Felix Wazekwa alitumia ndumba kuvuta mashabiki wa muziki


MOSHY KIYUNGI
Félix Wazekwa ni mwanamuziki mwenye mbwembwe wakati akiwa jukwaani,
akiimba huku akiongoza safu ya wanenguaji.
Mtindo wa unenguaji wanaoutumia ni wa aina yake, ambao haulingani na mitindo
mingine yoyote ya wanamuziki wa huko Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo (DRC).
Majina yake kamili anaitwa Feleix Nlandu Wazekwa S’Grave. Alizaliwa Septemba
1, 1962 katika jiji la Kinshasa, (DRC).
Alianza kujiingiza mzima mzima kwenye muziki wa kujitegemea mwaka 1995
baada ya kushauriwa sana na Papa Wemba.
Felix Wazekwa alifanikiwa kutoa albamu yake ya kwanza kwa msaada wa Papa
Wemba na Madilu System. Baada ya hapo akaanza kukusanya wanamuziki katika
jiji la Kinshasa ili kuunda bendi.
Yaelezwa kwamba mafanikio yake hayo yametokana na ushauri mkubwa
aliopewa na Papa Wemba, aliyemuhimiza kwanini asiwe mwimbaji moja kwa
moja, ikizingatiwa uwezo wa kutunga na kuimba nyimbo anao.
Alikubaliana na ushauri huo, akaamua kuanza kuimba na kuwa mwanamziki wa
kujitegemea mwaka 1996.
Historia yake katika muziki inaonesha kwamba, alianza kujifunza muziki miaka ya
1982 na 1983 akiwa na kundi la vijana ya Kin Verso, kwenye Manispaa ya Matete
jijini Kinshasa.
Mwaka 1985, Wazekwa alipata fursa ya kwenda Paris nchini Ufaransa, kwa ajili
ya kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu, akisomea masuala ya uchumi.
Mwaka 1990 kipaji chake katika muziki kilianza kuonekana kukua baada ya
kutunga za nyimbo kadhaa zilizomfanya kufahamika na watu wengi.
Kwenye miaka ya 1991 na 1993, Wazekwa alishirikiana na kiongozi wa kundi la
Quartier Latin, Koffi Olomide.
Akiwa na kundi hilo, alichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya albamu za
Haut De Gamme, Koweit Rive Gauche na Noblesse Oblige.
Kati ya mwaka 1993 na 1995, alishirikiana na Papa Wemba kutengeneza albamu
za Foridoles na Pole Position.
Aidha, alitoa ushirikiano wake kwa baadhi ya wanamuziki na makundi mengi
mbalimbali kama Soukous Stars, Damien Aziwa, Djeffard Lukombo, Bibidens na
Duc Herode.

