Fimbo ya mbali na udhaifu wake

Moja ya kaulimbiu alizotoa Mwalimu Julius Nyerere alipoanza kuongoza Tanzania ilikuwa kusisitiza vipengele vinne muhimu vya kuleta maendeleo: ardhi, watu, siasa safi, na uongozi bora.

Naijenga zaidi hoja juu ya umuhimu wa watu, siyo kwa ujumla wake kama ambavyo Mwalimu Nyerere alisisitiza, ila kufafanua ni jinsi gani mtu mmoja akiwepo sehemu mahususi anaweza kuleta matokeo chanya katika kufanikisha malengo yake na ya jamii.

Binadamu hawezi kuwa sehemu mbili kwa wakati mmoja, lakini binadamu wengi tunaendesha shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo hazipo sehemu moja na, kwa kawaida, pale inapokuwa tuko mbali na shughuli zetu matokeo yake si mazuri.

Sizungumzii shughuli za biashara na uchumi zinazoendeshwa kwa weledi wa hali ya juu na wafanyabiashara au kampuni kubwa za biashara na uchumi zilizopo kwenye sekta rasmi. Nazungumzia hali halisi ya uchumi kama wa Tanzania uliyo na watu wengi ambao huendesha shughuli ndogo za biashara na uchumi ambazo zinaongeza pato la taifa, lakini zinabaki pembezoni mwa duara rasmi la biashara na uchumi. Najumuisha wajasiriamali au wamiliki wa biashara ndogo, na hata waajiriwa.

Haitakuwa sahihi kusema kuwa naandika mahususi juu ya wadau wa sekta isiyo rasmi, lakini hao watakuwa ndiyo walengwa wangu wakuu.

Katika utafiti uliofanywa mwaka 2011, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiria kuwa sekta isiyo rasmi iliajiri zaidi ya asilimia 10 ya waajiriwa wote. Wapo Watanzania wengi wa aina hii, na wanao mchango mkubwa wa kutoa katika kuongeza ajira, kukuza uchumi, na kulipa kodi serikalini.

Uhusiano wa karibu kabisa kati ya mafanikio na ukaribu na shughuli inayosimamiwa si wa kubuni, ni wa uhakika kama ambavyo tuna uhakika mawio yanafuata machweo. Kwanza, bila kuwapo mhusika yale anayokusudia kuyatekeleza – na hasa kama anao uzoefu na utaalamu wa kuyatekeleza vyema – yanaweza yasitekelezwe kama alivyopanga kwa sababu ya uzoefu mdogo wa anayepewa dhima hiyo. Kuwapo mahali hapo kunatoa nafasi ya kurekebisha kasoro za utekelezaji ili kufanikisha malengo.

Tatizo lingine kubwa la usimamizi kutoka mbali ni kupata wasimamizi waaminifu wa kupokea na kuwasilisha mapato kikamilifu. Kipindi kirefu cha tabia za ubadhirifu ambazo zilikuwa hazisababishi hatua kali dhidi ya wabadhirifu zilizua tatizo kubwa. Tatizo lilishamiri kwenye sekta ya umma, lakini matokeo yake yametapakaa kwenye sekta binafsi. Miongoni mwa matokeo ni msamiati wa kuwaita wezi ni ‘wajanja’, na waaminifu kuwa ni ‘wajinga’. Tatizo la ubadhirifu linapungua sana kama mhusika yupo kwenye eneo la biashara au uzalishaji.

Kwa bahati mbaya desturi ya mtu kukaa kazini akifanya kazi kwa uaminifu miaka nenda miaka rudi akidunduliza pesa za kujenga nyumba ilionekana – kwa msemo unaopenda kutumiwa na vijana – kama suala ambalo limepitwa na wakati. Kwenye mtazamo uliozoeleka, kupata mafanikio ya haraka haraka bila kujali iwapo yanapatikana kwa njia za halali ndiyo ikawa maisha ya kawaida.

