Wananchi wa Kata ya Bumera, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wametaja sababu mbalimbali zinazofanya kuwapo kwa wimbi kubwa la ukodishaji wa mashamba, kwa ajili ya kulima zao haramu la bangi kwa raia wa Kenya.

Utafiti umebaini kuwa wakazi hao wa mpakani na Kenya wanakodisha maeneo ya mashamba yao kwa Wakenya, kwa ajili ya kilimo hicho na mengineyo kinyume cha sheria.

Mkazi wa Kijiji cha Kwisarara, Edwerd Ndege, ametaja sababu za wenyeji kukodisha mashamba kwa Wakenya kuwa ni mwingiliano wa watu wa koo za kabila la Wakurya wanaoishi Tanzania na wanaoishi Kenya. Wengi wao ni ndugu na jamaa wanaotegemeana kwa hali na mali.

Ndege ameongeza kuwa mila na desturi za jamii hiyo  zinafanana na wengi wao hawajali mipaka inayotenganisha Tanzania na Kenya. Katika hali hiyo ni rahisi kumkuta raia wa Kenya anaendesha shughuli za kilimo na kulisha mifugo na hata kuilaza Tanzania na kuchunga mifugo bila wasiwasi.

“Kuna sababu nyingi lakini kubwa ni kwamba watu wa jamii hii wana majina ya kufanana,’’ amesema Ndege na kuongeza: “Pia njia ya kukodisha mashamba ni moja ya mbinu za Wakenya hapa nchini na kupata vibali vya kuwahalalisha kuwa Watanzania ili kuendelea kufanikisha shuguli na malengo yao kama vile kufanya  biashara ama shuguli za kilimo.

 

“Unajua Wakenya ni watu wabunifu wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo kuliko Watanzania, wanaingia kwa lugha ya kukodisha mashamba ama kununua ardhi na wanakaa huku kwa muda wakijishugulisha na kilimo na ufugaji.”

Inaelezwa kuwa raia wa nchi jirani wanaingia kwa kuwatumia viongozi wa vijiji na kata, ambao huwaruhusu kuishi na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji hapa Tanzania. Baada ya kuona wamezoeleka, Wakenya huendelea kupanua shughuli zao za kilimo na ufugaji ama kufanya biashara katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia imebainika kuwa katika mwingiliano huo wa koo, kabila, mila na desturi, utakuta mwanaume anakuwa na wake zaidi ya mmoja, baadhi wanaishi Tanzania na wengine wanaishi Kenya lakini wakitembeleana na kushirikiana kama kawaida bila kujali mipaka ya nchi.

 

Kwa upande wake, mmoja wa polisi jamii, Nyamaruri Guriba, mkazi wa Kijiji cha Turugheti, amesema kuwa umaskini nao unachangia kuwapo kwa wimbi kubwa la wananchi wanaokodisha maeneo yao kwa raia wa Kenya ili kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha, ikiwa ni pamoja kugharamia elimu ya watoto wao.

Guriba ameongeza kuwa wananchi wengi wanakumbwa na umaskini mkubwa unaowalazimu kuwakubalia Wakenya wanaohitaji maeneo, kwa ajili ya kukodisha na kuendesha shuguli za kilimo cha bangi na mazao mengine.

“Ukodishaji wa ardhi kwa Wakenya umekuwa ukiwawezesha baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tarime kupata fedha za kuwalipia watoto wao karo hata katika vyuo vikuu,” amesema.

 

Amesema kuwa ili kukomesha tatizo hilo, Serikali haina budi kuwawezesha wananchi wake kwa kuwapatia hatimiliki za kudumu za mashamba, zitakazowawezesha kupata mikopo ya fedha katika Benki kwa ajili ya kuanzisha miradi ya uzalishaji mali, hivyo kumudu gharama za maisha kwa jumla.

 

“Pia elimu ya uraia inahitajika kwa wananchi waweze kujua umuhimu wa ardhi ambayo ni rasilimali muhimu zaidi katika maisha ya binadamu,” amesema Guriba.

Kwa upande wake, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, amesema msako mkali unaendeshwa na jeshi hilo dhidi ya watu wanaojihusisha na kilimo na biashara ya bangi na dawa za kulevya kwa jumla ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Kamanda Kamugisha ameongeza kuwa Julai 16 mwaka huu, polisi walifanikiwa kukamata magunia manne ya bangi yenye uzito wa kilo 500 (kete 3,734) ambapo katika tukio hilo mtuhumiwa alitoroka.

Sababu inayoonekana kuchukua sura mpya ni ile ya mila ya koo kuingiliana na kusababisha wakazi wa Kenya na Tanzania kushindwa kutambua na kuheshimu mipaka inayozitenganisha nchi hizo, huku ikielezwa kuwa baadhi ya watu wana uraia wa nchi mbili (Tanzania na Kenya).

 

Umaskini unaowakabili watu wa jamiii hiyo umekuwa ukisababisha kuwapo kwa migogoro mingi ya kugombea mipaka ya ardhi, wizi wa mifugo na kuzusha mapigano ya kikoo baina ya watu wa kabila la Wakurya wilayani Tarime.

 

By Jamhuri