Na Angalieni Mpendu
“Kweli nimeomba nipumzike kwa sababu, nimekitumikia chama changu muda
mrefu, nimeona niachie damu mpya. Nimependa nipumzike, lakini hayo mengine
yanayoandikwa ni ya kupuuza.”
Ni kauli thabiti iliyojaa hiari na uungwana; na iliyoshiba haki usawa na ahadi
kutoka moyoni mwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (2012-
2018), Abdulrahman Kinana, alipozungumza na gazeti JAMHURI, wiki iliyopita.
Kupenda kupumzika, kukitumikia chama na kuachia damu mpya ni sababu nzito
zilizomsukuma Abdulrahman Kinana kumwomba Mwenyekiti wa CCM na Rais,
Dk. John Pombe Magufuli, amruhusu kustaafu uongozi katika chama. Ombi
limekubaliwa.
Sababu hizi ni picha kamili inayotambulisha Watanzania jina Abdulrahman ni
mtumishi wa watu aliyejaa rehema. Si mchoyo wa madaraka, si mwenye hiana wa fadhila ya umma na si mdhulumati wa ahadi za majira ya vijana.
Kumbuka anaponena “nimeona niachie damu mpya.” Asante, kapumzike salama.
Abdulrahman Kinana anapongezwa na kuenziwa ndani ya chama, ndani ya
Tanzania na kwa majirani wa jumuiya ya Afrika Mashariki si kwa kisomo chake tu, bali ni kwa uzalendo wake na uwezo mkubwa wa kuchapa kazi popote
anapopangiwa kazi.
Aah! Wasaa ni mchache na nafasi ni haba kuandika ninavyofahamu utendaji
wake wa kazi na utu alionao tangu alipokuwa katika Umoja wa Vijana wa TANU,
TANU, CCM, bungeni na serikalini. Itoshe kusema ni kiongozi mkweli, mvumilivu,
jasiri, mpole na mpenda haki.
Tunampenda Kinana si kwa sura yake au umbo lake, ama rangi yake wala kabila
na dini yake tu; ni kwa sababu ya uongozi wake maridhawa na wa kutukuka.
Ndiyo maana Watanzania tunahoji ni nani vitamtosha viatu alivyoviacha Chama
Cha Mapinduzi?
Jibu laweza kuwa yupo anayeweza kuvivaa. Lakini viatu hivi vina sifa mbili;
kubana na kupwaya. Vikimbana ataumia. Lakini ataweza kutembea na kukosa
furaha ya kuvaa viatu. Na watu watamuona bwege na kumcheka muda wote.
Vikimpwaya hataweza kutembea sawa sawa na kupendeza mbele ya watu.
Atakuwa kichekesho viatu vitakapomvuka njiani. Kwa hiyo, mkabidhi viatu kwa
mvaaji hana budi kuwa mweledi na makini kwa sababu viatu vina mfumo wake
katika matembezi.
Ndiyo maana Mwenyekiti wa CCM na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, alikataa
rasmi mara mbili ombi la ndugu yetu Abdulrahman Kinana la kustaafu uongozi
katika chama. Magufuli alikuwa anatafuta mwanaCCM ambaye akivaa viatu vitamtosha.
Naam, hatimaye viatu vimempata mvaaji mpya ambaye ni msomi na mhadhiri wa
sayansi ya siasa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Ni
mbobezi na mchambuzi wa masuala na mijadala ya siasa. Huyu ni Dkt. Bashiru
Ally Kakurwa.
Chama Cha Mapinduzi, Watanzania na wazalendo wana matarajio na matumaini
makubwa kwa Katibu Mkuu wa CCM mpya, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, atafuata
pasi na shaka nyayo za mtangulizi wake, Kinana, na yeye mwenyewe kuweka au
kupasua njia mpya kuleta mabadiliko ndani ya chama na kujenga Tanzania mpya.
Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, anasema, “Siasa yetu inaongozwa kwa
misingi ya maadili, kwa misingi ya Azimio la Arusha. Kujenga jamii kubwa ya
kijamaa, kujenga chama ambacho ndicho kitakacholenga jamii hiyo na
wanachama madhubuti na kuweka misingi ya Taifa na kujitegemea.”

2634 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!