Gwiji wa ujangili Arusha atambuliwa

Mtuhumiwa mkuu wa ujangili katika Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire na katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, aliyetiwa mbaroni wiki iliyopita, ametambuliwa kuwa ni Frank William (32) au maarufu kama “Ojungu”.

Kukamatwa kwake ni matokeo ya kazi nzuri ya Kikosi Kazi cha Kupambana na Ujangili kinachoundwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

 

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu, Allan Kijazi, na Meneja Uhusiano, Paschal Shelutete, limethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

 

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, zinasema kukamatwa kwa Ojungu kumesaidia kikosi hicho kuutambua mtandao wa ujangili. Hadi mwishoni mwa wiki, mtuhumiwa huyo alikuwa akiendelea kuhojiwa Polisi. Anatajwa kama mmoja wa vijana matajiri mno katika Mkoa wa Arusha.

 

Alikamatwa wiki iliyopita akiwa mafichoni katika nyumba eneo la Sakina mjini Arusha. Amekuwa akisakwa kwa muda mrefu. Mara ya mwisho aliponea chupuchupu kukamatwa wakati askari wa Kikosi Kazi walipokuwa wakifukuza gari la mmoja wa mabalozi wa nchi za nje waliopo hapa nchini ambalo lilikuwa na nyara za Serikali. Polisi walisema Ojungu na mwenzake walifanikiwa kutoroka baada ya ajali hiyo.

 

Taarifa kutoka kwa maofisa wanaomhoji mtuhumiwa huyo, zinasema wamefanikiwa kupata taarifa za “kustaajabisha” ambazo zinawahusisha kwenye ujangili wa tembo na faru baadhi ya wanasiasa nguli, wakuu kadhaa wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini na wanasiasa. JAMHURI imepata majina ya watuhumiwa hao, lakini kwa sababu za kitaaluma, inayahifadhi kwa sasa.

 

Mpaka wa Namanga unatajwa kama mlango mkuu wa mtandao wa Ojungu wa kutorosha nyara za Serikali kwenda Nairobi, Kenya na Kampala, Uganda.

 

Katika mahojiano hayo, imebainika kuwa Ojungu amekuwa akimiliki bunduki nyingi ambazo amekuwa akiwakodisha walio kwenye mtandao huo kwenda kuendesha vitendo vya uuaji tembo na nyara nyingine za Serikali.

 

“Ana mtandao na maofisa wa juu kabisa wa Jeshi la Polisi, wengine wamo jeshini hadi sasa, na wengine ni wastaafu; kuna wanasiasa huwezi kuamini, kuna wafanyabiashara wa ngazi za juu hata wanajeshi kadhaa.

 

“Ojungu alikuwa Kenya, huko amekuwa akishirikiana na majangili wenye asili ya Kisomali, alipokimbizwa akarejea Arusha. Akajificha kwa sababu anajua amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Amekiri kuwa ujangili aliuanza miaka ya 2000. Anasema amepata fedha nyingi zilizomwezesha hata kumiliki migodi ya tanzanite huko Mererani,” amesema mmoja wa maofisa wanaosimamia Kikosi Kazi hicho.

 

Imeelezwa pia kwamba mtuhumiwa huyo amepata kuwaponyoka askari wa TANAPA Januari mwaka huu, walipolikamata gari la JWTZ katika eneo la Mto wa Mbu likiwa na meno ya tembo. Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser VX likikuwa na namba bandia, na linadaiwa ni mali ya Mwambata wa Kijeshi wa Zimbabwe hapa Tanzania.

 

Habari zaidi zinasema kwamba mtuhumiwa huyo ametoboa mbinu zinazotumika kushinda kesi au kupewa adhabu ndogo katika mahakama.

 

“Anasema fedha anazo, washirika wake wanapokamatwa wanawahonga baadhi ya wanasheria na mahakimu, wanaachiwa. Ametoa mifano hadi tukabaki midomo wazi. Anasema sehemu nyingine wanakuwa na nyara, wakifika kwenye vizuizi wanatoa shilingi milioni moja au chini ya hapo na kuachiwa. Tena anasema kwa kujiamini kabisa kwamba polisi ndiyo wepesi zaidi,” kimesema chanzo chetu.

 

Kushiriki kwa polisi kwenye ujangili kunathibitishwa na uamuzi wa Jeshi la Polisi kumwondoa mmoja wa askari polisi waliokuwa wakishiriki kwenye Kikosi Kazi hicho mwenye cheo cha inspekta.

 

“Huyu alikuwa anayumbisha kikosi, mara zote tulishindwa kujua ni nani anayetoa siri kwenye mtandao hadi tushindwe kuwanasa. Tumefanikiwa kumjua, ameondolewa na kurejeshwa Makao Mkuu, Dar es Salaam,” kimedokeza chanzo chetu.

 

Akihitimisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2013/2014, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alitoa wito kwa wahusika wote wa ujangili kuacha, kwa sababu Serikali imedhamiria kuchukua hatua ambazo hazijawahi kuchukuliwa, na kwamba zitabaki kuwa kwenye kumbukumbu za vizazi vijavyo.

 

Ujangili wa tembo

Kamati ya Kudumu ya Bunge imesema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni janga la kitaifa. “Ni ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa kimataifa zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka (TAWIRI 2011).

 

“Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutoka TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.

 

“Endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara moja, ni wazi tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka saba ijayo,” imeonya Kamati.

 

Kamati hiyo imeongeza; “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo. Kinachosikitisha ni kwamba Wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete, iliyoitaka Wizara kuomba msaada kwake kama tatizo la ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni hujuma inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara ambao wamepuuza kauli ya Mheshimiwa Rais.”

 

Kamati imeshauri Serikali kuendesha Operesheni Uhai kwa nchi nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia imependekeza Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu kali kwa watu wote watakaothibitika kuhusika na ujangili, hasa wa tembo.