DAR ES SALAAM

Na ALEX KAZENGA

Vicheko na furaha vimetawala kwa wafanyabiashara wadogo wenye vibanda (vioski) katika Soko la Chifu Kingalu lililopo Manispaa ya Morogoro, baada ya kodi yao kupunguzwa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella, ametangaza hayo hivi karibuni baada ya wafanyabiashara wengi kuvifunga vioski.

Kushushwa kwa bei za upangaji kutoka Sh 300,000 kwa mwezi hadi Sh 100,000, kumetokea wiki chache baada ya JAMHURI kuandika kwa kina kuhusu malalamiko hayo.

Bei hizo ni kwa vioski vya chini huku vibanda vya ghorofani gharama za upangaji zikishushwa kutoka Sh 200,000 hadi Sh 50,000 kwa mwezi.

Mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, Rose Minja, anasema wengi wao walikuwa wamekata tamaa na sasa anaishukuru serikali kwa kuwarejeshea matumaini.

“Mkurugenzi wa Manispaa aliyeondolewa alikuwa hajali utu, changamoto za soko tulizifikisha kwake lakini hatukusikilizwa. Tulifikia uamuzi wa kuachana na masuala ya soko hili tukihofia kuonekana tugombana na serikali,” anasema Rose.

Anasema baada ya kupata taarifa za kupungua kodi, sasa ataanza kutafuta mtaji afufue biashara zake.

Hata hivyo, anaiomba manispaa kusaidia kuitisha uchaguzi wa viongozi wa soko kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Wafanyabiashara wa Manispaa ya Morogoro (UWESOMO).

“Manispaa yetu kwa muda mrefu ilikuwa mikononi mwa watawala, badala ya viongozi,” anasema Aziza Omary, Katibu wa Kikosi Kazi kilichoundwa kutafuta ufumbuzi wa changamoto za soko hilo mwaka 2019.

Anasema yanayojitokeza Manispaa ya Morogoro ni fundisho kwa halmashauri nyingine nchini kwamba viongozi wanatakiwa kuwatumikia wananchi kwa haki.

Chanzo cha migogoro iliyopo katika Soko la Chifu Kingalu ni kukosa uongozi unaotokana na wafanyabiashara wenyewe.

“Uongozi wa soko wa sasa ni wa mpito. Haupo kwa masilahi ya wengi. Ulitumiwa na manispaa kuhalalisha baadhi ya hujuma, ikiwamo kutunyang’anya vibanda sisi wafanyabiashara wa zamani kwa kutumia kodi kandamizi,” anasema Aziza.

Mwenyekiti wa mpito wa soko hilo, Khalid Salum, ameliambia JAMHURI kwamba kuna watu wanachochea migogoro katika soko hilo, akikituhumu kikosi kazi cha akina Aziza kutumia fedha kuhonga waandishi wa habari waichafue Manispaa ya Morogoro.

“Sipo kwa ajili ya kugombania uongozi, kazi yangu ni kutetea masilahi ya wafanyabiashara wenzangu.

“Bei za vibanda zimeshushwa kwa sababu ya ushawishi wangu, hao wanaozunguka kila ‘stationery’ kuchapisha vikaratasi kueleza eti changamoto, waambie waje ofisini tuwasikilize,” anasema Khalid.

Kwa upande mwingine Soko la Chifu Kingalu linakabiliwa na changamoto kadhaa; mfano kuziba kwa mfumo wa maji taka eneo lililotengwa kwa mama lishe kuoshea vyombo.

Pia eneo hilo halina kibaraza cha kuzuia watu wasinyeshewe mvua nyakati za masika au wasifikiwe jua nyakati za kiangazi.

Kukosekana kwa kibaraza husababisha wateja kutofika kwa wingi kupata huduma ya chakula.

Kwa upande wa eneo lililotengwa kwa ajili ya kuchinja na kuuza kuku, wafanyabiashara wanadai mazingira si rafiki, kwani limejificha na halina eneo la kukusanyia uchafu.

Sasa wafanyabiashara hao wanamuomba RC Shigela kuzitafutia majibu changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kumaliza kero za wamachinga.

Kuhusu uvamizi wa eneo la soko uliofanywa na machinga, wafanyabiashara hao wanasema kuna eneo la wazi linaitwa ‘Kikundi’, ni vema serikali ikawahamishia huko, kwani kwa siku zote za juma huwa liko wazi isipokuwa Jumamosi.

Wanasema huenda hilo lisiwezekane kutokana na maeneo mengi ya wazi Morogoro kuuzwa kinyemela.

Wanaomba uongozi wa mkoa kuyafuatilia maeneo hayo na kuyarejesha ili machinga wapate sehemu ya kufanyia biashara.

Ujenzi wa Soko la Chifu Kingalu umegharimu fedha za walipa kodi Sh bilioni 17.6.

Soko hilo limefunguliwa Januari mwaka huu na kuingia katika mgogoro kwa miezi sita mfululizo na kusababisha wafanyabiashara wengi kufunga vibanda vyao na kukimbilia katika masoko ya Manzese na Mawenzi, Mtaa wa Sabasaba.

Lawama za soko hilo kutofanya vizuri zilielekezwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa, Sheilla Lukuba.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa, waliondolewa kwenye uongozi Juni 13 na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushindwa kusimamia wafanyabiashara wadogo.

Gazeti la JAMHURI toleo Na. 506, ukurasa wa kwanza na ukurasa wa tano liliandika kuhusu mgogoro wa bei za kukodi vioski katika soko hilo ukiwahusisha wafanyabiashara wadogo na uongozi wa manispaa.

By Jamhuri