Katika baada ya kipindi hiki cha miezi miwili hakika tumeshuhudia mtifuano wa wanasiasa waliochuana kutangaza sera na ahadi ili kupata nafasi ya kuongoza nchi.

Sera zote zililenga kumkomboa Mtanzania dhidi ya maadui watatu wa tangu Uhuru ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

Mtifuano huo umeonesha nafasi ya nchi kwa kufananishwa na mgonjwa mahututi anayetafuta nafuu na uimara wa afya yake kupitia kwa wanasiasa wetu, ili aweze kupona na hatimaye kusonga mbele miaka ijayo huku nchi ikisuasua kukua kiuchumi.

Hata hivyo, katika hali ya kuchuana na kutafuta mbadala wa kuweza kuikomboa nchi yetu, mbinu mbalimbali zimetumika kufanikisha hilo huku wanasiasa kupitia wapambe wakipambana kuhakikisha mgombea wanayempigia dede anashinda.

Wapo baadhi ya wagombea wamebahatika kubebwa na umaarufu wao wa kisiasa waliojijengea, wengine wamebebwa na umaarufu, uzoefu wa vyama husika huku wengine wakibebwa na kimbunga cha mabadiliko kinachoikumba nchi kwa sasa.

Hata hivyo, katika kutafuta tiba mbadala za kuikomboa nchi yetu pendwa kuonesha matumaini mapya, uwezo na mikakati kila mmoja wao amekuwa akibadili matibabu kwa wananchi kila mara.

Hivyo basi, baada ya kumalizika kwa kipindi cha kampeni za kutafuta viongozi wa Taifa letu kwa miaka mingine mitano, ni muda sasa wa kutoa mwanya wa kuiangalia nchi yetu bila pilikapilika za kampeni.

Tuna jukumu la kutafakari tunaipeleka wapi nchi yetu na tunahitaji nini katika maisha yetu, baada ya kushuhudia yaliyoendelea katika ulingo wa siasa kwa kipindi tulichoshuhudia.

Huu si wakati wa mihemko wala malipizi yasiyo na tija kwa nchi yetu pendwa, hatuhitaji kuishi kwa uhasama ulioonekana hapo awali kutokana na kutokubaliana kiitikadi.

Ni lazima tufike mahali tukubaliane kutokubaliana huku tukiijenga nchi yetu kwa kudumisha amani na utulivu. Watanzania tunalo jukumu la kutafakari kwa kina kuhusiana na mustakabali wetu na vizazi vyetu.

Tunayo fursa ya kujiangalia ndani ya nafsi zetu tunahitaji nini siyo kukaririshwa mambo yatakayokuja kutugharimu. Tuliwahi kudokeza kuwa ‘za kuambiwa changanya na …’ je, tunapomaliza kuambiwa tunachanganya na zetu au tunachanganya na za mbayuwayu?

Tumeshuhudia ni kwa kiasi gani wanasiasa wetu waliweza kuamsha mihemko ya hapa na pale, hasa kwa vijana, iliyotokana na ahadi na matumaini yao kwa wanasiasa. Watanzania wamechoka kuhadaiwa, wamechoka ahadi zisizotekelezeka, ahadi za maziwa na asali huku maisha yao yakiwa ya kuweweseka.

Wanasiasa wametumia udhaifu huo katika uchaguzi huu, lakini pia vijana na wananchi kwa ujumla wamejikuta wakitumika kuongozwa njia za porini badala ya sehemu salama.

Tumeshuhudia ni kwa kiasi gani wananchi wanavyohamasishwa na makundi ya wanasiasa kutotii sheria bila shuruti, kupambana kufa na kupona ili kupata kile wanachodai haki yao.

Naungana nao katika kudai haki, lakini haki hiyo idaiwe katika njia mwafaka siyo kuhamasishana mambo kushiriki katika uvunjifu wa amani.

Ni lazima kila mmoja wetu ajitafakari kwa kina na kujitambua kabla hajafikiria kufanya jambo litakalokuja kugharimu maisha yake, familia yake na Taifa kwa ujumla.

Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tumetimiza haki yetu ya kuchagua na kuchaguliwa, hivyo basi jukumu letu kubwa lililobaki ni kusimama kidete kulinda amani ya nchi yetu bila kuyumbishwa na matakwa ya watu wachache wenye nia mbaya.

Tukumbuke ya kuwa nchi yetu inazo rasilimali nyingi ambazo wapo wasiopendezwa na kubarikiwa huko, watu hao wapo tayari kutumia mbinu mbalimbali katika kipindi hiki ili tuweze kufarakana.

Hatutakiwi kutoa mwanya kwa mtu, kikundi chochote kile kitakachoonesha nia ya kutuhadaa ili tuanze kutengeneza mazingira ya kupigana wenyewe kwa wenyewe, huku wao wakinufaika na machafuko hayo.

Huu ni wakati wa Watanzania wote kusimama kwa pamoja na kulinda amani ya nchi yetu, hatupaswi kuyumbishwa na mihemko na maslahi ya wachache  wanaotaka kuyaweka rehani maisha yetu kwa maslahi yao binafsi.

Tanzania ni nchi yetu, rasilimali zilizopo ni zetu sote, ni jukumu letu kuilinda ili zitumike kwa faida yetu wote siyo kikundi fulani cha watu wachache.

Tunamaliza uchaguzi huku tukitafakari maisha yetu ya baadaye, mwisho wa uchaguzi siyo mwanzo wa vurugu bali mwanzo na mwendelezo wa maisha yetu ya kila siku. Kila mmoja wetu atimize wajibu wake.

By Jamhuri