Nianze kwa kuwasalimu wasomaji wa safu hii ya Anga za Uchumi na Biashara, ambayo haikuwa hewani kwa takribani wiki saba.

Sababu kubwa iliyonifanya nitoweka safuni kwa muda huo, ni msiba niliopata wa kufiwa na binti yangu wa kwanza na wa pekee, Faith, aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja.

 

Katika juhudi na mahangaiko ya kuokoa uhai wake, binti yetu alifariki katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wilayani Kilosa. Msiba huu uliniachia uchungu na majonzi makubwa mno kiasi ambacho akili, moyo na morali vilitoweka kabisa na isingekuwa rahisi kumudu tafakari pana zinazoijaza safu hii.

 

Nimekuwa na uzoefu (kiasi fulani) wa kumudu majanga, mitikisiko na mikasa ya kibiashara; lakini lilipokuja suala la kupoteza mtu muhimu kama mwanangu, hakika nilijikuta ni mgeni kabisa wa kuhimili mtikisiko wa msiba huu.

 

Matakwa yetu na maombi yetu yalikuwa ni kupona kwa binti yetu, lakini Mungu aliamua kuutwaa uhai wake. Tunamshukuru na kumtukuza Mungu kwa yote tuliyopitia, tunajua Mungu anabaki kuwa Mungu, hata kama hakujibu tulivyotaka.

 

Kwa namna ya kipekee, ninatumia fursa hii kuwashukuru wasomaji wa safu hii kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao baada ya kutoniona katika safu, walinitafuta na kutaka kujua kulikoni. Mbarikiwe sana mliotutumia rambirambi za fedha na salamu za faraja.

 

Ijapokuwa sikuaga wakati napotea safuni lakini sisiti kupiga mbiu inayoashiria kuwa nimerejea. Yapo mambo mengi ambayo tutaendelea kushirikishana yahusianayo na ustawi wetu kiuchumi, kiujasiriamali na kibiashara. Kwa kuwa leo ndiyo kwanza ninarejea, nitachambua kinagaubaga utamaduni wa watu kupenda fedha kuliko thamani ya walivyonavyo; jinsi unavyourubuni uchumi wetu.

 

Ni vema tukajikumbusha historia ya namna fedha zilivyoanza kutumika katika maisha ya wanadamu. Hapo zamani kulikuwa kukifanyika biashara ya ubadilishanaji wa vitu kwa vitu (barter trade). Ilikuwa mtu akiwa na ng’ombe basi atabadilishana na mwenye chumvi, vivyo hivyo kwa mwenye mahindi anaweza akabadilishana na mwenye nguo.

 

Kadiri mfumo huu ulivyoendelea, ikaonekana suala la kubeba vitu na kuzunguka navyo kutafuta wa kubadilishana naye ni usumbufu na lina ugumu wa kuoanisha hayo mahitaji.

 

Wakati mwingine mwenye ng’ombe anapohitaji chumvi halafu mwenye chumvi akawa hayupo tayari kupokea ng’ombe; basi hakuna biashara itakayofanyika na hivyo mwenye ng’ombe kukwama kupata chumvi.

 

Katikati ya mfumo huu yakaibuka matumizi ya vito vya thamani (mfano dhahabu, pembe za thamani, chuma na madini mengine); kama viambata vya kubadilishia bidhaa (media for exchange). Hapa ilikuwa kwamba mkulima anapovuna mahindi yake, pengine magunia kumi,  anayachukua na kuyapeleka kwa hao wanaotengeneza vito vya thamani, kisha anapewa idadi ya vito vya thamani vinavyolingana na thamani ya mahindi yake. Huu ndiyo uliokuwa mwanzo wa hiki tunachokiita fedha.

 

Hata hivyo, baada ya muda kupita ikaonekana kuna upungufu katika uthaminishaji wa vito vya thamani na bidhaa wanazozalisha watu. Ndipo kukatokea watu waliokuwa kama wahakiki wa thamani ya vitu, mali ama bidhaa alizonazo mtu.

 

Ilikuwa hivi; mkulima anapolima na kupata mahindi yake, pengine tuseme magunia kumi, alikuwa anayapeleka eneo maalum ambapo wanamtunzia. Wenye stoo (eneo alipotunzia) walikuwa wanaandika karatasi (kibali) inayoonesha kuwa mkulima A anamiliki magunia 10 ya mahindi yaliyopo stoo B.

 

Kwa hiyo mkulima alikuwa hana tena sababu ya kutembea na magunia ya mahindi kumtafuta mwenye chumvi; badala yake alitembea na ile karatasi kiasi kwamba anapofika kwa mwenye chumvi anampa ile karatasi na kupewa chumvi.

 

Yule aliyempa mkulima chumvi ataenda kule kwenye stoo na kuchukua mahindi yanayolingana na thamani ya chumvi aliyompa mkulima; kisha ile karatasi anaiacha pale stoo. Hizi stoo zilikuwa ndiyo chimbuko la benki tunazoziona sasa na zile karatasi zilizokuwa zinaandikwa na wenye stoo ndiyo chimbuko la hizi noti tulizonazo leo.

 

Hii ina maana mfumo wa benki na fedha ulitokea ili kuwe na haki, usawa na ukweli. Mkulima mwenye magunia 10 ya mahindi lazima apewe karatasi (fedha) inayoonesha kweli anamiliki hayo magunia, si vinginevyo. Kama huyo mkulima akipewa karatasi inayoonesha anamiliki magunia kumi ya mahindi wakati hajapeleka chochote kule stoo ingekuwa ni kumrubuni, kumdhulumu na kumlaghai yule mwenye chumvi.

