Shilingi bilioni 1.2 zikiwa ni fedha za malipo ya mafao ya walimu wastaafu katika Mkoa wa Mara zinadaiwa kukwapuliwa na mafisadi, Gazeti la JAMHURI linaripoti.

Mamilioni hayo ya fedha yameelezwa kuchukuliwa kupitia njia ovu ya mikopo hewa.

Baadhi ya viongozi wa serikali wanaosimamia masilahi ya watumishi wanahusishwa na tuhuma hizi.

Wanadaiwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara kufanikisha mchezo huo. Waathirika wa fedha hizo ni wastaafu wa mwaka 2017/2018, na baadhi wa 2018/2019.

Habari za kiuchunguzi zinasema fedha hizo zimekuwa zikiingizwa kwenye mikopo hewa, isiyo na masilahi kwa wastaafu wala familia zao.

Katika malalamiko ya wastaafu 12, inaonyesha walikopa fedha kwa viwango tofauti.

Viwango hivyo vinaanza na mikopo yenye thamani ya Sh 19,990,000.

Uchunguzi unabainisha, kati ya miezi sita na minane, wastaafu hao walitakiwa kulipa riba ya Sh 143,837,750 (sawa na asilimia 719.5).

Ukiweka na deni mama, walilipa kiasi cha Sh 163,827,750, sawa na asilimia 819.5 ya mkopo waliochukua.

Ripoti ya kiuchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara imeeleza yote hayo.

Zilivyochotwa

Ripoti hiyo inasema, mstaafu mmoja (jina linahifadhiwa kwa sasa) wakati akisubiri mafao yake, inaonyesha alikopa Sh milioni 17.4.

Anatakiwa kulipa riba ya Sh milioni 88.6, sawa na asilimia 509.2, hivyo kufanya deni zima kuwa Sh milioni 108.

“Mifano mingine ni mstaafu aliyekopa Sh 2,490,000 na kutakiwa kulipa riba ya Sh 22,510,000 ambayo ni sawa na asilimia 904.

“Mstaafu mwingine ni aliyekopa Sh 2,100,000 na kutakiwa kulipa riba ya Sh 31,000,000, ambayo ni sawa na asilimia 1,476,” Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Alex Kuhanda, amesema.

“Mikopo hii ni ya muda wa miezi sita hadi minane,” amesisitiza Kuhanda, kiongozi wa Takukuru Mkoa wa Mara.

Wakati Takukuru ikieleza hayo, ofisa mmoja wa ngazi ya juu mkoani Mara alipoulizwa na JAMHURI kuhusu suala hili, amesema hajui.

“Mimi ndiyo nazisikia kutoka kwako,” amesema ofisa huyo anayetoka Ofisi ya RAS, huku akikataa kutajwa majina yake gazetini.

Hata hivyo, majina ya wastaafu waliotapeliwa yamehifadhiwa, kwa hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa wa sakata hilo.

Kupitia ripoti hiyo ya miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2019, Kuhanda amesema mpaka sasa fedha zinazofanyiwa uchunguzi na Takukuru ni takriban Sh bilioni 1.2.

Ametoa wito kwa wastaafu wote Mkoa wa Mara walioathirika na mfumo huo wa kitapeli kuelekea Takukuru.

“Wakopeshaji na mawakala wote, waliohusika na wanaoendelea kuwakopesha wastaafu mkoani Mara kupitia mtindo huu, wajisalimishe ofisi za Takukuru Mkoa wa Mara.

“Baada ya hapo, tutaanza operesheni maalumu na hakuna atakayebaki salama,” Kuhanda amesema.

Amewasihi watumishi waliostaafu na wastaafu watarajiwa kuchukua tahadhari juu ya utapeli huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, mara kadhaa ametafutwa na gazeti hili ili azungumzie suala hilo bila mafanikio.

Mabilioni mengine

Kwa mujibu wa habari kutoka Takukuru, Sh 13,303,312,747.75 zinatiliwa shaka matumizi yake mkoani Mara.

Mamilioni hayo ya shilingi yanahusisha miradi 17 ya maendeleo.

Duru zinasema tuhuma nyingine tano zinazofikia Sh 1,539,479,835 nazo matumizi yake yana utata. Tuhuma hizo zinachunguzwa na mamlaka ya Takukuru.

Zinagusa miradi kadhaa ya maendeleo, ukiwamo wa Hoteli ya Musoma na Kiwanda cha Sukari Tarime.

“Majalada haya yamekwisha kuwasilishwa kwa mamlaka za juu kwa maelekezo na hatua,” Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara amesema katika ripoti.

Gazeti hili limethibitishiwa kuwa, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara kwa sasa haijui kinachoendelea katika mpango wa ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Tarime.

Hata hivyo, kwa kipindi hicho cha miezi mitatu, Takukuru mkoani humo imeshinda na kushindwa kesi tatu, kati ya sita zilizokuwa mahakamani.

Kati ya kesi hizo sita zilizofikishwa mahakamani, moja kubwa ilihusu mradi wa maji Wilaya ya Bunda.

JAMHURI imeelezwa kuwa Sh 590,783,111.63 zimeokolewa na Takukuru kupitia uchenjuaji wa dhahabu Mkoa wa Mara.

Mwanza

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, ameitaja  Mahakama mkoani humo kuwa kinara wa malalamiko yanayohusu vitendo vya rushwa.

Amesema malalamiko 20 kati ya 122 yaliyopokelewa na Takukuru katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2019, yanaiegemea Mahakama.

Stenga amelitaja pia Jeshi la Polisi, idara za Afya na Elimu kuwa sehemu ya taasisi zinazochunguzwa.

“Serikali za Mitaa tumepokea malalamiko 18 ya tuhuma za rushwa,” amesema Stenga kupitia ripoti yake.

Amesema kwa kipindi hicho, majalada 10 ya uchunguzi yamefunguliwa. Kesi 32 zingali mahakamani.

“Kesi tisa zimetolewa maamuzi. Upande wa Jamhuri umeshinda kesi tatu.

“Hata hivyo, kesi mbili kati ya hizo (sita ilizoshindwa Jamhuri) zimekatiwa rufaa,” amesema Stenga.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu nchini, ametaka jamii kujitenga na rushwa.

Anataka wananchi hususan wanawake na vijana wasidanganyike na wagombea, kwani upokeaji rushwa una madhara makubwa.

“Tuchague viongozi wazalendo, wanaojali masilahi ya nchi yetu.

“Wananchi tushirikiane kuwafichua wale wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa, katika chaguzi mbalimbali,” amesisitiza Stenga.

757 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!