Tutarajie nini Mtei ‘anapobaka’ demokrasia Chadema?


Tutarajie nini mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edwin Mtei, anapofikia hatua ya ‘kubaka’ demokrasia ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini?

Mtei aliyepata kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wiki iliyopita amenukuliwa na gazeti moja linalochapishwa kila siku hapa nchini, akimtaka Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto, kutojitokeza kuomba kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

 

Kauli hiyo ya Mtei imekuja siku chache baada ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kufichua migogoro ya kusigana kisiasa inayoshika hatamu miongoni mwa viongozi na wanachama wa Chadema.

Mtei anamtaka Zitto amwachie Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, nafasi ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, akitoa sababu zake kuwa (Dk. Slaa) ndiye chaguo la wananchi wengi.

 

Inawezekana kweli kwa sasa Dk. Slaa ndiye chaguo la wengi. Lakini Mtei akumbuke kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika nchini baada ya miaka mitatu ijayo. Bado ni muda mrefu. Watanzania kwa asili ni wapenda mabadiliko, wanaweza kubadili msimamo wakati wowote. Wanaweza kuwa na chaguo jingine kufikia mwaka 2015.

 

Ninatoa fikra hii huku nikitambua kwamba kuna watu katika nchi hii wasiopenda kuambiwa ukweli na wanaolazimisha rangi nyeupe iwe nyeusi! Hao wanaweza kubeza fikra hii ya hekima kutokana na msukumo wa hisia za unafiki, chuki na maslahi binafsi.

 

Mwanadiplomasia maarufu duniani, maarufu kwa jina la Markus, alisema, “Tutakuwa hatuitendei haki serikali kama hatuiambii ukweli.” Binafsi nahisi nitakuwa simtendei Mtei haki kama nitakaa kimya bila kumkosoa kwa kumwambia ukweli kwamba ameanza kuminya demokrasia ndani ya Chadema.

 

Matarajio ya wengi ni kwamba Mtei kama mwanzilishi wa Chadema, alipaswa kuwa kioo kwa viongozi wa sasa kwa kuhimiza demokrasia ya kweli na haki ndani ya chama hicho, kiendelee kustawi na kuvutia watu wengi zaidi.

 

Cha kushangaza zaidi Mtei amenukuliwa na gazeti hilo akiwaonya wanachama wa Chadema wenye hisia za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, kusubiri mchakato wa mchujo wa majina utakaofanyika ndani ya chama hicho utakapowadia muda mwafaka.

 

Hapa maswali mawili yanatosha kujiuliza. Kama ndivyo, mbona Mtei anamtangaza Dk. Slaa mapema kuwa ndiye chaguo la wengi anayestahili kugombea urais? Mbona anamtaka Zitto asigombee huku akijua kuna mchakato wa mchujo ndani ya chama hicho utakaoamua nani agombee wadhifa huo?

 

Fikra ya Hekima inaziona kauli hizi za Mtei kama dalili za kuvuruga demokrasia ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani huku kikijinasibu kuwa ni mtetezi wa haki za wanyonge nchini.

 

Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, amesukumwa na hisia za kugombea urais, ana ndoto za kuwa rais wa Tanzania, kama Mtanzania huru ana haki ya kutangaza nia yake hiyo ili vikao husika ndani ya chama hicho vitoe uamuzi.

 

Kitendo cha Mtei kumzuia Zitto kuomba kuteuliwa na Chadema kugombea urais mwaka 2015 ni cha kikandamizaji, ‘kinabaka’ haki yake ya kisiasa na demokrasia ndani ya chama hicho.

 

Dk. Slaa anapotajwa kuwa chaguo la wengi leo, kesho mambo yanaweza kuwa tofauti. Nguvu ya umma inaweza kuamua vinginevyo, inaweza kutaka rais kijana na hivyo wanachama vijana akiwamo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na wengine kupewa nafasi ya kugombea urais mwaka 2015.

 

Binafsi ninafurahi kuona matunda ya mikono ya Mtei (Chadema) yanawavutia wananchi wengi, lakini anapaswa kuwa makini asije akageuka kuwa mfano wa mvunja nchi ni mwananchi. Aliasisi na kuimarisha Chadema lakini asipokuwa makini atakivuruga na kukibomoa chama hicho.

 

Mtei aache utaratibu wa kuwapata wagombea aliouasisi ndani ya Chadema ufanye kazi yake. Zitto, Dk. Slaa, Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na wanachama wengine wana haki ya kueleza nia zao ikiwamo ya kuomba kugombea uongozi katika nchi hii.

 

Bahati nzuri Zitto ametangaza kutozungumzia tena suala la kugombea urais hadi itakapopatikana Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Chadema kuweka utaratibu wa mchakato huo. Angalau hatua hiyo inaweza kuepusha mgawanyiko wa wanachama wa chama hicho, jambo ambalo wengi hatupendi kusikia na kuona linatokea.

 

Wakati Zitto akitangaza msimamo wake huo, swali linaendelea kubaki lile lile, kwamba Watanzania tutarajie nini kama Mtei ataendelea ‘kubaka’ demokrasia ndani ya Chadema? Atafakari na kujisahihisha.

 

1116 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!