 

Hii ni kwa sababu mwenye chumvi atakapoletewa ile karatasi na mkulima (aliyedanganya) ataitoa chumvi yake; lakini atakapoenda kule stoo ataambiwa hapa hakuna magunia ya hayo mahindi yanayoonekana kwenye karatasi uliyotuletea.

 

Baadaye jukumu hili la kuandika (kuchapisha) hizi karatasi (fedha) zinazoonesha fulani kazalisha nini kilichopo wapi, likachukuliwa na mamlaka za kiserikali zilizokuwa zinasimamia jamii mbalimbali. Hivyo, ikawa mkulima akizalisha mahindi yake anapewa karatasi yake (fedha), vivyo hivyo kwa mfugaji anapofuga na kuongeza mifugo na mjenzi anapojenga jengo. Kila mtu katika jamii alikuwa anashika fedha inayoonesha thamani halisi ya kile alichozalisha katika uchumi.

 

Kwa jinsi hii, tunaona kuwa fedha katika uhalisia wake ni matokeo ya uzalishaji anaoufanya mtu katika uchumi.  Fedha si mafanikio, isipokuwa ni utambulisho wa mafanikio. Utajiri wa mkulima hauwi katika zile karatasi alizozishika (fedha), isipokuwa utajiri wake unakuwa kwenye yale magunia aliyoyazalisha. Thamani ya mwalimu haitakiwi kupimwa kwa kiwango anacholipwa isipokuwa kwa maarifa aliyoyazalisha kwa wale anaowafundisha.

 

Lakini katika jamii na nchi yetu sasa, watu wamekuwa wanathamini fedha kuliko uzalishaji. Watu wanapenda kupata fedha ‘hewa’. Ndiyo maana wanataka kuonekana ni matajiri wakati hakuna lolote walilozalisha katika mfumo wetu wa uchumi. Tunapokuwa na jamii inayothamini fedha kuliko uzalishaji; maana yake ni kuwa tuna jamii inayopenda kurubuni, inayopenda mikato-mikato, uongo-uongo na unyonyaji kwa wengine.

 

Katika mizania ya uchumi ni kwamba moja ya sababu za mfumko wa bei ni uwepo wa ujazo mkubwa wa fedha katika uchumi usiolingana na uzalishaji (uzalishaji mdogo). Kinachotokea ni kuwa fedha zinakuwa nyingi na bidhaa ni chache.

 

Wale walioshika fedha wanaanza kugombea zile bidhaa chache zilizopo. Kinachotokea; watu wanapandishiana ‘dau’, mwenye nguvu ananunua na mnyonge anabaki kulalamika. Matokeo; ndiyo tunasikia vitu vinapanda bei kwa kasi kubwa!

 

Unapoona madalali wamejaa mtaani, ambapo kila unachotaka kununua wapo katikati, ujue kuna ulaghai unafanyika kiuchumi. Ikiwa ninataka kununua nyumba na mwenye nyumba anayeuza namfahamu, dalali wa nini hapo katikati? Kwa kuwa tumeshauzoea mfumo wa udalali, ninayenunua nyumba ya Sh milioni 25 ninalazimika kulipa Sh milioni 30 ili dalali apewe Sh milioni tano yake.

 

Kiuchumi ni kwamba tunakuwa tumempa dalali Sh milioni tano za uongo kwa sababu hakuna uzalishaji wowote alioufanya; ingawa ‘kijamii’ tutamuona anamiliki utajiri wa Sh milioni tano! Dalali anapoichukua ile Sh milioni tano na kwenda kwa mkulima kununua mahindi, unakuwa ni ulaghai kiuchumi.

 

Ni ulaghai kwa sababu hela ile (Sh milioni tano) imechapishwa wakati hakuna uzalishaji katika uchumi. Kesho na keshokutwa mkulima anapotaka kuitumia ile Sh milioni tano kununua pembejeo anajikuta haitoshi tena (imeshuka ama kupoteza thamani) kwa sababu ni ya uongo!

 

Sina ugomvi na madalali na wala siwachukii; isipokuwa tunatakiwa tuwatumie madalali pale tu panapokuwa na ulazima na ikiwa kweli uwepo wao unazalisha thamani halisi ya gharama wanazotaka. Madalali ni mfano mmoja tu lakini ulaghai wa kupata fedha pasipo uzalishaji upo katika mazoea mengi.

 

Kahaba anapodai malipo ya Sh 50,000 ni nani anayekuwa amethibitisha kiuchumi kwamba huduma yake ina thamani hiyo? Mfanyakazi wa Serikali anapotaka asilimia kumi (10%) ili kutoa tenda kwa upendeleo, ni uzalishaji gani ameufanya kiuchumi? Mfanyakazi anapolilia mshahara mkubwa pasipo kuongeza tija kiuzalishaji, anatutakia nini kiuchumi kama si balaa?

 

Uchumi wetu hauwezi kusonga mbele kwa kiwango kizuri ikiwa tunaendekeza kupata fedha na utajiri usiolingana na uzalishaji tunaoufanya katika uchumi. Hakuna fahari ya mtu kujiridhisha na utajiri, ama mafanikio ya fedha yaliyopatikana kiujanja-ujanja, kimteremko-teremko na kiusanii-sanii.

 

0766 74 24 14, [email protected]


Please follow and like us:
Pin Share