Kwa muda wa miaka kadhaa sasa, nimekuwa kwenye harakati za kuhakikisha nchi yetu inatambua uhuru wa vyombo vya habari, haki ya kupata habari na uhuru wa kutoa mawazo. Harakati hizi zimenifikisha hatua ya kufahamu kwa kina umuhimu wa habari na hasa habari sahihi.

Nimepata fursa ya kufahamu kuwa nchi yetu imechelewa katika maendeleo kutokana na taarifa au habari sahihi kuchelewa kuwafikia wananchi. Hii inakuwa sawa na duka linalouza saruji kwa bei nafuu, lakini wateja wanaotafuta saruji hawajui wapi kwenye duka hilo linalouza saruji kwa bei nafuu. Wote wanaishia kupata hasara.

 

Nimetumia mfano wa saruji mapema kwa nia ya kujaribu kukufikirisha wewe msomaji uweze kutambua umuhimu wa taarifa au habari sahihi. Uweze kuona kuwa kumbe ungepata taarifa sahihi ungeweza kununua saruji kwa bei nafuu na ukaokoa sehemu ya fedha ulizonazo mfukoni. Hata hivyo, kwa kutokuwa na taarifa sahihi pengine unaishia kununua saruji ya bei ghali.

 

Sitanii, wiki mbili zilizopita sikuandika katika safu hii. Sikuandika kwa sababu nilikuwa Bukoba nilikokwenda kufuatilia mgogoro unaoendelea katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba (BMC).

 

Leo nitazungumzia eneo moja tu la mgogoro huo. Baada ya hapo nitagusia mafanikio tuliyoyapata katika vita dhidi ya wauza dawa za kulevya, kisha nitasisitiza umuhimu wa haki ya kupata habari kwenye Katiba.

 

Nilipofika Bukoba niliambiwa na watu mbalimbali mambo mengi. Binafsi sikutaka kuyaamini kabla ya kushuhudia hadi nilipozungumza na wananchi walioguswa na uamuzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuhusiana na ardhi katika upimaji wa viwanja 5,000. Mmoja wa walioguswa ni Stephen Ngaiza. Huyu ni mkazi wa Kata ya Nyanga, Wilaya ya Bukoba Mjini.

 

Nilipozungumza na Ngaiza aliniambia kuwa awali alikuwa anamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari sita. Maafisa wa BMC walifika katika shamba hili na kulipima kisha wakamwambia asaini karatasi, na baada ya hapo aende Posta atakuta akaunti yake ina fidia Sh 1,200,000.

 

Hapa ukipiga hesabu za haraka, ekari sita zina mita za mraba 29,400. Kwa kulipwa Sh milioni 1.2, ina maana kila mita ya mraba alilipwa Sh 40.8. BMC wao wanauza mita ya mraba Sh 4,000. Ngaiza akitaka kurejeshewa ardhi hiyo aliyolipwa fidia anapaswa kuilipa halmashauri Sh 117,600,000.

 

Huyu ni mwananchi aliyelipwa Sh milioni 1.2, leo akitaka kurejeshewa eneo lake anapaswa alipe Sh milioni 117.6. Hivi atazipata wapi? Hakika kwa kila kiwango huu ni wizi wa mchana. Ndiyo maana BMC wanasema waliishapata faida kutokana na uuzaji huu wa ardhi ya wananchi.

 

Sitanii, hatari kubwa inayowanyemelea wakazi wa Bukoba ni kugeuka ombaomba. Mtu yeyote anapokunyang’anya ardhi, bila kujali itikadi za kisiasa anakuwa hakutakii mema. Anataka sasa ugeuke mpangaji au kijakazi nyumbani kwake. Mpango huu umesukwa kimkakati kuwanyima fidia stahiki wananchi wa Bukoba, kisha kuwageuza watumwa ndani ya nchi yao.

 

Nasema kama wananchi hawa wangepata habari kwa wakati, sidhani kama wangekubali kuachia ardhi yao, wakalipwa fidia hii isiyokidhi mahitaji kisha wageuke ombaomba. Habari sahihi zinakufanya ufanye uamuzi sahihi. Muungano wa Wadau wa Habari ukiongozwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) unadai haki hii ya kupata habari.

 

Tukio kama hili la Bukoba ingekuwa Katiba ya sasa inatambua haki ya kupata habari, ni wazi viongozi wa BMC wasingevamia mashamba ya watu na kupima ardhi bila kuwapa taarifa sahihi. Ni wazi wananchi wasingekubali kulipwa fidia ya mtego na ni wazi maendeleo ya wananchi yasingedumaa kwani wangedai fidia stahiki na fedha ambazo wangepata zingewasaidia kuanzisha miradi ya maana.

 

Mfano huu unatuonesha umuhimu wa Katiba mpya kutambua Haki ya Kupata Habari. Zipo halmashauri nyingi zinazofanya mchezo huo hapa nchini. Zinanyang’anya wananchi ardhi na kuwauzia tena kwa bei ‘mbaya’. Wananchi wengi wanashindwa kulipa gharama kubwa na hivyo wanaishia kufukuzwa katika maeneo yao.

