FIFA kufanya mapinduzi ya soka

Rais mpya wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amekuja na mapendekezo mapya ya kutaka kufanya mabadiliko katika mchezo wa soka.

Baada ya kuongeza timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2026 na kufikia 48, Rais huyo amekuja na mapendekezo mapya jinsi anavyotaka soka liendeshwe.

Katika ujumbe alioutoa kupitia Mkurugenzi wa Ufundi wa FIFA, Maco van Basten, amependekeza sheria mpya katika mchezo huo akilenga kutaka kuboresha mchezo huo unaopendwa na wengi duniani.

Katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Bild, Van Basten anasema wanawaza kuondoa sheria ya kuotea (mchezo wa kuzidi) katika soka.

“Sipati picha, soka isipokuwa na sheria ya kuotea (offside), washambuliaji watapata nafasi nyingi sana za kufunga,” anasema mkurugenzi huyo wa ufundi.

Anasema mchezo huo utakuwa wa kuvutia sana kama offside itaondolewa na anaamini jambo hilo litawafurahisha mashabiki na washambuliaji.

Van Basten pia anaona kuna haja kubwa kwa FIFA kubadili aina ya upigaji wa penalti, ambako kwa sasa adhabu ya penalti mchezaji anauweka mpira mita kadhaa karibu na goli na kuupiga.

Katika mapendekezo hayo ya kubadilishwa kwa aina ya upigaji wa penalti, Van Basten anataka mpiga penati aweke mpira mita 25 kutoka kwenye goli na ikiwezekana kama anaweza atembee nao kuelekea golini kwa muda usiozidi sekunde nane.

Aina hii ya upigaji penalti siyo ngeni katika mchezo wa soka, kwani mwaka 1999 ilishafanyiwa majaribio nchini Marekani, na pia kuna mapendekezo ya kupunguzwa kwa adhabu ya mipira ya kunawa.

Van Basten anaona kuwa adhabu ya kadi nyekundu ni kali mno kwa tukio kama hilo, kwani analiona kama tukio dogo lisilohitaji kadi nyekundu na kwamba adhabu hiyo ipunguzwe.

Anasema kusitolewe kadi nyekundu mpira ukishikwa kama ilivyotokea kwa Luis Suarez mwaka 2010 wakati wakicheza dhidi ya Ghana, aliposhika mpira uliokuwa ukiingia golini na badala yake iwe kadi ya njano.

Anapendekeza nahodha awe mtu pekee kuongea na mwamuzi, akitoa mfano wa mchezo wa raga (rugby) ambao kapteni pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuongea na mwamuzi.

Katika mapendekezo hayo pia kuna kipengele cha kupunguzwa kwa idadi ya mechi kutoka 80 hadi 50, na hii inaweza kuwa suluhisho kwa malalamiko ya siku nyingi kwa makocha wengi hasa katika Ligi Kuu nchini Uingereza.

Alianza Van Gaal akiwa katika Klabu ya Man United, akaja Jurgen Klopp – walilalamikia idadi ya mechi kuwa nyingi EPL. Van Basten anataka idadi ya mechi ipunguzwe kutoka mechi 80 hadi 50 kwa msimu.

Kuongeza idadi ya wachezaji wanaobadilishwa wakati wa mechi, Van Basten anatamani kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba (substitutes) kuanzia watano hadi saba.

Kwa muda mrefu wadau wa soka wamekuwa wakizungumzia kuhusu suala la kuongeza wachezaji wa akiba, na sasa FIFA inatarajia kuliangalia suala hilo.

Mapendekezo haya yaliyotolewa na mkurugenzi huyu wa ufundi, yanatarajiwa kuwasilishwa katika kamati ya FIFA kwa ajili ya kujadiliwa.