Mtindo anaotumia kunengua akishirikiana na wanenguaji wengine wa kundi hilo,
ni wa aina yake ambao huwavutia watu wengi. Ana sauti nzito aimbapo, ni
mtanashati ajuaye kuyapangilia mavazi wakati wote.
Mwaka 2001, Wazekwa alitoa albamu ya Signature, iliyopokewa vizuri na
wapenzi wa muziki wa rhumba.
Mwanamuziki huyu alipachikwa majina bandia ya ‘Mokua Bongo’, ambayo alipewa
na mashabiki wake kuelezea kiwango cha busara za kisomi alizonazo mtaalamu
huyo. Hufahamika zaidi kutokana na aina yake ya uimbaji, huku akitumia sana
methali na mafumbo.
Kwenye albamu ya Pauvre Mais Felix Wazekwa alitamka maneno haya: “Un idiot
on lui montre le Soleil, mais lui regarde le doigt” Kwa lugha yetu ya Kiswahili
yanatafsirika kuwa “Mtu mjinga unapomuonesha wapi lilipo jua, yeye huishia
kutizama kidole.”
Baadhi ya albamu ambazo zimetolewa na guli huyo ni Tétragramme, YHWH ya
mwaka 1995, Pauvres Mais ya mwaka 1997, mwaka 1998 aliachia albamu ya
Bonjour Monsieur na Sponsor nayo ilitolewa mwaka 2000.
Pia, Signature ya 2001, Yo nani ya 2002, Et après ya mwaka 2005, La chèvre de
Monsieur Seguin, Que demande le peuple L’intégral Des 2009, Faux mutu moko
boye ya mwaka 2006 na Que demande le peuple ilifyatuliwa mwaka 2008.
Wazekwa aliendelea kuachia albamu nyingine za Mémoire ya Nzambe ya mwaka
2010, Haut les Mains ya mwaka 2011 na Single za Adamu na Eva aliaitoa mwaka
2013.
Aliendelea kutengeneza albamu lakini hazikuwa zenye mafanikio kutokana na
muziki wake kuwa mgumu. Wengi waliuona kana kwamba umekaa kisomisomi
sana, kiasi kutopata umaarufu sana kwa wapenzi wakubwa wa muziki ambao ni
watu wa kawaida.
Lakini, aliweza kutambulika na wataalamu wa muziki kwamba anafanya muziki wa
ukweli lakini sokoni hali haikuwa nzuri. Nguli huyo hakukata tamaa akaendelea
kufyatua albamu zaidi chini ya uzalishaji ya JPS Productions.
Pamoja na kuyafanya hayo, hali ikawa ile ile isiyo ya kuridhisha ama mbaya mno
katika soko la muziki, kutokana na sababu iliyotajwa hapo juu. Pia, kulikuwa na
hujuma ambazo yasemekana alikuwa akifanyiwa fitna na Koffi Olomide.
Kampuni ya uzalishaji ya JPS haikuridhishwa kabisa na kusuasua kwa albamu za
Wazekwa zikiwa sokoni, kwa kuwa walikuwa wakijua anafanya muziki wa ukweli
bado wakaendelea kumvumilia na kumpa muda zaidi.
Baadaye rafiki yake mmoja wa karibu akiitwa Kaffe Etienne Tshimanga,
akamfuata na kumweka kitako kisha akamg’ata sikio kwamba muziki wa Kongo
bila ushirikina hutofanikiwa kamwe.
Tshimanga alimshauri kuwa ni lazima aanze kutumia uchawi, lakini akakumbana
na upinzani mkali kutoka kwa Wazekwa, msomi huyo wa uchumi, mtu mwenye
imani kali sana katika dini yake ya Kikristo.

Baada ya ushawishi mzito yaelezwa alikubali ushauri huo, ambapo albamu yake
baada ya kufanya ushirikina ilitoka 2001 kidogo ikapata mafanikio.
Wazekwa bado hakuridhika na mafanikio hayo madogo akawa anapanga
kuachana na muziki baada ya kuona amejitoa sana lakini mafanikio hayaridhishi
kabisa.
Tshimanga aliendelea kumtia moyo ‘akomae’ kwenye gemu atatoka tu. Baadaye
kidogo akapata bonge la mkataba na Primus. Hapo akapata moyo wa kufanya
kazi zaidi na kuanza kuona mwanga wa mafanikio huku washabiki nao wakianza
taratibu kumfuatilia na kumkubali.
Pamoja na mafanikio hayo, baadhi ya wanamuziki wakubwa wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo hawakumhesabu kama ni mmoja wa wanamuziki tishio
au mshindani kwao.
Mwaka 2004, Tamasha la Fikin kamati yake ya ushindi ikiongozwa na Tshimanga,
ikajipanga vilivyo kwenye mambo ya ushirikina wakiamini hii ndiyo nafasi ya mtu
wao kutoka na kuheshimika na wanamuziki wakubwa wa DRC, kama ni mmoja
wa wanamuziki wakubwa.
Wafadhili wakaanza kuwekeza pesa nyingi kwake kwa lengo la kushindana na
wapinzani wao wakubwa wanaozalisha product kama ya kwao SKOL (Primus na
Skol ni kampuni za bia), lengo kubwa likiwa ni kumfunika Ngiama Werrason
ambaye alikuwa akidhaminiwa na SKOL.
Werrason siku moja baada ya kukutana uso kwa uso na Wazekwa, baadaye
alimtumia ujumbe mzito Tshimanga kwamba asifanye tena mchezo alioufanya
jana yake.
Tshimanga akawa anasakwa na Mawerrason, ikabidi alikimbie jiji la Kinshasa,
huku nyuma tayari ikiwa kumuachia ushindi mnono Wazekwa. Tangu wakati huo,
wanamuziki wote wakubwa wakaanza kuhofia kupambana naye ana kwa ana
jukwaani.
Lakini taarifa ilipo hivi sasa ni kwamba Wazekwa na Tshimanga, si marafiki tena.
Hivi karibuni Wazekwa ameachia wimbo mpya wa Bouffer Moi Tout.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0713331200, 0784331200 na
0767331200.