Mfanyabiashara maarufu nchini na kimataifa, Reginald Mengi, amekuwa na maisha yenye mengi, kuanzia mwenendo wake binafsi na mwenendo wake ndani ya jamii alimoishi.

Undani wa maisha yake umejibainisha katika kitabu chake cha hivi karibuni kinachoitwa “I Can, I Must, I Will” chenye kaulimbiu ya “The spirit of success”.

Mengi, katika kitabu hicho amepata kukizungumzia kifo, hasa baada ya kufariki dunia kwa mtoto wake, Rodney, ambaye anaamini kuwa ni mmoja wa waliomshawishi kukamilisha kitabu chake hicho.

Mengi: Siogopi kifo

Katika kukizungumzia kifo, Mengi alimjadili mwanawe huyo, Rodney, aliyefariki dunia Oktoba mwaka 2005, miaka 14 hadi kifo chake mzee Reginald Mengi.

Mzee Mengi ameandika: “Rodney, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, aliona fahari namna ambavyo nimeibuka kwa mafanikio makubwa kwenye tasnia ya biashara nikizishinda changamoto za umaskini.

“Aliona kwamba maisha yangu ni ya kipekee na yanatakiwa kuwa wazi kwa Watanzania na watu wengine duniani. Ushawishi wa Rodney kwangu ulikuwa wenye nguvu mno kiasi kwamba pale alipofariki dunia mtazamo wangu kuhusu mambo mbalimbali ya dunia ulibadilika. Sasa siogopi tena kifo.”

Mengi ni baba wa watoto watano, watatu akiwa amewapata kwa mkewe wa kwanza, Mercy ambaye amekwisha kufariki dunia. Watoto hao kwa mkewe wa kwanza ni Regina, Rodney na Abdiel. Watoto wake wengine wawili mapacha amewapata kwa mkewe wa sasa, Jacqueline, aliyefunga naye ndoa mwaka 2010, watoto hao ni Jayden na Ryan.

Alivyohusika mamlaka za maji

Mzee Mengi akiwa kiongozi wa kampuni binafsi ya masuala ya biashara na ukaguzi wa hesabu – Coopers and Lybrand Associates, mwaka 1982 aliongoza utafiti uliosababisha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji Mijini (NUWA), ambayo baadaye ilikuja kuzalisha Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka, Dawasco na sasa ni DAWASA.

Baadaye, msingi ukiwa utafiti huo ulioongozwa na mzee Mengi, zilianzishwa mamlaka nyingine za maji kwenye majiji na miji mikubwa.

Lakini zaidi ya hapo, kati ya mambo makubwa mengi aliyofanya mzee Mengi ni pamoja na utafiti wao kupitia Kampuni hiyo ya Coopers, kwa ajili ya Wizara ya Kilimo, wakilenga masuala ya usalama wa chakula.

Matokeo ya utafiti huo ni kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Nafaka – kwa sasa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Kisa chake na Mtikila

Katika kitabu chake, Mengi ameandika akirejea tukio la mwaka 1993. Anasema wakati huo mwanasiasa Christopher Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu kutaka kuruhusiwa mgombea binafsi katika kinyang’anyiro cha urais, ubunge na udiwani wakati wa uchaguzi, na akashinda kesi.

Hata hivyo, haraka serikali ilikabiliana na hukumu hiyo ya Mahakama Kuu kwa kufanya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania bungeni, mabadiliko ya 11 ya Katiba yaliyoharamisha uamuzi huo wa Mahakama.

“Kutokana na hilo, imebaki katika rekodi kwamba Mwalimu Nyerere alipinga hatua hiyo ya kufuta uamuzi wa Mahakama kwa kuifanyia mabadiliko Katiba.

“Kwangu huo uamuzi naona kama mgogoro wa wazi kati ya kile kinacholengwa na matakwa halisi ya demokrasia, na kile ninachoweza kukitazama kama msimamo usio wa kidemokrasia.

“Juhudi za Mtikila kutaka mgombea binafsi kwenye chaguzi za kisiasa hazikuishia hapo, na juhudi za serikali kuzima harakati zake hizo hazikuishia hapo, ziliendelea.

“Nalizungumzia hili kwa kuwa kumewahi kuwa na mtazamo miongoni mwa wanasiasa na watendaji wa serikali [kuwa] nilikuwa nyuma ya Mchungaji Mtikila kwa kuwa nilikuwa na nia ya kushiriki uchaguzi kama mgombea binafsi katika urais. Nilishangazwa sana na mitazamo na minong’ono hiyo,” anasema.

Kukwamishwa kibiashara

Mengi, katika maisha yake amekuwa akikumbuka matukio mengi ya kukamishwa, na mojawapo ambalo amelibainisha kwenye kitabu chake ni lile la mwishoni mwa mwaka 2000 alipoingia katika ushindani wa zabuni ya kununua Hoteli ya Kilimanjaro ya jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, hakuwahi kupewa majibu ya ombi lake hilo katika mazingira ambayo yanaweza kutafsiriwa kuwa kupuuza wawekezaji wazawa.