 

Sitanii, ukiacha hilo la Bukoba linalothibitisha umuhimu wa Haki ya Kupata Habari kuingizwa kwenye Katiba, kwa maana kwamba viongozi nao wawe na wajibu wa kutoa habari kwa wananchi wao kuepusha uamuzi wa kidikiteta, nguvu ya habari sisi tumeishuhudia tulivyoanzisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

 

Gazeti JAMHURI lilipoandika mara ya kwanza, baadhi ya watu walifikiri hakuna kitakachotokea. Leo kesi nyingi zinasikilizwa kuliko wakati wowote, wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya wanakamatwa kuliko wakati wowote na kubwa tunalojivunia Sheria Kuzuia Dawa za Kulevya Na 9 ya mwaka 1995 inafanyiwa marekebisho makubwa.

 

Taarifa sahihi tulizoziandika katika gazeti hili zimeizindua Serikali kutoka usingizini. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, ametangaza rasmi kuwa Serikali inaifuta Sheria ya sasa ya Kuzuia Dawa za Kulevya na kutunga mpya. Anasema sheria itakayotungwa sasa kwa atakayethibitika kufanya biashara ya dawa za kulevya adhabu yake itakuwa ni kifungo na faini.

 

Sitanii, ieleweke vizuri hapa. Sheria ya sasa inasema kifungo au faini, lakini sheria hiyo ijayo itasema mtu anafungwa halafu analipa faini – si kuchagua kati ya kifungo au faini kama ilivyo sasa. Hatua hii imefikiwa kutokana na kazi iliyofanywa na vyombo vya habari. Vimelisimamia kidedea suala hili na jamii sasa inashuhudia matunda yake.

 

Nasema sheria hii ikitungwa na ikapitishwa na Bunge, basi ni wazi hao wauzaji wa dawa watajifikiria mara mbili kabla ya kufikia uamuzi wa kuuza dawa hizi. Watakuwa wanajua fika kuwa kifungo ni hadi maisha na hakuna mwanya wa kupigwa faini kama ilivyo sasa.

 

Taratibu za ushahidi pia zinatajwa kuwa zitabadilishwa. Badala ya mtuhumiwa kukamatwa upande wa mashitaka ukaendelea kuhifadhi vielelezo, chini ya sheria mpya vielelezo vitateketezwa mara tu mtuhumiwa atakapothibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa kweli amekutwa na dawa hizo.

 

Uamuzi huu wa Serikali kutunga sheria mpya unathibitisha nguvu ya habari. Serikali nyingi duniani zimepunguza uhalifu, zimepunguza gharama za kukusanya kodi, zimepunguza gharama za matumizi mabaya ya mali za umma kwa kuwa na sheria zinazoruhusu uwazi.

 

Leo ikitokea kila kiongozi, taasisi, mfanyabiashara au chombo chochote kikatakiwa kutoa taarifa sahihi bila mizengwe kwa mujibu wa sheria, pato la Taifa litaongezeka ajabu. Wananchi watajikuta huduma za jamii zinaimarika kwa sababu hakutakuwapo ukwepaji kodi, mapato ya Serikali yataongezeka na wadokozi hawatakuwa na nafasi.

 

Hawatakuwa na nafasi kwa maana kwamba kila senti itakayokusanywa itapaswa kuelezwa kwa uwazi jinsi ilivyotumika. Hii italisaidia Taifa kufahamu hata miradi ya maendeleo fedha zinazotolewa zimefanya nini na kwa ubora upi. Sheria hapa itamlazimisha mtu kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.

 

Sitanii, ibara ya 30 ya Rasimu ya Katiba pamoja na upungufu wake wa ibada ndogo ya 4, imefanya jambo jema kutambua uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari. Najua watunga sheria watakuwa na kazi ya kuandika Katiba mpya ifikapo Novemba mwaka huu, kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.

 

Nasema haki zote za msingi zilizotolewa katika rasimu hii zinaweza kutekelezwa pale tu kama haki ya msingi ya uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari itakuwa imetekelezwa. Haki hii ikiingizwa kwenye Katiba hakuna mtu atakayefanya biashara haramu kwa kinga ya uhuru wa mtu binafsi.

 

Vyombo vya habari vitakuwa huru kuingia kwa undani na kuchambua hadi mapato ya mtu mmoja mmoja yanatokana na nini kama wanavyofanya Marekani. Nchini Marekani inafika mahala mwananchi wa kawaida anashtakiwa kwa kudanganya mamlaka akalipa kodi kidogo ikilinganishwa na alichostahili kulipa.

 

Sitanii, kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa letu, nasema kila Mtanzania sasa anapaswa kuwa Balozi wa Haki ya Kupata Habari. Serikali imetoa ahadi mara nyingi kuwa ingepeleka bungeni muswada wa uhuru wa habari, lakini hadi leo muswada huo haujulikani ulipo. Tangu mwaka 2006 wadau wanadai muswada huu na hadi leo haujapatikana!

 

Ni maoni yangu, na kama tunataka maendeleo ya haraka na ya kweli, basi yatupasa Watanzania kushikamana kuhakikisha nchi yetu inapata haki ya kupata habari kwenye Katiba ijayo. Narudia kama nilivyopata kusema, hii haki ya kupata habari si kwa ajili ya waandishi wa habari pekee, bali kwa ajili ya Watanzania wote.

 

Mifano miwili niliyoitumia ya uporaji wa ardhi Bukoba na kutungwa sheria mpya ya kuzuia dawa za kulevya, inapaswa kutufanya Watanzania tuwe kitu kimoja katika kudai haki hii ya kupata habari, kwani ni wazi ikipatikana Watanzania wote tutaifaidi na nchi yetu na itapata maendeleo ya kasi.

 

Mungu ibariki Tanzania.

 

By Jamhuri