Julai 18, mwaka huu mtu mashuhuri kutoka Afrika Kusini alifariki dunia baada ya kupata matatizo ya afya wakati akikwea Mlima Kilimanjaro. Huyu ni dereva wa magari ya mashindano na mtangazaji wa runinga, Gugu Zulu.

Kifo chake kimezua mjadala juu ya hatari zinazohusiana na kukwea Mlima Kilimanjaro. Kila mwaka, wastani wa watu 10 hufariki dunia wakikwea Mlima Kilimanjaro; sawa na wastani wa mtu mmoja kwa kila siku 36.

Kabla hujaamua kuwa kukwea Mlima Kilimanjaro ni suala la hatari, tafakari kuwa mwaka 2013 watu 16,211 walikufa kwa ajali za barabarani. Idadi hiyo ni karibia watu wanne kufariki kila siku. Kwa kifupi, kuna tishio kubwa zaidi kuwa barabarani wakati wowote kuliko kuamua kukwea Mlima Kilimanjaro.

Lakini kifo ni kifo tu, na ndio sababu hata Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amelazimika kutoa tamko akijitetea na kukanusha kuwa Serikali inapaswa kulaumiwa.

Mtu yeyote anayeamua kukwea Mlima Kilimanjaro, au mlima wowote ambao una urefu unaozidi mita 3,000 kutoka usawa wa bahari anapaswa kutambua kuwa anajiweka kwenye hatari ya kuathiriwa na upungufu wa hewa ya oksijeni, au hypoxia kwa lugha ya Kiingereza; hewa ambayo iko kwa wingi kwenye usawa wa bahari, lakini hupungua kadri mtu anavyopanda juu kuelekea kwenye maeneo ya miinuko. Na ndio athari zilizosababisha kifo cha Zulu.

Ni tatizo linaloathiri asilimia 77 ya watu wote wanaokwea Mlima Kilimanjaro. Wengi wao huishia tu huumwa kichwa, kutapika, kupata kichefuchefu na kuharisha, lakini kama ambavyo imetokea kwa Zulu, wapo wanaofariki dunia.

Tunaweza kusema kuwa kosa kubwa ambalo wale wanaotangaza safari za kukwea Mlima Kilimanjaro hufanya ni kutokusisitiza vya kutosha kuwa kukwea Mlima Kilimanjaro si jambo rahisi.

Mimi nimeshafika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro zaidi ya mara saba, lakini wakati wote ninapokuwa kwenye misafara hiyo sijawahi kufikia uamuzi kuwa ni jambo rahisi, na mara zote huwa najiuliza ni nini kilichonipeleka huko.

Watu waliobobea katika kukwea milima duniani wanasema kuwa kukwea Mlima Kilimanjaro ni suala rahisi kulinganishwa na kukwea milima mingine, na linaweza kufanywa na mtu yeyote ambaye ana hali ya wastani tu ya afya, au mtu ambaye amejiandaa kwa mazoezi kwa miezi mitatu.

Na hii ndio hoja ambayo inatumiwa mno kuwavutia watu wa aina mbalimbali duniani kuweka nia na kufunga safari ya kuelekea kwenye kilele cha Uhuru.

Pamoja na kuvutia watu wengi, ukweli unabaki kuwa Mlima Kilimanjaro hautabiriki. Anayedhaniwa kuwa ana hali nzuri ya afya kuliko wote anaweza kushindwa kufika kileleni, wakati yule ambaye anaonekana goigoi anaweza kuwashangaza wote na kufika kileleni. Katika misafara yangu nimekutana na vikongwe waliofika kileleni, na kupishana na vijana mabaunsa walioteremshwa chini baada ya kushindwa kufika kileleni.

Hali kadhalika, wapo wanaotangulia kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa afya zao kabla ya kukwea Mlima Kilimanjaro ambao wataambiwa kuwa wana hali ya afya inayowaruhusu kupambana na mlima huo, lakini wakaanza mpambano huo na kujikuta wana tatizo la afya ambalo halikuonekana.