Anasema, licha ya kutokupewa majibu, baadaye alibaini hoteli hiyo imeuzwa kwa mwekezaji wa kigeni katika mazingira aliyoamini kuwa yamejaa utata.

Lakini pia anakumbuka machungu mengine. Anasema: “Mwaka 2013 nilipotangazwa na Jarida la Forbes, toleo la Afrika kuwa ni mmoja wa matajiri zaidi barani Afrika, kiongozi mmoja wa kisiasa hapa nchini wakati anahutubia mkutano wa viongozi wa dini uliofanyika Dar es Salaam mwaka uliofuata (2014) ikiwa katikati ya kilele cha msuguano kati yangu na Waziri wa Nishati na Madini kuhusu kupata leseni ya utafutaji gesi na mafuta [alinibeza].

“Alionyesha mtazamo wake kwamba niridhike na utajiri wangu, na kitendo cha kuendelea kusaka utajiri nitaonekana mtu mwenye ubinafsi na uroho. Sikuamini hayo, kwamba kiongozi mmoja mkubwa wa kisiasa anakuwa na mawazo yasiyo na mantiki.

 

Ushauri kwa wanasiasa

Moja ya ushauri wake kwa wanasiasa nchini ni kwamba, wasipambane na matajiri au utajiri wa watu, bali kinachotakiwa kufanywa ni kuhakikisha wanalipa kodi inayostahili, na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikusanye kodi hizo kwa haki.

Amepata kuhoji, unawezaje kuweka ukomo wa utajiri? Nani anaweza kuweka ukomo huo? Na anaweka kwa vigezo gani?

Mengi na Mwalimu Nyerere

Mzee Mengi amewahi kuguswa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika maisha yake.

Ameandika katika kitabu chake kwamba alivutiwa na ujumbe uliokuwamo kwenye kitabu cha Mwalimu Nyerere cha “Uhuru na Umoja”.

Katika kitabu hicho ujumbe uliomvutia Mengi ambao ameunukuu ni ule unaosema kwamba, kwa wale wenye ujasiri katika ushawishi, imani na juhudi katika kazi, Tanzania ni sehemu mwafaka.

Anasema maneno hayo kutoka kwa Mwalimu Nyerere miaka ya nyuma ni kati ya mambo yaliyomtia nguvu mno kusonga mbele.

Anasema Mwalimu Nyerere ndiye mfano mmojawapo halisi wa mantiki ya ‘I can’ moja ya maneno yaliyomo kwenye jina la kitabu chake. Anaeleza kwamba ‘I can’ ya Mwalimu Nyerere ilikuwa yenye nguvu mno kwa kuwa ilijitosheleza katika maono ya masafa marefu zaidi.

Mtazamo kifamilia

Katika familia, Reginald ni mtoto wa tano kati ya watoto saba wa mzee Abraham Mengi na mama Ndeekyo. Watoto wengine wa wazazi hao ni Apaansia, Elitira, Asanterabi, Karileni, Evaresta na Benjamin.

Amezaliwa katika familia maskini iliyokuwa ikimiliki ekari moja ya ardhi, na ikiishi katika ‘nyumba’ ya matope pamoja na mifugo; ng’ombe na kuku.

“Mama yangu alikuwa akidamka alfajiri, anakata mikungu ya ndizi, anaibeba kichwani na kutembea umbali wa kilomita tano kwenda soko la Kalali, Machame. Anauza ndizi hizo hapo sokoni na fedha inayopatikana ananunua bidhaa za nyumbani kwa ajili ya familia.

“Wakati mwingine aliweza kununua bidhaa za aina tofauti na kuziuza katika soko la Kalali, bidhaa kama ulezi.

“Wakati mwingine aliweza kuongezea thamani ulezi huo kwa kuulowesha usiku ili uwe na rangi ya kuvutia kwa wateja wake katika soko la Kalali. Kutoka katika soko la Kalali wakati mwingine alielekea soko jingine la kijiji cha jirani lililokuwa likiitwa Kombo, ambako aliuza ulezi wake kwa faida ndogo.

“Haikunishangaza, kwa mama yangu kupewa jina la ‘nkambusha’ kwa lugha ya Kichaga likiwa na maana ya mwanamke mfanyabiashara.

Mama yangu alikuwa mchapakazi hodari, aliyejitoa kwa ajili ya familia yake na kwa ujumla, alikuwa mjasiriamali kwa viwango vya maisha ya kijijini.

“Baba yangu pia alikuwa mfanyabiashara, alikuwa akinunua mbuzi, anawaosha kwa brashi kisha kuwauza kwa faida, kwa kuwa wanakuwa katika kiwango cha juu.

“Wazazi wangu walikuwa wachapakazi, wenye maadili na wanaoheshimiwa na jamii inayowazunguka, walikuwa wenye msaada kwa wenye mahitaji, imekuwa kama fumbo, kwamba licha ya umaskini wa familia yetu [tuliweza kusaidia].

“Mara kwa mara nilishuhudia mama yangu akiwapa chakula kidogo alichopika kwa ajili ya familia yake watoto maskini wa majirani. Wazazi wangu walijaliwa moyo wa kujitolea kwa wengine. Naamini nimekuwa nikifanya shughuli zangu katika mwelekeo wa uadilifu na kiutu, mambo niliyojifunza kwa mifano kutoka katika maisha ya wazazi wangu.

