Mbunge Nyimbo kanena,

Rais apewe kipaumbele

Hivi karibuni, Mbunge wa Viti Maalumu, Tauhida Cassian Nyimbo (CCM), alivishauri vyombo vya habari kujenga dhana ya kuzipatia kipaumbele habari za Kiongozi wa Nchi, Rais.

Nyimbo alitoa changamoto hiyo bungeni mjini Dodoma, wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

 

Alikosoa vyombo vya habari vya hapa nchini vinavyoandika na kutangaza habari kwa upendeleo, ikiwa ni pamoja na kutotoa fursa pana kwa Mkuu wa Nchi.

 

Kwamba habari zinazomhusu Rais mara nyingi zimekuwa hazipewi uzito wa juu katika vyombo vingi vya habari ikilinganishwa na za watu wengine.

 

“Vyombo vyetu vya habari vimekuwa vikifanya kazi kwa upendeleo mkubwa, tena hili linasikitisha, wakati mwingine habari za Rais wetu hazipewi uzito,” alisema Nyimbo na kuongeza:

 

“Katika taarifa zao za habari utakuta habari ya Rais ni ya tatu, ya nne, au ya mwisho, na katika magazeti utakuta habari ya Rais imewekwa ndani.

 

“Hii si haki Mheshimiwa Spika, hatumtendei haki Rais. Mimi nashauri ili kumtendea haki, habari zinazomhusu Rais ziwe za kwanza, halafu habari nyingine zifuate.”

 

Tunaweza kusema huo ni mtazamo wa Mbunge Nyimbo, lakini umebeba ujumbe mkubwa na muhimu kwa Taifa. Binafsi ninamuunga mkono kwani ameonesha uzalendo mkubwa kwa nchi yetu. Sitaki kuamini kuwa kauli hiyo ya mbunge Nyimbo ina madhara katika uhuru wa vyombo vya habari.

 

Kwa ukweli usiopingika Rais ndiye mtu mwenye dhamana kubwa kwa wananchi kuliko mwingine yeyote. Ni kiongozi mwenye hadhi ya pekee katika Taifa.

 

Kwa mantiki hiyo, wananchi wangependa; na wana haki ya kujua na kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa Rais wao. Vyombo vya habari ndivyo vyenye uwezo wa kukidhi kiu hii ya wananchi.

 

Baadhi ya wananchi wamekuwa wakimshutumu Rais kwamba hawajibiki ipasavyo katika kushughulikia masuala yenye maslahi kwa umma. Wengi wao wamelishwa upotoshaji huo na wanasiasa na wanaharakati wanafiki, wenye chuki binafsi na wasiolitakia mema Taifa letu.

 

Baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamekuwa wakimtangaza Rais mbele ya umma kwamba ni mtu wa kutalii katika mataifa mbalimbali. Lakini hawaelezi madhumuni ya safari hizo za nje ya nchi na manufaa yake kwa Watanzania. Huo ni unafiki tu.

 

Lakini Rais wetu (pamoja na kwamba hakosi upungufu ya kibinadamu) si kweli kwamba hajizatiti kutafuta maendeleo ya waajiri wake (wananchi). Tatizo hapa ni kwamba baadhi ya mambo anayoyafanya kwa manufaa ya umma ama hayatangazwi kwa uzito unaostahili, au hayajulikani kwa wananchi wengi.

 

Idadi kubwa ya vyombo vya habari siku hizi vimejikita katika kuandika habari zinazoelezea matatizo yanayolikabili Taifa. Hili ni jambo zuri na linalostahili pongezi. Lakini pia hata maendeleo yanayopatikana kutokana na juhudi za viongozi wetu nayo yanastahili kutangazwa yajulikane kwa wananchi wengi kama si wote.

 

Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari ni kama vimesahau kuwa habari za Rais nazo ni hitaji muhimu kwa wananchi. Watanzania wanahitaji kujua kiongozi wao wa nchi anashughulikiaje matatizo yanayozikabili sekta mbalimbali zikiwamo nishati na madini, kilimo, mifugo, afya, elimu, utalii na kadhalika.

 

Wananchi wakijionea na kujua mwenendo wa utendaji wa Rais wao wanakuwa na nafasi nzuri ya kumhukumu kwa haki, tofauti na pale wanapotegemea kuambiwa na wanasiasa na wanaharakati waliochagua maisha ya kulazimisha hata rangi nyeupe iitwe nyeusi.

 

Binafsi nimefurahi kusikia na kuona kuwa wapo wananchi wazalendo katika nchi hii kama Mbunge Nyimbo, anayetambua umuhimu wa habari za Rais kupewa kipaumbele katika vyombo vya habari. Hii ni changamoto kubwa kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari Tanzania.

 

By Jamhuri