Wapo wanaojiandaa kwa kila namna na wasifanikiwe kufika kileleni, na wapo wasiojiandaa vya kutosha na wakafanikiwa kufika kileleni.

Lakini tukirudi kwa Zulu ipo sababu nyingine ambayo inaweza kuwa imechangia yaliyomkuta. Zipo njia saba zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro za kupita kuelekea kwenye kilele cha Uhuru; zote zikiwa na ugumu unaotofautiana.

Zulu na wenzake walitumia njia ya Marangu ambayo huitwa pia njia ya Coca Cola. Maandiko karibu yote kuhusu njia hizi yanashauri kuwa njia ya Marangu ni njia rahisi kwa sababu inatumia muda mfupi kufika kileleni na kwa sababu haina miinuko mikubwa kwa siku mbili za mwanzo.

Uzoefu wangu ni kuwa njia ya Marangu ni mojawapo ya njia ngumu za kufika kileleni kwa sababu haimwandai vya kutosha mtu anayekwea Mlima mrefu kama Kilimanjaro kwa mara ya kwanza.

Ni njia inaoyomfanya mtu abweteke kuwa suala la kufika kileleni ni rahisi kwa sababu ya urahisi wake wa siku mbili za mwanzo. Tatizo linaanza usiku wa siku ya tatu; siku ya kuelekea kileleni ambako, ghafla unapambana na mwinuko mkali ambao unaharakisha kasi na athari za kupungukiwa hewa ya oksijeni; athari ambayo inawakumba zaidi watu wanaoishi kwenye maeneo ambayo yapo karibu na usawa wa bahari.

Tofauti na njia ya Marangu, njia nyingine kama Lemosho zinauandaa mwili kuzoea pole pole ile hali ya kupungukiwa na hewa ya oksijeni na hivyo kuongeza ustahimilivu wa mwili wa kukabili miinuko ya juu zaidi siku ile ya kuelekea kileleni.

Kwa wale wanaotafuta mchawi, kifo cha Zulu hakina mchawi yeyote. Kampuni zote zinazoongoza watu kukwea Mlima Kilimanjaro hutoa tahadhari juu ya safari hiyo, na wote wanaolekea huko hufahamu au wanapaswa kufahamu kuwa si suala rahisi na lina hatari zake.

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya mumewe, mke wa Zulu; Letshego alisema kuwa ataanzisha harambee ya kuchangisha pesa ili kianzishwe kituo kidogo cha afya kikiwa na daktari wakati wote kwenye kambi ya Horombo, kambi ya mwisho inayopitwa kwenye njia ya Marangu kuelekea kileleni ili waathirika waweze kupata huduma ya matibabu mapema.

Ilivyo sasa ni kuwa vikosi maalumu vya kuhudumia waathirika huwateremsha kwa machela waathirika na kuwapeleka kwenye hospitali za Moshi kupata matibabu.

Tiba kubwa ya hypoxia ni kuteremshwa mwathirika haraka, hatua ambayo inaongeza kiwango cha hewa ya oksijeni anachovuta. Watu wengi wanapona kwa kuwateremsha chini tu. Lakini wale walioathirika zaidi na ambao wanahitaji huduma ya tiba haraka wanaweza kupata ahueni kubwa zaidi iwapo watapata huduma ya matibabu mapema. Kwa hiyo wazo la Letshego likitekelezwa litaleta manufaa.

Kutekelezwa kwa wazo hili kikamilifu, awepo daktari siyo tu kwenye kambi ya Horombo, bali pia kwenye kambi ya Barafu ambayo ni kambi ya kwanza kwenye njia nyingine ya kuteremka kutoka kileleni.

Wataalamu wanaochunguza ajali za ndege husema kuwa kila inapobainika sababu ya ajali huongeza usalama wa abiria wa ndege. