FASIHI FASAHA

Kuchinja nyama ni sababu ya kufarakana?

Sikilizeni maneno, wasanii tunayosema, jiepusheni navyo vitendo vitakavyotutenganisha, kufarakana, kuchukiana kumeshaanza, kukamiana kutukanana sasa ni sera, Watanzania kuweni macho, Taifa linakwenda pabaya tutakuja jijutia.

Kila pembe sikia, ni maneno ya chokochoko, tuwaulize wenzetu mmechoka na amani, misikitini, makanisani sote ni wa Mungu, sisi ni bora wale si bora yametoka wapi, Watanzania kuweni macho, Taifa linakwenda pabaya, tutakuja jujia.


Wanaleta maneno, kutuchonganisha ndugu kwa ndugu, huyu wa bara yule wa pwani, Tanzania ivunjike, Watanzania tujihadhari nazo vurugu, tuvunjevunje kisingizio ni mageuzi wa Ulaya wanaungana, mwenye macho sasa aone, tutakuja jijutia.


Nimeanza na wimbo huo ulioimbwa na kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), kikiongozwa na msanii mkongwe maarufu nchini, Kapteni John Komba, miaka 20 iliyopita.

 

Madhumuni ya kuweka wimbo huo wa ‘Kilio cha Wasanii’ ni kuwakumbusha Watazania thamani ya amani na upendo miongoni mwetu. Pili, jinsi wasanii wetu walivyotusihi kutunza amani na kuepuka madhara yaletwayo na chokochoko.

 

Ni mwezi mmoja sasa, kule mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kumechipuka sokomoko la Wakristo kupinga Serikali kuzuia Wakristo kuchinja mnyama katika machinjio ya Serikali na kuruhusu Waislamu pekee kuchinja.

 

Serikali kupitia viongozi wake waandamizi – Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikillo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, na Waziri Mkuu Mizengo Pinda – wote wametoa maelezo kuwa Waislamu waendelee kuchinja ni desturi, mila na taratibu tangu zamani.

 

Kauli hiyo ya viongozi imepingwa  na Umoja wa Makanisa ya Mkoa wa Mwanza na Kanda za Ziwa, katika tafsiri ya kuzuia Wakristo kuchinja ni upendeleo kwa Waislamu, kinyume cha Katiba ya nchi na uonevu mkubwa wa wazi dhidi ya imani ya Kikristo.

 

Wakristo hao wanataka Rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa tamko kinyume cha kauli ya Serikali. Kama si hivyo, hoja yao ya kutaka kuchinja wataifikisha mahakamani.

 

Si hivyo tu, wametishia kurudisha kadi za uanachama wa CCM na wataihukumu Serikali katika chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 2015.

 

Wakristo hao wamefika hadi mbinguni na kusema kama CCM itaungana na Serikali yake, wataingia katika maombi ili Mungu mwenyewe awaeleze cha kufanya kwa vile ni suala la imani. Wanasema watagoma kula nyama zinazochinjwa na Waislamu hadi Yesu atakaporudi na wataelimisha Wakristo madhara ya kula nyama iliyochinjwa na Waislamu.

 

Sina hoja juu ya imani yao, kwani hivyo ndivyo inavyotakiwa mtu kuwa mdini kwa maana ya kufuata taratibu za dini yake. Lakini linapokuja suala la udini hapo ndipo hoja kadhaa zinapojengeka. Naomba isiwe hivyo.

 

Kauli zilizotolewa na Wakristo kwa Serikali zinanipa mashaka. Hivi kweli Watanzania tutaendelea kuzozana katika masuala ya dini hadi lini? Ni busara kulumbana katika hoja ambazo jibu lipo wazi? Hivi tunapotoa tishio baada ya kupewa jibu sahihi, na tunapohukumu kabla ya rufani kusikilizwa, maana yake nini?

 

Leo unapokataa kula nyama iliyochinjwa na Waislamu lakini miaka kadhaa nyuma umekula nyama iliyochinjwa na Waislamu kulikoni? Je, imani hiyo ipo sasa tu, haikuwapo wakati ule?

 

Nimesoma Maandiko Matakatifu ya Bibilia kama Umoja wa Makanisa hayo yalivyonukuu katika Kitabu cha 1 Wakorinto 10:23-28, ambayo yanakataza Mkristo kula kitu kilichotolewa sadaka kwa miungu mingine. Maandiko mengine Matakatifu katika Kitabu  cha Hesabu 25: 1-9 jinsi wana wa Israeli walivyouawa na kuangamia kwa kula nyama iliyochinjwa kwa ajili ya sadaka.

 

Hoja yangu inasimama, nyama inayochinjwa na Waislamu ni sadaka kuliwa na watu?

 

Ni mwaka jana tu Wakristo waliadhimisha miaka 100 na ushei tangu kuingia nchini. Muda wote huo Wakristo wanakula nyama iliyochinjwa na Waislamu, mbona hatujasikia Wakristo waliouawa na kuangamia?

 

Miezi miwili iliyopita katika safu hii ya Fasihi Fasaha, nilizungumzia sana madhara ya udini katika vipengele vya ubinafsi, upendeleo, chuki na dhuluma na kuinasihi Serikali, viongozi na waumini wa dini kuwa macho na kuacha chokochoko.

 

Leo tunaambiwa damu za waumini wa Kiislamu na wa Kikristo imemwagika na wengine kupoteza maisha, katika mapigano yaliyosababishwa na uchinjaji nyama katika Kijiji cha Buseresere, Wilaya ya Chato, Mkoani Geita.

 

Naona hoja hii haina tija zaidi ya chokochoko kama walivyosema wasanii wa TOT. Aidha, kutaka kuipa turufu wazo eti Serikali ina upendeleo ya dini moja, kukazia udini na kuona Serikali si lolote si chochote.

 

Ni hoja yenye uchochezi iliyobeba chuki, inda na mawazo ya nchi za Magharibi za kutaka mauaji yafanyike Tanzania, na kuondoa sifa ya utulivu na upendo kwa kisingizio cha dini. Serikali iwe macho.