Serikali inapodhamiria kukandamiza wanyonge

 

Kuwapandishia nauli watu wanaoshinda na kulala na njaa ni sawa na kuwachimbia kaburi; maana sasa watashindwa kwenda kujitafutia riziki ya kujikimu na familia zao, na hatimaye watakufa kwa kukosa chakula.

Watanzania wengi ni walalahoi wasiojiweza kiuchumi, kiasi cha kulazimika kushindia mlo mmoja badala ya milo mitatu kwa siku, kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.


Hata hivyo, Serikali yetu pamoja na kufahamu ukweli huu, imetoa mwanya kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kupandisha nauli.


Wiki iliyopita, uongozi wa Sumatra ulitangaza kupandisha nauli za daladala, mabasi yaendayo mikoani, treni, meli na feri kuanzia Aprili 12, mwaka huu.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Ahmad Kilima, alitangaza kwamba nauli ya daladala imepanda kwa ongezeko la Sh 100 kwa wakubwa na Sh 50 kwa watoto/wanafunzi. Kwamba nauli hiyo imepanda kutoka Sh 300 hadi 400, Sh 350-450, Sh 500-600, Sh 650-750 kwa wakubwa kutegemeana na umbali wa safari, na Sh 200 kwa wanafunzi bila kujali umbali wa safari mijini.


Nauli ya mabasi yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na mikoa mbalimbali, imepandishwa kwa kiwango cha kati ya Sh 8,000 na 21,000. Kwa mfano, nauli ya basi la hadhi ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza imepanda kutoka Sh 40,000 hadi Sh 61,400.

 

Kwa upande wa usafiri wa reli, Sumatra imepandisha nauli ya treni za mikoani kwa ongezeko la kati ya Sh 6,000 na 15,000. Kwa mfano, nauli ya treni ya daraja la kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma imepanda kutoka Sh 60,599 hadi 75,700.

 

Sumatra imeridhia pia ongezeko la asilimia 34.3 ya nauli kwa vyombo vya usafiri wa majini vinavyotumia bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Uongozi wa Sumatra umeagiza kuwa kupanda kwa nauli kutekelezwe sambamba na utoaji huduma bora, lakini jambo la kushangaza ni kwamba hatujaona uboreshaji wa huduma za usafiri wa vyombo hivyo.

 

Hili linathibitishwa na wadau wengi akiwamo Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, ambaye anasema:

 

“Nauli zimepanda bila huduma kuboreshwa, nadhani hiyo ilikuwa hoja ya msingi ya Sumatra kukataa kupandisha nauli.


Watanzania ni maskini, na hivi sasa kila kitu bei yake iko juu, leo tena nauli zinapanda, hapa tunajenga taifa la walalahoi.”


Madai ya kwamba kupanda kwa nauli hizo kumetokana na msukumo wa kupanda kwa bei ya vipuri vya magari hayana uzito, kutokana na ukweli usiopingika kwamba mfanyabiashara siku zote anachotaka ni kupata faida kubwa zaidi na ikiwezekana aone kila shilingi yake moja inazaa nyingine kumi na kuendelea.

Serikali siku zote imekuwa ikiruhusu upandishaji wa nauli, lakini haijapata kuwa na ujasiri wa kusimamia kuhakikisha pindi vipuri na mafuta ya vyombo husika vinaposhuka bei nauli nazo zinashuka.

 

Sasa, pengine Serikali yetu imelewa madaraka, kiasi cha kusahau kwamba mwajiri wake mkuu ni hawa wananchi wa kawaida kama si wanyonge inaowaacha wakiendelea kupigika kiuchumi na kimaisha.

 

Binafsi siwezi kuamini kuwa Serikali yetu haina uwezo wa kuzuia upandishaji huu wa nauli unaowaongezea wananchi kero, katika kipindi hiki ambacho tayari wanalizwa na mfumko wa bei za bidhaa mbalimbali unaoendelea kushika hatamu nchini.

 

Fikra ya Hekima inalitazama moja kwa moja suala la kupandisha nauli kipindi hiki, kama hatua mojawapo ya kupanua wigo wa tabaka kati ya wenye nacho na wasio nacho, maana lina sura ya kuwakandamiza wananchi wanyonge na kutoa mwanya kwa matajiri kujineemesha zaidi. Hii ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu!


Enyi Sumatra, Wizara ya Uchukuzi na Serikali kwa jumla, watazameni Watanzania wanyonge kwa jicho la huruma.

By Jamhuri