekta ya utangazaji nchinina chama hicho kimesajiliwa jina la VEMA ikiwa ni kifupi cha Veterans Electronic Media Association.

 

Wahaka nilionao unanisukuma kwa nia ya amani na upendo tu, kutamka wastaafu hao wamekuwa wanakereka sana na mwenendo wa baadhi ya vyombo vya utangazaji – redio na runinga. Wanadhani unatokana na kukosekana maelekezo sahihi kitaaluma, kitu ambacho utaalamu walionao, badala ya kuupumzisha nyumbani ungeweza kutumika kukisawazisha.

 

Kwa muktadha huo, wastaafu wameamua kutumia kaulimbiu hiyo kwa maana ya kuwa taalamu yao isiachwe kuoza bila kutumiwa, kwani nao watasahaulika.

 

Chama cha VEMA kina wastaafu katika fani za utangazaji, uandishi wa habari, ufundi mitambo na sauti, na ukutubi. Pamoja na kuwa waanzilishi ni wastaafu wa iliyokuwa radio pekee hapa nchini ya Serikali, RTD, Katiba ya VEMA inakaribisha wanachama kutoka sehemu yoyote nchini, ilimradi wawe ni wastaafu wa sekta ya utangazaji.

 

Wastaafu hao wanastahili kongole, kwani lengo na madhumuni ni kuendelea kutumia utaalamu na ujuzi wao, kujitegemea katika kuendesha maisha yao na kudumisha udugu, urafiki na umoja uliokuwapo enzi za shughuli zao mahali pa kazi.

 

Kwa mujibu wa Katiba iliyoidhinishwa na Msajili wa Vyama, Wizara ya Mambo ya Ndani, Oktoba 5, 2012, chama kina malengo manane, makubwa yakiwa kutoa huduma za ushauri na utayarishaji vipindi kwa wateja mbalimbali na kutoa mafunzo ya fani zote zinazohusika kwenye vituo vya utangazaji, pamoja na kuanzisha taasisi ya mafunzo, vituo vya radio na runinga.

 

Wastaafu wanaamini ipo haja kubwa ya kurekebisha kasoro zinazoendelea kujitokeza katika utayarishaji wa vipindi vya radio na runinga, usomaji wa taarifa za habari na utangazaji wa matukio katika vyombo hivyo.

 

Zipo kasoro nyingi, kwa mfano, kutumia lugha za mitaani badala ya lugha sanifu, kufanya masihara na utani katika kutangaza badala ya kutangaza habari za ukweli na uhakika zenye maadili na maudhui ya Kitanzania.

 

Ipo haja ya kutoa mafunzo ya miongozo na maelekezo kwa watangazaji wanaojiita watangazaji wa dotcom, yaani watangazaji wa kizazi kipya, kuacha mazungumzo ya udaku, kejeli, matusi na usongombwingo wakati wanapowasiliana na umma (hadhira). Kufanya hivyo hewani ni kufundisha na kuvunja mila na maadili ya Kitanzania.

 

Watangazaji hao hawana budi kufahamishwa na kuelimishwa madhara wanayowapatia Watanzania na hasa vijana wenzao na vijana chipukizi pale wanapopokea, wanapochombeza na wanaporusha hewani vipindi vyenye utamaduni wa nchi za Magharibi.

Ukweli, idadi kubwa ya vipindi vya redio na runinga ni matangazo yao yanayopotosha vizazi vyetu na kuvijaza kasumba kinyume na maadili ya Kitanzania.

 

Sera ya Habari na Utangazaji, 2003 inatambua upungufu wa vyombo hivyo katika kutoa huduma kwa wananchi, na watumishi wa redio na runinga wengi hawana taaluma ya kutosha. Sera inaendelea kueleza kuwa vipindi vya redio na runinga havikidhi na havizingatii maadili ya Kitanzania.

 

Maeneo mengi vijijini hayana huduma za vyombo hivyo na vituo vya utangazaji vina vipindi vichache vyenye maudhui ya Kitanzania, na hakuna utaratibu maalum kwa vituo binafsi vya redio na runinga kujiunga na vituo vya Serikali katika kutangaza matukio maalum ya kitaifa.

 

Dira ya sera hiyo inataka kuwapo vyombo vingi vya habari vinavyomilikiwa na umma na sekta binafsi, na kuzingatia maadili ya taaluma na ya jamii ili viweze kuchangia katika kufanikisha Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

 

Mwaka 1992 kulikuwa na kituo kimoja cha redio nchini, leo vipo vituo 90, kati ya hivyo, vituo sita vya Taifa, 19 vya mikoa, 62 vya wilaya na vitatu vya jamii. Kwa upande wa runinga mwaka 2000 kilikuwapo kimoja, leo kuna vituo 26 nchini, kati ya hivyo, vituo sita vya Taifa, viwili vya mikoa na 18 vya wilaya.

 

Mafanikio hayo yameweza kupatikana baada ya kutolewa Sera ya Habari na Utangazaji kwa mara ya kwanza sambamba na kuanzishwa Tume ya Utangazaji Tanzania mwaka 1993, kusimamia sekta ya utangazaji na baadaye mwaka 2003 iliunganishwa na Tume ya Mawasiliano kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

 

Pamoja na mafanikio hayo ya kuanzishwa vituo vya utangazaji na chombo cha Serikali kusimamia sekta ya utangazaji nchini, baadhi ya vipindi havizingatii maadili na havina maudhui ya Kitanzania kwa sababu watumishi wengi vituoni hawana taaluma ya kutosha.

 

Napenda kuwakumbusha watumishi katika vyombo hivyo na wadau wa habari kuwa Machi 8, 2006 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitembelea Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na kuzungumza na viongozi na watendaji wakuu wa wizara hiyo.

Alisema na nanukuu: “Kusema kweli, uhuru wa vyombo ya habari ni uhuru wa kutoa habari za kweli. Siyo uhuru wa kutunga uongo. Changamoto kubwa ya vyombo vya habari ni kujijengea hadhi na heshima” mwisho wa kunukuu.

 

Itaendelea

 

By Jamhuri