Tatizo la uaminifu lina michepuko mingi. Mmiliki anaweza kubebeshwa malipo ya wafanyakazi au vibarua hewa. Anaweza kuambiwa kazi fulani ilifanyika jana, kumbe anayesema hayo alichapa usingizi siku nzima.

Suluhisho lipo dhidi ya ukosefu wa uzoefu na, kwa kiasi fulani, uaminifu, lakini hupatikana kwa gharama ya ziada. Mmiliki wa shughuli inayosimamiwa hawezi kuwa na uzoefu wa kutosha wa shughuli aliyoanzisha, lakini anaweza kuajiri mtu mwenye uzoefu wa kutosha ambaye, akilipwa vizuri, anaweza kuongeza maradufu ufanisi wa shughuli inayosimamiwa.

Faida kubwa ya kuajiri msimamizi mwenye elimu na weledi kwenye shughuli hizo ni kuongeza ufanisi, na ufanisi huongeza kipato. Kipato kikubwa kinaruhusu kuajiri mzoefu wa kufikia mafanikio yanayokusudiwa. Malipo mazuri ya wataalamu hayafuti tatizo la ubadhirifu, lakini yanalipunguza kwa kiasi kikubwa. Kichocheo kimojawapo cha wizi ni njaa. Njaa inapopungua kwa sababu msimamizi ana kipato cha uhakika kwa ajili yake na wategemezi wake, wizi nao unaweza kupunguka.

Wapo wengi wanaoelewa vyema umuhimu wa kuwepo karibu na shughuli wanazofanya kama njia muhimu ya kupunguza ubadhirifu na kuleta mafanikio, na hufanya hivyo wakati wote. Lakini wapo wengi ambao hawafahamu umuhimu huo au huupuuzia. Baadhi ya hawa wa kundi la pili huamini kuwa ndugu wa karibu wana wajibu wa kuwa waaminifu zaidi kuliko waajiriwa wasio ndugu, lakini ukweli ni kuwa hata ndugu nao hupata alama nzuri tu kwenye mitihani ya ubadhirifu.

Wale wa kundi la kwanza wanaweza kuwa ni watu wanaoamini kuwa watu wote – hata mama zao – ni wezi; kwamba wakipata upenyo wa kuiba wataiba tu. Sitashangaa kusikia kuwa ni watu wa aina hii ya pili wanaokuwa na mafanikio makubwa zaidi kwenye biashara na shughuli zao za uchumi.

Lakini hawatakuwa wamejenga tabia hiyo kutokana na kuangalia sana Bongo Movie. Yapo matukio mengi ya Watanzania wanaoishi ughaibuni walioamua kujenga nyumba nchini kwa kupitia usimamizi wa ndugu zao wakadanganywa kuwa ujenzi unaendelea na wakaendelea kutuma mamilioni ya pesa, wakati ukweli ni kuwa walikuwa wanalipia ujenzi hewa.

Changamoto hazijamzuia mwanadamu kufanya shughuli ambazo hawezi kuzisimamia yeye mwenyewe moja kwa moja. Kwa hiyo, pamoja na kwamba yapo matatizo ya kusimamia shughuli zetu tukiwa mbali bado zipo sababu nyingi zinazofanya tusiwe huru kuziacha kwa urahisi.

Shughuli hizi zina manufaa siyo kwetu tu, bali zinaongeza ajira na zinakuza uchumi. Kuchangia kukua kwa ajira na uchumi kunachangia pia uwepo wa amani. Ni mchango wa kizalendo sawa na ule wa wapiganaji wetu walioondosha majeshi ya Idi Amin kwenye ardhi ya Tanzania. Wajibu wa wale wanaoendesha shughuli hizi ni kuongeza ujuzi na maarifa ya kupunguza athari ya kuwa mbali na shughuli zenyewe.

Ni kweli kuwa fimbo ya mbali ina udhaifu wake. Njia mojawapo ya kuipa nguvu ni kwa mhusika mkuu kusogea karibu na shughuli zake mara kwa mara.