Sehemu ya pili ya kumbukumbu ya maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu ya Afrika ilifanyika Jumatano Oktoba 21, 2015 kwenye Hoteli ya New Afrika. Siku hiyo mambo yalinoga kweli. 

Kwanza, mgeni rasmi alikuwa Rais mstaafu wa Awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Huo uteuzi wa mzee aliyetuzidi wazee wote mle ndani kwa umri ulionesha namna Tume ile ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilivyolichukulia suala zima la wazee kwa uzito unaostahili.

Kwa vile yeye mwenyewe ni mzee alijiona wazi anashiriki kikamilifu katika mambo ya wazee wenzake. Halafu alialikwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, na tena walialikwa mabalozi wa nchi za Afrika wanachama wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (AU).

Tulifikiri au tulijisikia Tume ya Haki za Binadamu wametujali na kutuheshimu kimila za Waafrika kwa kufikia hatua ya kutufikisha katika hoteli ile ya kitalii ya “The New Africa Hotel”. Labda hapa niwataarifu wasomaji wangu kuwa enzi za ukoloni, mahali pale ilipo hoteli hii ilikuwapo hoteli ya Wazungu tu, na enzi hizo Mwafrika (kwa maana ya mtu mweusi tulivyojulikana miaka hiyo) hakuruhusiwa kuingia pale, wala kula chakula katika hoteli ile.

Na pombe za Kizungu tunazoita beer Mwafrika ilikuwa marufuku kunywa hapa nchini. Ndiyo maana moja ya shabaha za African Association ilikuwa kudai Waafrika waruhusiwe kunywa beer! Hatai Baba wa Taifa enzi hizo za ukoloni miaka ile ya 1950 na kitu hakuruhusiwa kunywa pombe ile ya Wazungu. ‘Beer’.

Leo hii Mngoni wa kutoka Litapwasi au Msukuma wa Simiyu au Mhaya wa Muleba tumeingia New Afrika Hotel kufanya kumbukumbu za Haki za Binadamu ya Afrika eti na kula lanchihumo humo, ni badiliko kubwa hilo katika nchi yetu!

Akimkaribisha mgeni rasmi katika siku hiyo ya kumbukumbu za Haki za Binadamu ya Afrika, Mwenyekti wa Tume, Bahame Tom Nyanduga, alionesha kupendezwa kwake kwa upendo wa viongozi wa Serikali, waheshimiwa mabalozi wa nchi wanachama Umoja wa Afrika na mwakilishi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu. Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi wa wazee kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu kuhudhuria katika makumbusho yale. 

Aidha, mwenyekiti huyo alielezea kwa kifupi historia ya chanzo cha maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu ya Afrika. Akaturudisha nyuma hadi mwaka 1979 wakati viongozi wa Afrika walipokubaliana kuanzishwa kwa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za watu (African Charter on Human and Peoples Rights – ACHPR).

Aliendelea kusema kuwa Juni 27, 1981 viongozi wa Afrika walikubali mkataba huo katika mkutano wao uliofanyika mjini Nairobi, Kenya. Tanzania ilisaini mkataba huo mwaka 1981 na Februari 18, 1984 iliridhia mkataba huo. Lengo la maadhimisho haya ni kuikumbusha Serikali yetu na jamii ya Watanzania kwa ujumla umuhimu wa kuheshimu, kulinda, kuhifadhi na kukuza HAKI ZA BINADAMU zikiwamo HAKI ZA WAZEE ili kudumisha ustawi wa jamii kwa ujumla. 

Wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula alipozungumza na wazee, hakumung’unya maneno. Alisema wazi wazi namnukuu “Undoubtedly, in any country, important reforms can only be carried out effectively with the active participation of civic society as useful link between government bodies and common person. The presence of so many from CSOs, NGOs and International Organisations is a clear commitment that they attach to the plight of the elderly persons in Tanzania.” Kwa tafsiri yangu (isiyo rasmi) ni dhahiri au bila shaka katika nchi yoyote, mabadiliko muhimu yawezekana tu kwa ushiriki kamili wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo huwa kiungo muhimu kati ya Serikali na mwananchi.

Hivyo, uwepo wa mashirika mengi namna hii kama CSOs, NGOs na yale mashirika ya kimataifa ni ishara wazi ya kujitolea kwao katika kuwaenzi na kuwaendeleza wazee wa Tanzania. Aliendelea kueleza kuwa kila mara tunapokusanyika tarehe hii ya Oktoba 21, tunakumbuka waanzilishi wa Umoja wa Afrika na mchango wao mkubwa katika kuunda chombo hiki.

Hapa Tanzania, utaratibu au mpango huu unalinda Haki za Wazee hasa kiusalama wao, zaidi akina mama haki zao za kuishi na kuwa na mali yao na hata haki yao ya kushiriki katika uchaguzi wa viongozi.

Kadiri tunavyosogelea mwanzo wa utawala kwa Awamu ya Tano (bado siku chache tu sasa) nadhani ni wakati mwafaka jambo hili la haki za wazee nchini lipewe msukumo mpya unaostahili. Tumekumbushwa hapa eti ile sera ya wazee ya tangu miaka hiyo mpaka leo haijatungiwa sheria ya utekelezaji wake. Yapata miaka 12 sasa! 

Kwa kawaida, sera ikishatolewa huhitaji maboresho ya mara kwa mara baada ya kila miaka 5 ili iendane na wakati, sasa hii miaka 12 bila sheria ndiyo kusema imeshapitwa na wakati! Jambo hili ni changamoto kwa Serikali.

Aidha, warsha iliyoendeshwa jana imekuja wakati muafaka maana kuna mchakato wa kupata Katiba mpya – nadhani ni wakati muafaka mambo ya wazee yakawekwa sawa humo. Basi mijadala mliyokuwa nayo jana itasaidia kurekebisha mapungufu katika Katiba mpya pendekezwa kabla ya kukubaliwa. Nashauri wazee muendelee kutoka mchango wenu katika uboreshaji wa hiyo Katiba pendekezwa kabla haijakamika na kukubalika. 

Kiwizara sisi tumejipanga kuhakikisha ushiriki wetu katika mikutano ya kimataifa pale inapohusu masuala ya wazee tutawashirikisha kikamilifu. Sote tushirikiane katika hili. 

Ninapenda kuwahakikisha wazee, tutakuwa bega kwa bega nanyi kuona wazee wanatendewa ipasavyo. Muda wa utekelezaji ndiyo huu. Tunapaswa kuwa na mpango kabambe (we must draw road map on this drive with the timelines) kukamilisha majambo haya. 

Mwishoni alisifia uteuzi wa Tume wa Mgeni rasmi. Hangepatikana mtu bora zaidi ya huyu Rais Mstaafu mzee wetu Mwinyi kuja kuongea nanyi. 

Wazee walilipuka kwa vifijo na makofi na baadhi yetu tulijitahidi tumshukuru angalau kwa kumshika mkono. Nilibahatika kuwa mmoja wa wale waliomshika mkono na kumshukuru kwa dhati kabisa. Hii imekuwa mara ya kwanza kiongozi wa juu kutoka Serikali kutuonesha anavyojali na kuchukulia uzito masuala ya wazee. Yuko tayari kwa kutusikiliza na hasa kutekeleza matatizo yetu kisera, na kisheria. 

Baadaye wazee walisoma maazimio yao yale 14 (yameorodheshwa hapo juu) na wakamkabidhi mgeni rasmi. Ilipatikana nafasi waathirika wa haki za binadamu kutokana na dhana potofu za uchawi kule Kanda ya Ziwa walifika mbele ya mgeni rasmi wakaongea na kuonesha makovu ya mapanga.

Mwisho, mzee wetu Rais Mstaafu Mwinyi aliongea na wazee. Huyu mzee alishikwa na huzuni na aliongea kwa kuwatumainisha wazee kuwa kama MJUMBE atayafikisha yale yote kwa kiongozi yeyote wa juu atakayechaguliwa baada ya uchaguzi wa Jumapili tarehe 25 Oktoba, 2015. 

Alianza kwa kusema “…. Maadhimisho haya yanatokana na maamuzi ya Mkutano wa Nairobi wa 1981 wa wakuu wa nchi na Serikali za Afrika ulioafiki kuanzishwa kwa Mkataba wa HAKI ZA BINADAMU na Watu. Mkataba huu uliridhiwa na kupata nguvu ya kisheria tarehe 21 Oktoba 1986 ambavyo ndiyo siku tunayoadhimisha leo. Siku hii ni siku muhimu sana na ya kihistoria kwa Waafrika, kwani viongozi wa Afrika waliamua kutambua HAKI ZA BINADAMU na HAKI ZA MAKUNDI ya watu yaani “People’s rights” na hivyo kulifanya bara la Afrika kuongoza dunia nzima kutambua uwepo wa haki za makundi maalum. 

Alipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Shirika la HelpAge International kuchagua kaulimbinu “ULINZI NA USTAWI WA WAZEE TANZANIA”. Ni ujumbe wa kuwalinda na kutetea haki za wazee. Alisema kuna haki za msingi za wazee ambazo jamii inapaswa kuzitambua na kuzisimamia. Akaagiza wataalamu na wadau mbalimbali wa “Haki za Wazee” na “Hifadhi ya Jamii” wanapaswa kujadiliana hili kwa kina na kuwasilisha mapendelezo Serikalini. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora italivalia njuga utekelezaji wa suala hili. 

Mzee Mwinyi alisikitishwa sana na lile jambo la kuuliwa wazee kutokana na imani potofu za kishirikina, alilaani mauaji hayo na akatoa wito kwa wadau wote ikiwamo Serikali kuchukua hatua stahiki zitakazokomesha kadhia hii ya kitaifa. Mwisho alitambua jitihada na huduma zitolewazo na taasisi mbalimbali zikiwamo HelpAge International na mpango wa TASAF. 

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua iliyochukua ya kuhudumia wazee (SMZ imeshaamua kumlipa kila MZEE kule visiwani PENSHENI au malipo ya UZEENI kiasi cha Tshs. 10,000/= kila mwezi kwa kila mzee mwenye umri wa miaka 70 na kuendelea). Ni uamuzi uliowafurahisha wazee wote katika sherehe ya sherehe ya siku ile. 

Sisi wa Bara tunajiuliza iweje watu wa Jamhuri moja, wazee wote wa VISIWANI wanalipwa malipo hayo ya uzeeni hawa wa Bara hawalipwi, tueleweje hapo? 

Mzee Mwinyi alihimiza wazee tujitokeze kwa wingi siku ya Jumapili tarehe 25 Oktoba tukapige kura kwa utulivu tupate Serikali itakayotusikiliza. 

Baada ya Mzee Mwinyi, Rais mstaafu, kuongea na wazee, Naibu Mwanasheria Mkuu alitoa shukrani (vote of thanks) kwa mgeni rasmi na aliahidi kutekeleza baadhi ya yale yaliyolalamikiwa pale kwa upande wa sheria. 

Kwa vile nilikuwa mmoja wa wazee na niseme mwenye umri mkubwa sana katika warsha ile (miaka zaidi ya 85+) ni mzee Mwinyi tu umri wa miaka 91 amenipita umri wa miaka 6 nikajiona kuwa na bahati ya mtende namna ile ninawajibika kutoa elimu ya urais kwa wenzangu ndiyo sababu ya kuandika makala hii. 

Ningependa wazee wote 2, 507,568 wa nchi hii angalau tuyaone na tuyasome yale maazimio yetu kwa Serikali. Si hivyo tu, lakini huko tuendako sina shaka kwa matumaini tuliyopewa na Mzee wetu, Rais mstaafu Mwinyi, na yale matamshi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa si ajabu wazee wakapata malipo ya uzeeni muda si mrefu na walipata sheria ya kuwatekelezea mambo yao. 

Hapo wasishangae wajue wakiona vyaelea wajue wapo baadhi ya wazee wamekuwa wakiviunda hivyo vinavyoelea. Tukae mkao wa kula wazee – Mzee Mwinyi ametupa matumaini ya uzima mpya. Tukaimbe; Mwinyi yupo, Mwinyi yupo, ukiona kundi la wazee na Mwinyi yupo! 

Sisi wazee tuna usemi wetu au amkio letu “Wazee tupo! Walikuwapo, na watakuwapo” kwa maana kuwa sisi tunaojiita wazee hapa unatuona TUPO. Lakini kabla yetu wazee duniani walikuwapo na baada yetu sisi, nyinyi vijana wa leo mtajakuwa wazee UZEE HAUKWEPEKI jamani. 

1265 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!