Katika sehemu ya pili ya makala haya, Sheikh Dk. Ibrahim Ghulaam, alizungumzia nyudhuru za funga, nguzo za funga, unavyothibiti kuingia Mwezi wa Ramadhani na yanayobatilisha funga. Sasa mfuatilie zaidi katika sehemu hii ya tatu…

Yasiyo funguza

1. Kula au kunywa kwa kusahau. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Mwenye kusahau naye amefunga, basi akala au akanywa na aikamilishe funga yake….} (Al Bukhariy na Muslim).

2. Kusukutua au kupandisha maji puani wakati wa kuchukua udhu (bila ya kubalighisha).

3. Kuoga au kujiburudisha kwa kujimwagia maji kiwiliwilini (hasa katika maeneo yenye joto kali).

4. Kuonja chakula kwa mpishi (kwa sharti la kutokumeza alichokionja).

5. Kutokwa mbegu za uzazi (manii) katika usingizi (ndoto) au bila ya kukusudia.

6. Kuamka na janaba. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mamama Aishah na Ummu Salamah (Radhiya Allahu ‘anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiamka na janaba kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anaoga na kufunga (Al Bukhariy na Muslim).

7. Kupiga mswaki (wakati wowote).

8. Kuchoma sindano ya kawaida ya tiba.

9. Kung’oa jino na mfano wake.

10. Mwanamke kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au nifasi.

 

Adabu za funga

Baadhi yanayosuniwa kwa mfungaji

 

1. Kula daku. Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas ibn Maalik (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema: amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Kuleni daku kwani hakika  chakula cha daku kina baraka ndani yake} (Al Bukhariy na Muslim). Na inasuniwa kuchelewesha kula daku hadi kukaribia alfajiri.


2. Kuharakisha kufuturu (mara tu likizama jua). Imepokewa hadithi kutoka kwa Sahl ibn Saad (Radhiya Allahu ‘anhu). Hakika Mjumbe wa Mungu (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) amesema: {Watu watakuwa bado wapo katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari}. (Al Bukhariy na Muslim).


Na inasuniwa (kuanza) kufuturu kwa tende au maji. Imepokewa  hadithi kutoka kwa Salmaan ibn’Aamir (Radhiya Allahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) amesema: {Anapofuturu mmoja wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata (tende) basi na afuturu kwa maji, kwani hakika ya maji ni kitoharisho (kisafisho) ( Wameipokea Maimamu watano).


Na pia inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati wa kufuturu, kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa kufuturu ni katika dua zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) .

 

Baadhi yanayotakiwa ayakithirishe Mwislamu katika mwezi wa Ramadhani

 

1. Kisimamo cha usiku (Swalah ya tarawehe). Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Mwenye kusimama (kwa ibada) katika mwezi wa Ramadhani kwa imani (thabiti) na hali ya kutaraji malipo kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa yale aliyoyafanya katika madhambi yake}. (Al Bukhariy na Muslim).

Na inafaa kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika misikiti maadamu watachunga na kufuata taratibu za dini (sharia). Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Msivizuilie vijakazi vya Mwenyezi Mungu (wanawake) (kuhudhuria ibada) katika misikiti ya Mungu}. (Al Bukhariy na Muslim). Na haifai kwa wanaume kuwazuilia wanawake walio katika usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo bila ya kuwa na sababu za kimsingi zinazokubalika kisheria, amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Wakiwaombeni ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni}. (Muslim).

 

2. Kuzidisha kusoma Qur-aan. Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qur-aan na ndiyo mwezi ulioteremshwa ndani yake Qur-aan, Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala): {{Hakika tumeiteremsha (Qur-aani) katika Laylatul-Qadr (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa Mwezi wa Ramadhani).}} (97:1). Na {Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qur-aani…} (2:185).

 

3. Sadaka. Pamoja na fadhila zake katika masiku yote huzidi fadhila na thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allahu ‘anhuma): Alikuwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) mkarimu (mtoaji) na alikuwa mkarimu zaidi katika Mwezi wa Ramadhani wakati anapokutana na Jibriyl (A.S.) (Al Bukhariy na Muslim).

Na katika sadaka zinazotiliwa mkazo katika Mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha waliofunga. Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Mwenye kumfuturisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano wa malipo ya aliyemfuturisha na hayapungui malipo ya aliyefunga kitu chochote}. (Ahmad na Annasaiy).

 

4. Kufanya Umrah. Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Umrah katika Mwezi wa Ramadhani una malipo sawa na Hijjah}. (Muslim).

 

5. Itikafu (nako ni kubaki msikitini bila ya kutoka ukijishughulisha na ibada mbalimbali). Inasuniwa kufanya itikafu na hasa katika kumi la mwisho la Mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhuma) amesema: Alikuwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akifanya itikafu siku kumi za mwisho za Mwezi wa Ramadhani. (Al Bukhariy na Muslim).

 

6. Kuutafuta usiku wa cheo (laylatul-qadr), na zaidi katika kumi la mwisho la Ramadhani. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mama ‘Aishah (Radhiya Allahu ‘anha) amesema: Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Utafuteni usiku wa cheo (laylatul-qadri) katika siku kumi za mwisho za Ramadhani} (Al Bukhariy na Muslim).

Na amepokea Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu)  kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) amesema: {Mwenye kusimama katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani thabiti na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala),  husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya hapo)} (AlBukhariy na Muslim).

 

7. Toba. Nako ni kurudi kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na makosa aliyoyatenda mja na kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia kutokuyarudia makosa hayo).

 

*Tukumbuke ya kuwa mwanadamu si mkamilifu, daima yupo katika hatari ya kufanya makosa, hasa makosa hayo ikiwa ni ambayo ameyahisi au hakuyahisi wakati wa kuyafanya kwake. Toba ndiyo njia ya kujikosha na madhambi ya makosa hayo, na kipindi cha Mwezi wa Ramadhani ni fursa muhimu ya kutubia.

Ikiwa katika makosa yake kuna haki za wanadamu inamlazimu kuzirejesha kwa wenyewe haki hizo.

 

Itaendelea

3066 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!