Watanzania tujitambue zaidi

Kabla ya kuzungumzia mada tajwa hapo juu, nichukue nafasi hii kuwashukuru wasomaji waliotoa maoni na mitazamo yao mbalimbali, kuhusu makala niliyoyaandika wiki iliyopita, yaliyokuwa na kichwa cha habari “Godbless Lema acha kuwa ndivyo sivyo.”

Watu wengi wamenitumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), baadhi wakinikosoa vikali na wengine wakiniunga mkono kulingana na wanavyofahamu uhalisia wa nilichokizungumza.

 

Kimsingi, nimejifunza mengi kutokana na SMS hizo. Kikubwa zaidi nimegundua kuna watu wasiotaka kukosolewa daima. Ukisema ukweli kuhusu wanasiasa; na ukweli huo usipokuwa na maslahi nao wanakuchukia kama si kujenga kinyongo dhidi yako! Hata hivyo, ninaheshimu uhuru wa kutoa mawazo, maoni na mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali.

 

Leo nimeona vema kuzungumzia umuhimu wa Watanzania kujitambua zaidi katika kipindi hiki cha mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na ushindani wa kimaisha.

 

Kwa muda mrefu sasa Watanzania wengi wameonekana kutotambua umuhimu na wajibu wao katika ujenzi wa taifa letu kwa maslahi ya umma.

 

Wengi hawajitambui wala kujiamini kuwa ndiyo wenye nchi na wenye wajibu na haki ya kulinda na kunufaika na rasilimali zilizopo.

 

Wapo wananchi waliojiweka kando na kuamini kimakosa kwamba ni watu fulani tu ndiyo wanaofaa na wenye haki ya kuwasemea wengine, kulinda na kusimamia rasilimali za nchi yetu.

 

Wengi wamekosa ujasiri wa kujitokeza kukosoa na kukemea utendaji mbovu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa wanasiasa na watumishi wengine wa umma.

 

Ndiyo maana matatizo yameendelea kuongezeka katika jamii, licha ya kuwapo wanasiasa na watumishi wa Serikali wanaotoa tambo za kuyatokomeza bila mafanikio.

 

Chuki na maslahi binafsi vimetawala mioyo ya watu kiasi cha kushindwa kujitambua kuwa wana uwezo wa kuyafanya matatizo lukuki, yanayotunyima maendeleo kubaki historia hapa nchini.

 

Kasumba ya kuamini kuwa ni watu fulani pekee ndiyo wenye jukumu na uwezo wa kufuta matatizo yaliyopo, itatudumisha katika umaskini badala ya kutuinua kiuchumi na kuboresha maisha yetu.

 

Ni dhahiri kuwa viongozi wetu katika nyanja mbalimbali wameshatambua udhaifu huu wa Watanzania walio wengi, ndiyo maana wameendelea kuhujumu mali za umma na kuzitumia kujineemesha na familia zao kwa kujilimbikizia utajiri uliokithiri.

 

Wananchi wengi wameshindwa kutafakari maneno na matendo ya viongozi wetu, iwapo kweli yana dhamira ya dhati na dalili za kutusaidia kufuta umaskini unaotuzingira.

 

Viongozi ambao siku zote wanaahidi kutuletea maendeleo ya kweli ndiyo hao hao tunaowashuhudia wakizidi kujiongezea mishahara, marupurupu na posho.

 

Wanatumia fedha za umma kujijengea nyumba na kujinunulia magari ya kifahari, bila kujali kuna familia nyingi za Watanzania zisizo na uwezo wa kujigharamia chakula, matibabu na elimu.

 

Tumeshindwa kuwaadhibu viongozi wa aina hiyo, kwa kosa la kuendelea kutuambia maneno mengi matamu mithili ya asali kuliko matendo. Kwanini tuendelee kuwa watumwa wa wanasiasa na kuwaona kama wafalme na miungu-watu?

 

Umefika wakati Watanzania tujitambue zaidi. Tuweke kando ushabiki wa kisiasa usio na tija kwa umma. Tuwahoji viongozi wetu watueleze ni lini watasimamia na kutumia kwa uadilifu rasilimali za nchi ziweze kumnufaisha kila mmoja wetu.

 

Hatuna sababu ya kuendelea kutojitambua, tuna haki ya kufuatilia mienendo ya viongozi wetu, kuwakemea na kuwakosoa pale tunapoona wameendelea kujikita katika ahadi hewa za kutuondolea matatizo yanayotunyima maendeleo miaka nenda miaka rudi. Tujitambue zaidi.

1094 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!