Si kila homa ni malaria! Kauli hii inapaswa kuzingatiwa hasa kipindi hiki ambacho ugonjwa wa homa ya dengue unatajwa kushika kasi jijini Dar es Salaam.

Serikali imethibitisha ugonjwa huo kusambaa kwa haraka katika wilaya za Ilala, Kinondoni na Ubungo.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wa maeneo hayo wametakiwa kuwahi katika vituo vya afya ama hospitalini wanapohisi mabadiliko katika miili yao ili wafanyiwe uchunguzi wa kitabibu.

Wakati Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile, akithibitisha uwepo wa ugonjwa huo, Aprili mwaka huu alisema: “Asilimia zaidi ya 70 ya homa tulizonazo si malaria, kuna UTI, homa ya matumbo, haya yote yanasababishwa na virusi.

“Na dengue ni moja ya ugonjwa unaosababishwa na virusi.” Virusi vya ugonjwa huu vinaitwa dengue na vinasambazwa na mbu aina ya Aedes.

Inaelezwa kuwa mbu huyu hupendelea kuishi karibu na makazi ya watu na huweza kumuuma binadamu mchana ama usiku.

Ugonjwa unaotokana na virusi vya mbu hao vinatajwa kuathiri nchi za kitropiki hasa Amerika ya Kusini na Afrika.

Katika juhudi za kudhibiti ugonjwa huo serikali imeshusha gharama za kupima homa ya dengue hadi kufikia Sh 15,000.

Kushushwa kwa gharama hizo kumetokana na vituo vya afya binafsi kutoa huduma ya kupima ugonjwa huo kwa bei ghali.

Kushuka kwa gharama hizo kumetokana na serikali kuingiza vifaa vya maabara vya kupima ugonjwa husika na kuanza kuvisambaza katika vituo vya afya.

Vituo ambavyo vipimo hivyo vimesambazwa ni pamoja na hospitali za Mwananyamala, Temeke na Vijibweni jijini Dar es Salaam pamoja na Hospitali ya Bombo, Tanga.

Ikumbukwe kuwa wakati serikali inathibitisha uwepo wa ugonjwa wa homa ya dengue nchini, watu 307 waligundulika kupata ugonjwa huo.

Kati ya hao, wagonjwa 252 walikuwa wakazi wa Dar es Salaam huku wengine 55 wakiwa wa mkoani Tanga.

Mpaka sasa wagonjwa waliothibitika kuugua ugonjwa huo wamefikia 1,237 huku vifaa vya maabara vilivyoletwa kwa ajili ya kupima ugonjwa huo vikitajwa kuwa na uwezo wa kupima wagonjwa kuanzia 1,870.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi, amesema wizara inatambua upimaji wa ugonjwa huo kuwa ghali hivyo wanawasiliana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuingiza ugonjwa huo katika orodha ya magonjwa yanayohudumiwa kwa bima hiyo.

Kutokana na ugonjwa huo kuenea kwa kasi Dar es Salaam, wananchi wametakiwa kufanya usafi wa mazingira kwa kuharibu mazalia ya mbu.

Profesa Kambi amesema kutokana na ugonjwa huo kuenezwa na mbu, serikali imeunda kikosi kazi cha wataalamu cha kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa wa dengue.

“Wakati jamii ikiendelea kuhamasishwa juu ya ugonjwa huo, serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa huo uliopo kwenye vituo maalumu,” anasema Profesa Kambi.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma na Kinga, Wizara ya Afya, Dk. Leonard Subi, anasema lengo la serikali ni kuhakikisha kusambaa kwa homa ya dengue kunapungua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wote wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo kupima.

Mfumo wa kufuatilia ugonjwa huo ambao umeanzishwa na Wizara ya Afya unatajwa kuwa imara na kwamba kupitia mfumo huo wizara inakusanya taarifa kutoka kila sehemu kuhusu ugonjwa huo.

Dalili za ugonjwa huu zinatajwa kufanana na ugonjwa wa malaria ambazo ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa, uchovu, maumivu ya viungo na misuli, kichefuchefu na kutapika.

Dalili nyingine za ugonjwa huo zikiwa ni maumivu ya macho pamoja na kupata muwasho na vipele vidogo.

Mpaka sasa hakuna dawa iliyogunduliwa kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo, japo wataalamu wanashauri mgonjwa wa homa ya dengue kupima afya kabla ya kuanza kutumia dawa za kutuliza maumivu, kunywa maji mengi na kupumzika vya kutosha.

Please follow and like us:
Pin Share