Mwimbaji Nyota wa Muziki wa Taarab nchini, Hussein Mohammed ‘Hammer Q’ (pichani kushoto) amesema kuwa alifanya muziki wa bongo fleva kama njia ya kutafuta njia ya kufanikiwa katika tasnia ya muziki.

Hammer ameupa kisogo muziki bongo fleva na kugeukia muziki wa taarabu amesema hayo alipozungumza moja ya kituo cha televisheni  hapa nchini kuhusu maendeleo ya muziki wake. Mwanamuziki huyo amesema kuwa muziki wa bongo fleva ni mwepesi kwa sababu wanamuziki hawaumizi vichwa.

 

“Muziki wa bongo fleva ni wa kawaida sana kwa sababu msanii  anatengenezewa kila kitu studio, anachofanya yeye ni kuingiza maneno kwenye mdundo ambao umeisha tengenezwa na prodyuza,” amesema.


Tofauti na bongo fleva, msanii huyo amesema kuwa utengenezaji wa muziki wa taarabu ni tofauti na kuongezea kuwa siyo kazi rahisi kama ilivyo kwenye bongo fleva.


“Kama nilivyosema awali huko kwenye muziki wa taarabu ni kama vile kwenye muziki wa dansi, kwa sababu baada ya kutunga wimbo, unatakiwa pia kujua vyombo vitapigwaje, amesisitiza.


Msanii huyo  ambaye kwa sasa anafanya vizuri katika muziki wa taarab amesema kuwa kwa sasa ana imani kwamba anaweza kufanya makubwa zaidi katika tasnia ya muziki wa taarabu kutokana na uwezo alio nao kwa sasa.


Kauli ya Hammer Q inakuja wakati mwafaka ambapo vijana wengi wameona kuwa muziki ni kazi rahisi kwa baadhi yao kujaribu kwa kupitia katika stahili ile ya bongo fleva.


Hata hivyo muziki huo ambao kwa sasa unapewa kipaumbele na vituo vingi vya redio kwa kupigwa kila wakati, umeonekana kutodumu sokoni.


Baadhi ya wadau wamefikia hatua ya kuufananisha muziki wa bongo fleva kama kitu kinachotafunwa mara moja na kuisha muda wake kwa muda mfupi.


1409 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!