STARS2Wahenga walinena “haraka haraka haina baraka” tena wakanena “mwenda pole hajikwai.” Wahenga pia walitambua kuwa kwenye dharura haraka inaweza kutumika ndiyo maana wakanena pia “ngoja ngoja yaumiza matumbo.”  Tunajua vyema kuwa dharura huwa haidumu, na jambo la mara moja linatatuliwa na kwisha kisha taratibu nyingine za kawaida zinaendelea.
Tanzania kama nchi tunafahamu juu ya dharura hizi na kutenda mambo kwa uharaka. Pia pasipo na shaka yoyote tunafahamu kuwa mara nyingi njia za ‘fasta fasta’ huwa hazimalizi tatizo ndiyo maana njia hizo huwa hazidumu.


Tunafahamu vyema kuhusu walimu wa ‘fasta fasta’ walivyosaidia hapa nchini kwetu katika utekelezaji wa sera ya Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE), lakini pia katika uanzishwaji wa shule za kata. Baada ya muda walimu wale waliagizwa kusoma na sasa hawapo tena. Dharura imekwisha.
 Katika michezo dharura bila kujali na haijulikani itakwisha lini. Hakuna maandalizi yoyote ya kumaliza tatizo la kuwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ katika michezo yote. Katika soka vipigo, riadha hatuna pumzi, kuogelea hatujui pamoja na kuzungukwa na mito, maziwa na Bahari ya Hindi. Kuna wakati unajiuliza nchi yenye watu zaidi ya milioni 40 hakuna watu wenye vipaji wakatuondolea hii aibu ambayo Rais mstaafu Mzee Mwinyi aliiona mapema na akaona sisi hatuna tofauti na kichwa cha mwendawazimu?


Ukienda Ukerewe, kule kuna watu wanaogelea mpaka unaweza ukasahau umuhimu wa boti. Hao utawakuta kule Kakonko Ziwa Nyasa sawa na wale wa Malagarasi kule Kaliua. Watu wale wanajua kuogelea sana wanachohitaji ni kukusanywa na kulelewa ili wazijue kanuni.
Kule vijijini kila kona kuna vijana wanasukuma kandanda la uhakika. Wapo watu wanakimbizana huko milimani kwa burudani tu. Kuna watu wanarusha mikuki huko vijijini mpaka utashangaa. Ikifika muda wa kwenda kwenye Olimpiki na michezo mingine hawa hawaendi. Wale wanaokwenda nao hukutana kwa dharura na namna gani unaweza kupata nafasi ile wengi hawajui ndiyo maana yule mpiga mbizi kule Mto Ruvuma anajua hayamuhusu.


Ukichunguza vipigo na ‘utalii’ wetu si sababu ya kukosa vipaji. Tuna vipaji vingi kila kona, vipo tena vingine ni vikubwa kuliko hata vile tulivyozowea kuviona. Tatizo kubwa katika michezo ni mfumo wa kugundua, kukuza, na kulea vipaji hivyo. Kila siku na kila mwaka tunapoteza vipaji kimya kimya.
Vipaji hivi vinapotea bila kusaidia Taifa hili kuondokana na aibu hii. Jambo linaloangamiza vipaji hivi ni mambo ya ‘fasta fasta’. Timu inakwenda mashindanoni wiki ijayo leo watu wanakusanywa. Katika mfumo kama huu huwezi kupata vipaji halisi na hata kama vikipatikana havijalelewa na kuivishwa mpaka kumudu mashindano.


Ninatambua vipaji vilivyopo na ninaviheshimu sana na nina imani hata hao wangeweza kuleta heshima, lakini na wao wamejitutumua tu mpaka wamefika hapo hakuna juhudi zilizofanyika kulea vipaji vyao. Walipojituma na kufikia hapo wakatakiwa kuanza kuleta matokeo na si kulelewa tena. Hakuna muda wa kuleana tunataka matokeo ‘fasta fasta’ na akikosea lazima azomewe. Kijana aliyepambana na vikwazo vyote mpaka kuja kuonekana havumiliwi tena, hatakiwi kukosea, anatakiwa kuleta tunachokitaka. Hatuna huruma na wala hata hatujiulizi kama tumemwandaa kuleta hayo matokeo?
‘Fasta fasta’ imetujaa na hatutaki kuvumilia tena kana kwamba kuna uwekezaji mkubwa tulioufanya huko. Tumekuwa kama Perezi wa Madrid au Abramovich wa Chelsea kwamba hatuna uvumilivu kwa kuwa tumewekeza vya kutosha. Wengine hujitetea ati sisi ni nchi maskini hatuna pesa za uwekezaji mkubwa katika michezo. Nani amesema kuwa uwekezaji unahitaji pesa muda wote?


