Kuna kuendelea, lakini katika majanga ya asili ni nguvu kidogo sana mwanadamu anaweza kumzuia anayeyaleta.

Nilipokuwa najiandaa kwa sherehe za Krismasi kwa maana ya kuhakikisha majokofu yamejaa vyakula na familia inapata mahali pa kupendeza kwenda siku hiyo, nilishtushwa na matangazo ya televisheni.

 

Zilikuwa habari za kuzuia watu kusafiri upande fulani wa nchi, kwa sababu ya mafuriko yanayoonekana sasa kuwa kero ya kudumu. Kinachonifanya nikumbuke zaidi kuhusu tatizo hili ni maneno ya mtangazaji baada ya ile taarifa muhimu.

 

Huyu alikuwa ni hawa ma-DJ kama wa redio zetu za FM za Dar, Mwanza na Arusha wanaotangaza siku hizi. Akasema kwa Kiingereza kwamba kuzuiwa huko kusafiri ni kutokana na “predictable unpredictability of United Kingdom weather’.

 

Eti ‘predictable unpredictability’ ya hali ya hewa kwa nchi hii ya Mtukufu Malkia.

 

Alichosema na anachoendelea kusimamia katika vipindi vyake ni kwamba imeshakuwa kawaida sasa kwa Uingereza na teknolojia zake za “super computer” na mengineyo, kushindwa kujua nini kitafuata, maana hali ya hewa haitabiriki, na kila mtu anatabiri juu ya kutotabirika huko.

 

Sisi tulikuwa tumepanga kuondoka hapa ninapoishi wanapoita White City ndani ya Jiji la London, na kwenda kusini magharibi mwa England. Mipango ilikuwa kutumia usafiri wa treni, ili iwe kama “adventure” kwenye maeneo mbalimbali ambayo tungepita na kufanya utalii tuliokwishalipia na vibali vyake vinakwisha muda wake mwaka huu.

 

Sasa watu wa hali ya hewa na wale wa kampuni ya usafiri wa treni, mahsusi hii ya First Great Western, wanasema tusisafiri huko. Kisa cha haya yote ni mvua kubwa iliyonyesha na matatizo yatokanayo na hali hiyo, pamoja na mvua kubwa zaidi zilizotabiriwa kunyesha wakati wa sikukuu, japokuwa huenda ikabadilika kutokana na “predictable unpredictability” ya hali ya hewa.

 

Kiangazi cha mwaka huu kilichukuliwa kuwa kikali sana, wakafika mahali wakaona kama maji yanaisha nchini. Hatua kali zilianza kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuzuia matumizi ya maji kwa mipira ya kumwagilia au kuosha magari na vitu vingine. Kulikuwa na kipimo cha mwisho cha kutumia maji, wakawa wanasema mambo haya hayajawahi kutokea miaka mingi, na hawajui ukame huo utaifikisha wapi nchi.

 

Lakini baada ya muda ikanyesha mvua ya haja, mafuriko yakaingia hadi kwenye makazi ya watu, helikopta zikaruka kama nzige wa Namugongo, Uganda kuokoa watu. Baada ya tathmini, Waingereza wakasema hicho kilikuwa kiangazi chenye mvua kubwa zaidi Uingereza katika miaka mingi. Sasa kipupwe kikaja, miti ikapukutisha majani wakasema msimu wa baridi kali umeingia, au tulivyozoea kusema hata hapo Bongo, kiwinta kikali.

 

Huwa hakuna mvua kubwa sana iliyozoeleka wakati wa baridi kama huu isipokuwa barafu. Lakini mvua imeendelea kunyesha kitambo sasa, na kina cha maji (water table) kipo juu sana maeneo mengi ya nchi.

 

Theluji ilianguka kiasi hasa kaskazini, lakini baridi ilipokwenda hadi nyuzi hasi tano kule kusini, watu walidhani theluji ingedumu hadi Krismasi. Halmashauri zikaanza kumwaga chumvi barabarani ili magari yaweze kupita kwenye mabonge ya barafu.

 

Iliyeyuka chapuchapu na sasa ni stori za mvua zaidi. Watu wamekuwa wakiokolewa kutokana na wingi wa maji kujaa maeneo mengi, inakuwa kama pale Jangwani karibu na uwanja wa mpira wa Yanga wakati wa mafuriko ya Mto Msimbazi.

 

Kuna maeneo yametolewa onyo la rangi nyekundu kwamba kuna hatari ya maisha, hayo ni mawili katika Cornwall na mengine mawili huko Devon. Mimi si mkazi wa sehemu yoyote ya huko, lakini rafiki zangu wanakaa huko na wameanza kuhamishwa.

 

Shirika la Mazingira limetoa maonyo 100 ya madhara na mengine zaidi ya 320 ya mafuriko kwa ujumla, yanayoweza au kutoweza kuwa hatari katika England na Wales. Uskochi nako kuna maonyo 15. Wasomi wanapanga kila siku kwa kusoma kwenye kompyuta na utafiti mwingi, lakini bado Uingereza na kuendelea kwake kote haijaweza kudhibiti majanga ya asili.

 

Acheni Mungu aitwe Mungu tu, maana pamoja na werevu wote na utajiri wote, bado kwenye utabiri wa hali ya hewa na udhibiti vinabaki mbali nao. Sasa Krimasi na Mwaka Mpya vinaliwa tu hapa hapa London, kama ni bata ni kununua na kuchinja hapa, hakuna tena kusafiri hovyo – kila mtu abaki alipo.

 

Si Tanzania tu ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwamba inatoa habari za hali ya hewa baada ya matukio badala ya kutabiri. Hapa pia wanatabiri lakini inakuwa tofauti kidogo au hawatarajii kwamba maafa yangekuwa makubwa kiasi hicho. Heri ya Noeli na Mwaka Mpya wana-Jamhuri.

1208 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!