Kwa mara ya kwanza nimeshiriki sherehe za maadhimisho ya siku ya Haki za Binadamu Afrika. Ilikuwa Oktoba 21, 2015. Kwa kweli ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia sherehe hizo na nashukuru kualikwa nami nikapata kushiriki katika kilele cha sherehe ile. 

  Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International hapa nchini, walishirikiana kuandaa sherehe za siku hiyo. Ili kufanikisha shughuli za kilele cha siku ya Haki za Binadamu ya Afrika waliwaalika wazee kutoka asasi mbalimbali za wazee humu nchini.

  Walikuwako wadau wanaohusika na mambo ya wazee kwa namna moja au nyingine kama vile wizara ya Serikali, Ustawi wa Jamii, Afya, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wanasheria, mabalozi  mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika yenye makao makuu yake kule Arusha, asasi za kiraia na hata wanahabari. Kwa ujumla tulikuwa na uwakilishi wa kutosha katika siku ya kumbukumbu hii. 

  Lakini sherehe za kumbukumbu za namna hii zina malengo maalum. Waandaaji wa kumbukumbu hii walilenga maudhui ya kusikiliza kero au kilio cha wazee wa nchi hii. Wakaja na kaulimbiu ya “Ulinzi na ustawi wa wazee wa Tanzania”.

  Hapo utaona wazi Haki za Binadamu zinazoongelewa ni zile zinazokiukwa juu ya wazee. Sisi wazee tulijisikia tumepewa fursa ya kusikilizwa na chombo husika hasa katika kilio chetu cha miaka nenda miaka rudi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

  Tumekuwa tunaomba, kila tukutanapo na uongozi wa ngazi za juu katika Serikali mambo kadhaa. Tumeomba Haki za Wazee ziainishwe katika Katiba ya nchi kama vile Katiba Pendekezwa ilivyoainisha haki za yale makundi mengine kama Haki za Watoto; Haki za Wanawake na Haki za Watu wenye Ulemavu. 

  Wazee kwa miaka mingi wameomba wapate hifadhi ya jamii, malipo ya uzeeni kama inavyokuwa katika mataifa yaliyoendelea, lakini Serikali imekuwa inawaahidi kwa lugha laini, “mchakato” unaandaliwa, mikakati imeshawekwa, hivi karibuni mtaona matokeo (kwa Kiingereza wanasema ‘it is in the pipeline) je humo ndani ya bomba huo mchakato hauwezi kutoka wazee wamesema sera ya wazee ilishatolewa tangu mwaka 2003 hakuna sheria ya kuelekeza utekelezaji wake, huu sasa ni mwaka wa 12.

  Mpaka lini sheria itakuja kutolewa ili sera ifanye kazi? Wazee hasa kule kwenye Ukanda wa Ziwa wamekuwa wanauliwa kila mwaka kwa kisingizio cha imani potofu ya uchawi, lakini hatuoni juhudi za kukomesha mauaji namna hii ya wazee. Tunajiuliza mbona yalipoanza mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (zeruzeru au albino) nguvu ya Serikali ilionekana?   

  Hivi kuna tofauti kati ya kifo cha mzee na albino? Hatujapata jibu la kuridhisha. Kuna kero za wazee kufukuzwa katika maeneo yao, kunyimwa chakula, kukosa dawa au kukebehiwa katika vituo vya afya ilimradi kuwasononesha tu. 

   Waandaaji walipanga sherehe za mwaka huu zifanyike kitaifa na ziwe za siku mbili. Siku moja wadau wote – wazee, watumishi wa Serikali na mashirika ya umma, taasisi mbalimbali wawe na warsha elimisha juu ya ulinzi na ustawi wa wazee Tanzania. Siku ya pili pawe na hitimisho la siku ya kumbukumbu ya Haki za Binadamu ya Afrika. Kilele chake akaribishwe mzee wa heshima sana katika Jamhuri yetu tushiriki naye katika kuadhimisha kumbukumbu ya siku yenyewe.

   Oktoba 20 tukakusanyika katika Ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pale Luthuli Road. Kule kuingia tu mle ukumbini tukakutana na bango kubwa lenye ujumbe “BINADAMU WOTE HUZALIWA HURU NA SAWA” mimi nikaona ‘ee’ hapa kweli ni mahali wazee tutakaposikilizwa. Niliamini hivyo kwa sababu ninajua Umoja wa Mataifa ulishatoa tangazo la hizo haki za binadamu tangu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

  Sidhani kama vijana wa siku hizi wameona tangazo lile “original version”. Kwa kuwa ninalo, nilikwenda na kile kijitabu cha UNO. Tangazo limeandikwa hivi “UNIVERAL DECLERATIONN OF HUMAN RIGHTS” final Authorised Text (United Nations Department of Public Information) dated 10 December 1948. Katika tangazo lile zimeainishwa HakiI 30 za Binadamu wote. 

  Haki ya kwanza kabisa kifungu No. 1 inasema BINADAMU WOTE HUZALIWA HURU na SAWA katika UHURU na HAKI. Wamepewa akili na dhamira na wanapaswa kutendewa kidugu (soma Tangazo la Baraza Kuu/General Assembly uk. 11).

  Hivyo, niliona pale sisi wazee Tume imetufikisha mahali pake panapostahili sisi wazee kusema na kusikilizwa. Hivyo siku ile ya Jumanne, Oktoba 20, Tume ilipanga warsha yenye mada tatu zinazohusiana na wazee. Mada ya kwanza iliandaliwa na Tume yenyewe. Hii ilikuwa juu ya “AFRICAN HUMAN RIGHTS” na ilijikita katika kuelezea misingi ya haki za binadamu kwa mtazamo wa sisi Waafrika kimila, desturi na mapokeo ya kimataifa yetu.

  Kiafrika wazee ndiyo msingi wa familia, kabila na Taifa zima. Wanakuza na kuendeleza lugha, tamaduni, mila na desturi kutoka kizazi hadi kizazi. Wanalea watoto wao kimapokeo katika majando, manyata na unyago. Hivyo wanaendeleza desturi nzuri za kila kabila. Funzo la kwanza ni heshima kwa wazee na yeyote aliyekuzidi kiumri. 

  Kwa mada ile haki za watoto na wajibu wa watoto zilikumbushwa. Utu wa binadamu ulifafanuliwa na hivyo heshima inayopaswa kutolewa kwa wakubwa yaani wazee isiwe ya amkio tu la ‘Shikamoo’ bali iwe ni heshima ya kutambua umri, hekima na busara za wazee katika ukoo, kabila na Taifa zima. 

  Mada ya pili, ilikuwa juu ya “THE SITUATION OF OLDER PERSONS” (Hali ya wazee) hapa nchini Tanzania. Hii mada iliongelewa kwa kirefu na Ofisa wa HelpAge International. Zilitolewa takwimu za idadi ya wazee hapa Tanzania kutokana na ile sensa ya mwaka 2012. Tuliambiwa sensa ilionesha tuko wazee wa umri wa miaka 60 na kuendelea mpaka 100 — wazee 2,507,568.

  Katika idadi hiyo wazee wanawake wako 1,307,358 wakati wazee wanaume tuko 1,200,210.  Unaweza kujionea takwimu hizo kutoka Ripoti ya Sensa ya 2013 vol. II uk. 65). Basi miongoni mwa wananchi tupatao 44,928,923 wazee tupo kama asilimia 5.6. Katika jumla yote ya wazee 2,507,568 zaidi ya asilimia 80 wanaishi vijijini (rural areas).

  Aidha yalitolewa maonevu wanayopata wazee katika sehemu mbalimbali na hivyo kukiukwa kwa haki za msingi za binadamu. 

  Matatizo ya wazee hasa wale wa vijijini ni ukosefu wa kipato cha kuendesha maisha yao na ya wategemezi kama watoto yatima, wanaowatunza, wananyang’anywa mali zao mashamba/mifugo nyumba na kadhalika.   Wanauliwa kwa kisingiizo cha uchawi, wanapokwenda kwa vyombo vya ulinzi na usalama (Polisi, Mahakama za Mwanzo, watendaji wa Serikali za Mitaa (WEO) huwa hawasikilizwi mara na pengine uchunguzi huchukua miaka kadhaa bila matokeo ya haki zao. 

  Zilitolewa takwimu za mauaji ya kikatili kwa wazee huko Kanda ya Ziwa kati ya mwaka 2008 mpaka 2013 kuwa wazee 2,866 waliuliwa kutokana na imani potofu za uchawi. Idadi hiyo ni wastani wa mauji 573 kila mwaka.

  Mwaka huo wa 2013 wazee 765 waliuawa na katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2014 wazee 320 waliuawa. Je, mauaji ya wazee wengi namna hiyo kwanini Taifa lisishituke? Au kwanini yasiitwe janga la kitaifa? Kwa mtazamo hasi namna hiyo wa Serikali, wazee tunaona usalama wetu uko hatarini.

