Tunakubali rushwa ni adui wa haki? (2)

Juma lililopita, nilielezea madhumuni ya Serikali kuunda Tume ya Kero ya Rushwa, na nilionesha matatizo makuu mawili yaliyoikabili katika harakati za kubaini kero ya rushwa nchini.

Leo ninazungumzia juhudi zilizofanywa na Serikali ya kikoloni hadi hii ya Uhuru, za kutunga sheria mbalimbali dhidi ya rushwa na kuweka vyombo vya kuzuia na kupambana na rushwa nchini.

 

Historia inatueleza kuwa rushwa ilikuwapo hata kabla ya Uhuru, lakini kwa kiwango kidogo. Mwaka 1958 wakoloni walitunga sheria ya kuzuia rushwa iliyohusisha maofisa wa ngazi za chini na kati waliokuwa wanahudumia wananchi.

 

Baada ya Uhuru, Serikali ilirithi sheria hiyo na kuanzia hapo zikatungwa sheria nyingi na vyombo mbalimbali vya kuzuia rushwa vikaundwa. Mathalani, mwaka 1966, Serikali iliunda Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, kwa lengo la kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka kwa maofisa wa Serikali na mawakala wake.

 

Mwaka 1975 Serikali ilianzisha Kikosi cha Kuzuia Rushwa baada ya Bunge kupitisha Sheria Na. 16 ya mwaka 1971 ya Kuzuia Rushwa; na mwaka 1983 Bunge lilitunga Sheria ya Kuhujumu Uchumi ya mwaka 1983.

 

Sheria hiyo ya Kuhujumu Uchumi haikudumu, kwani ilifutwa na Serikali badala yake Bunge likatunga Sheria ya Kudhibiti Uchumi na Uhalifu ya mwaka 1984.

 

Wimbi hilo la kutunga sheria kuhusu rushwa halikukomea hapo, kwani mwaka 1995 Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, kiliitangaza rushwa kama adui namba moja wa wananchi, hivyo idhibitiwe.

 

Baada ya uchaguzi huo, Serikali ilianza hatua kadhaa kwa dhamira ya kushughulikia tatizo la rushwa. Bunge lilitunga Sheria nyingine Na. 13 ya mwaka 1995 ya Miiko ya Uongozi (Leadership Code of Ethics).

 

Madhumuni ya Sheria ya Miiko ya Uongozi ni kudhibiti tabia zisizofaa kwa viongozi wa umma wa ngazi ya juu.

 

Aliyekuwa Rais wa Tanzania (mwaka 1995-2005), Benjamin William Mkapa, aliunda Tume ya wajumbe tisa ya Uchunguzi dhidi ya Rushwa, Januari 17, 1996 iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

 

Nimejaribu kuonesha jitihada za Serikali katika dhamira ya kutokomeza rushwa nchini. Pamoja na mlolongo huo, Serikali imeboresha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Swali la kujiuliza: Hivi kweli Serikali ina nia ya dhati ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini?

By Jamhuri