Tuchukue vijana wadogo kabisa wa miaka 14 hadi 17 au chini ya hapo tuanze kuwalea taratibu kwa gharama za kawaida kabisa. Wale makocha wanaofundisha timu zinazokwenda kupokea vipigo walee hawa vijana katika shule maalum za michezo. Walimu wa kufundisha masomo ya kawaida wapo wengi wanaweza kupangiwa huko baada ya kupewa mbinu kadhaa za lulea wanamichezo.
Yanahitajika mapinduzi kimichezo na tuachane kabisa ni hii ‘fasta fasta’. Tuache hii ‘fasta fasta’ inayotuangamiza maana hata hailengi dharura. Timu inayojiandaa kwenda kupigania tiketi ya kushiriki CHAN inaalikwa COSAFA inatumia mashindano yale kwenda kupata vipigo vya kujiondolea hata heshima ya kualikwa.


Labda hata vipigo vile vingekuwa vinalenga maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya Egypt lakini haikuwa hivyo, ilikuwa ni kikosi cha dharura tu. Wengi tuliamini kuwa kama wangepelekwa vijana kwa malengo ya maandalizi fulani hata kama ya ‘fasta fasta’ kungekuwa na faida fulani. Haikuwa hivyo, ilikuwa ni mambo ya dharura tu kana kwamba kuna jambo tunaloliwahi katika hivi vipigo.
Ni wazi kuwa watu wengi wamezoea ‘fasta fasta’ kila eneo ndiyo maana tumeridhika na maandalizi ya wanamichezo ila tunalaumu kwa nini hawaleti matokeo. Hatuoni kama hii dharura isiyo na ukomo ni tatizo. Tumeikubali kwa kuwa maisha yetu yamejaa ‘fasta fasta’ na hata hiyo ‘fasta fasta’ ya michezo tumeiona ni ya kawaida.


Leo vijana wengi wamekuwa watu wa kutaka kulala maskini na kuamka tajiri, hawana mikakati maana hawaitaki itawagharimu muda na wao hawataki kusubiri. Watu wapo tayari kununua vitu ‘feki’ kwa kuwa ni dharura lakini dharura hiyo haitaisha miaka nenda rudi na hata ‘feki’ ikiharibika watanunua tena ‘feki’ kwa kuwa amezowea ‘fasta fasta’.
Kupenda mafanikio bandia ndiko kulikohamia mpaka kwenye michezo. Lazima tukubali kubadili fikra zetu kama tunataka mafaniko ya kweli na ya kudumu. Tuamue kuanza maandalizi ya wanamichezo wetu. Tuwalee kimichezo na wakue kimichezo kama ambavyo tunalea walimu, wahasibu, madaktari na wengineo.


Hao tunaowaandaa nao huwa wanakosea na hatuwazomei inakuwaje kwa hawa ambao hawakuandaliwa? Tuanze sasa na kila mpenda michezo ana wajibu wake hapa na hii inafika mpaka kwa asiyependa michezo maana atafaidika kwa namna yoyote. Serikali iandae sera ya elimu ya michezo na iingizwe katika mtaala wa shule maalum. Tupate, mtaala, shule, walimu, vitabu na mazingira ya kimichezo tuandae wanamichezo wetu.


Watu wa kutoa mapendekezo haya wanaeleweka na ninaamini wakiyaandaa vyema yatapokewa na kukubalika huko kwa wakubwa waliochoka sisi kuwa kichwa cha mwendawazimu. Hii itapunguza hata tatizo la ajira na tutakapoanza kuuza wachezaji nje hata milango ya utalii itafunguka zaidi.
Mashabiki tukubali kuanza upya, tushangilie vipaji vipya vinavyoandaliwa tukijua ya kuwa wapi tunaelekea. Tutaanzia hapa kwenye ‘kichwa cha mwendawazimu’ na fahamu zitarejea taratibu mpaka tutakapomshika mkono mwedawazimu kuwa akatafute mwendawazimu wenzake wa kujifunzia kunyoa.
Tuseme ‘fasta fasta’ imetosha na aliyetufundisha hilo neno aje alichukue sisi limetuumiza vya kutosha sasa tunarejea kwa wahenga wetu na kuanza na mwendo wa pole ili tusijikwae kila wakati mpaka watu wakatuona wendawazimu. ‘Fasta fasta’ nenda kwenu na sisi tunaanza upya wala hatukuhitaji tena.

Baruapepe: amrope@yahoo.com Simu: 0715 36 60 10

 
2135 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!