  Waliletwa baadhi ya waathirika wa ghasia za unyanyasaji kutoka kule Kanda ya Ziwa. Kutoka Muleba alikuja mzee aliyechomewa moto mji wake, kukatiwa migomba yake na hivi sasa hana mahali pa kuishi kutoka na tuhuma za uchawi.

Kutoka Simiyu walikuja akinamama wawili walioteswa kwa kukatwa mapanga na kuchomewa nyumba zao huo ulikuwa ushahidi halisi (live exhibits) wa manyanyaso ya wazee katika nchi yetu. Mpaka leo hii uchunguzi wa kesi zao Polisi wanasema haujakamilika, ni zaidi ya miaka 12 hivi eti uchunguzi unaendelea. Hapo pana haki tena kwao?

  Waliletwa wazee kutoka Muleba na Simiyu kuelezea walivyoteseka kwa kukatwa mapanga na kuchomewa moto makazi yao. Huu ni mwaka wa 12 sasa uchunguzi haujakamilika! Haki za wazee hapo hazipo. 

  Mada ya tatu ilitolewa Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka makao makuu ya Idara. Hii ilijikita katika kile kilichoitwa “NATIONAL FRAMEWORK FOR PROTECTION OF OLDER PERSONS – RIGHTS AND WELFARE. Alielezea Idara inavyoshughulikia suala la sheria za kusimamia ile sera ya wazee namna wazee wanavyoshughulikiwa siku ya wazee ulimwenguni – Oktoba mosi – na ugumu wa kupata mafungu ya fedha kwa Idara. 

  Vipaumbele kwenye bajeti vinafanya Hazina kufyeka mafungu ya mahitaji ya wazee katika makambi ya wazee na shughuli nyingine. Suala la sheria, Wizara ilisema Tume na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ziingilie kati. Baada ya kusikiliza vilio halisi vya wazee katika warsha hii, na ili sheria itungwe ilishauriwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wasaidie katika kuharakisha upatikanaji wa sheria za wazee. 

  Baada ya mada hizo zote kusikilizwa, wazee walichangia mawazo yao na kuelezea uzoefu wao.  Wawakilishi kutoka sharia, Mahakama, Hifadhi ya Jamii na TASAF walitoa majibu au maelezo yao ili kupoza vilio vya waze.

Hitimisho la kuchangia mawazo na kutoa maelezo kinaganaga juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wazee wa nchi hii, warsha ilifikia uamuzi wa kutoa maazimio 14 ili kuwakilishwa kwa Serikali kama njia mwafaka ya kumaliza kero za wazee na upatikane ufumbuzi za kudumu katika ulinzi na ustawi wa wazee wa Tanzania.

 

Maazimio hayo ni pamoja na:

• Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kufanya mchakato wa kuanzisha mabaraza ya wazee kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya wazee.

• Ushiriki wa Tanzania katika shughuli za wazee za Umoja wa Mataifa uzingatiwe.

• Sheria ya wazee itungwe (mchakato wa utungaji wa sheria ukamilike kwa muda mwafaka).

• Ulinzi wa haki za wazee upewe kipaumbele ikiwa ni pamoja na kutekeleza mikakati ya kukomesha mauaji ya wazee nchini.

• Katiba pendekezwa iainishe haki za wazee kama ilivyo kwa makundi mengine (ya watoto, wanawake na watu wenye ulemavu zilivyoainishwa).

• Kuhakikisha malipo ya pensheni kwa wazee wastaafu yanafanyika kwa wakati na kuanzisha mfumo wa kulipa pensheni jamii kwa wazee wote.

• Sheria ya uchawi ifanyiwe marekebisho.

• Jamii ielimishwe kuhusu haki za wazee kupitia wadau kutoka serikalini na asasi za kiraia.

• Serikali iandae na kutekeleza mipango endelevu ya kurasimisha mali za wazee hususan umiliki wa ardhi.

• Huduma za afya kwa wazee ziboreshwe ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa wahudumu maalum wa afya na madawa ya kutosha na vyumba maalum kwa ajili ya wazee.

• Halmashauri zitambue na kutenga bajeti kwa ajili ya familia yatima zinazolelewa na wazee.

• Huduma kwa wazee ni suala mtambuka hivyo ipewe kipaumbele katika kila wizara, taasisi na idara za Serikali.

• Kuendeleza programu za kuhamasisha jamii kujiunga na mifuko ya hiari ya jamii.

• Wazee wawe na wawakilishi katika ngazi na vyombo vya uamuzi.

Wazee tunaamini Serikali na mamlaka mbalimbali zinazohusika na wazee watapokea na kutekeleza hayo yote.

 

>>ITAENDELEA

1824 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!