“Lakini vilevile kuna mengi kutoka katika maisha yangu ya utoto yanayoendelea kuninyoosha maishani. Kaka yangu, Elitira ni mshawishi na mwalimu mkubwa wakati wa ujana wangu, nitatoa mifano kadhaa katika hili.

“Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, Elitira aliwafuata wazazi wetu na kuomba pesa ili akanunue mayai matano. Akayanunua mayai hayo na kuyachemsha. Akala yai moja kama chakula cha mchana na yale mengine manne akayauza kwa wanafunzi wenzake.

“Kinachovutia hapo ni kwamba kila anapopata faida anaongeza idadi ya mayai kwa ajili ya kuuza, matokeo yake, mtaji wake uliongezeka na hakurudi tena kwa wazazi kuomba pesa.  Elitira alijifunza somo la kuweka akiba na kuwekeza.

“Kuna wakati biashara yake hiyo ya mayai ilikua zaidi hadi akapata soko kwenye kambi ya jeshi iliyokuwa umbali wa kilomita kadhaa kutoka nyumbani.

“Siku za mwishoni mwa wiki usiku alikuwa akienda kambi ya jeshi kupeleka mayai na asubuhi anarejea nyumbani akiwa amenunua kutoka huko sigara kuja kuuza, kwa kuwa huko (jeshini) alikuwa akinunua kwa bei nafuu zaidi.

“Akirejea kijijini aliuza sigara au bidhaa nyingine aliyonunua huko jeshini na kupata faida. Alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kubaini fursa na kuzitumia kufanya biashara. Usiku mmoja akiwa anapeleka mayai jeshini, alikimbizwa na simba, aliweza kunusurika kwa kuwa alipanda juu ya mti lakini mayai yakavunjika, hata hivyo hakutaka tamaa baadaye alirejea tena kwenye biashara.

“Kwa mfano, kuna wakati alijiunga jeshini akiwa kijana wa kujitolea, baada ya kukubaliwa akabaini kila askari anatakiwa gwaride la asubuhi akiwa amevaa viatu (buti) vilivyong’aa.

“Basi akaamua kuwa mng’arisha viatu (shoe shine). Usiku aling’arisha viatu vya askari na walikuwa wanamlipa mwisho wa mwezi kutoka katika mishahara yao kiasi kwamba alipoondoka jeshini miaka kadhaa baadaye alipata mtaji wa kufungua duka dogo.

Mwapachu anavyomkumbuka

Mmoja wa viongozi waliowahi kufanya kazi kwa karibu na Mengi ni aliyepata kuwa katibu mkuu, waziri na mkuu wa taasisi mbalimbali za kitaifa nchini, katika serikali kuanzia ya Mwalimu Nyerere hadi ile ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, Harith Mwapachu.

“Mengi alikuwa rafiki yangu, tumefanya kazi nyingi tangu nikiwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Biashara za Nje. Mwaka nadhani 1975 akiwa Meneja Mtendaji wa Kampuni ya Coopers and Lybrand walipewa kazi ya kukagua na kuweka mifumo ya kihasibu kwa kampuni za biashara za serikali.

“Baadaye nilipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Umeme na Madini nilimwita kupitia taasisi yake kutazama na kuweka mifumo juu ya masuala ya huduma ya maji. Ndipo baadaye kutokana na kazi yao, tukaunda mamlaka za maji za miji, ndizo hizi zinazoendelea sasa.

“Hata nilipokwenda Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) mwaka 1981 alitusaidia kuweka mifumo ya kihasibu katika taasisi hiyo.

“Nathubutu kusema Mengi amefanya kazi kubwa zaidi kusaidia kujenga mifumo ya kitaasisi katika taasisi za serikali. Lakini amekuwa hodari katika biashara zake.

“Nakumbuka wakati fulani alisaidia sana katika mpango wa ‘import substitution ’(kuzalisha bidhaa za ndani kama mbadala wa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi). Kampuni zake zilifanya kazi kubwa,” anasema Mwapachu katika mahojiano na Gazeti hili la JAMHURI.

Katika hatua nyingine, mdau wa maendeleo nchini Renatus Mkinga amemzungumzia Mengi kama mmoja wa wafanyabiashara wa mfano nchini katika uaminifu wa kulipa kodi.

“Sikuwahi kumsikia katika kashfa za kukwepa kodi. Amekuwa mstari wa mbele kusaidia wasiojiweza, amepata kusaidia hata waliopatwa na matatizo. Lakini amewahi kuwa shujaa katika kupinga ufisadi miongoni mwa wafanyabiashara wenzake. Tunamkumbuka kwa mengi,” anasema Mkinga.

Mengi amefariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, mwaka huu Dubai, UAE. Taratibu za kutoa heshima za mwisho kwa mwili wake zitafanyika Jumanne (leo), na anatarajiwa kuzikwa Alhamisi (kesho kutwa) kijijini kwao Machame, mkoani Kilimanjaro.

Please follow and like us:
Pin Share