Serikali ya Japani imekiri kuvutiwa na kuhamasishwa na fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini, hususan katika sekta ya nishati ambako imeonesha nia ya kuwekeza.

Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa Japan, Toshimitsu Motegi, aliyasema hayo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo, jijini Dar es Salaaam, hivi karibuni.

 

Waziri Motegi aliyeongoza ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Japani, alitaja baadhi ya maeneo ambayo nchi yake ingependa kufanya uwekezaji kuwa ni uzalishaji na usambazaji wa umeme.

 

Aidha, wafanyabiashara waliofuatana na Waziri Motegi, walimweleza Waziri Muhongo kuwa fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini, hususan upatikanaji wa gesi asilia zimekuwa ni kivutio na kichocheo kikubwa kwao kutamani kuwekeza Tanzania.

 

Mbali ya kuonesha nia ya kuwekeza hapa nchini, Wajapan wameonesha pia utayari wa kuwasaidia Watanzania katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali zilizopo kwa kutoa mafunzo.

 

“Serikali yangu iko tayari kupokea wanafunzi kutoka Tanzania kwa ajili ya mafunzo katika fani ya masuala ya jotoardhi,” alisema Waziri Motegi.

 

Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa sasa serikali yake inafanya maandalizi ya kuanza kupokea Watanzania kwa mafunzo husika na kwamba endapo mambo yataenda sawa, huenda mafunzo yakaanza rasmi mapema mwakani.

 

Kwa upande wake, Waziri Muhongo aliishukuru Serikali ya Japan kwa utayari wa kuwapatia mafunzo Watanzania na kusisitiza kuwa hilo ni jambo la msingi kwa nchi kuweza kusimamia rasilimali zake kikamilifu.

 

“Serikali imedhamiria kuongeza wataalamu wazawa watakaoweza kusimamia rasilimali zetu vizuri pasipo kutegemea wataalamu kutoka nchi za nje,” alisema.

 

Aidha, Profesa Muhongo aliwahakikishia Wajapan kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji na hivyo, kuwakaribisha wafanyabiashara hao kuja kuwekeza, hususan katika miradi ya uzalishaji na usambazaji umeme kupitia vipaumbele vilivyoanishwa na serikali vya jototardhi, tungamotaka, gesi asilia, upepo na umemejua.

 

1039 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!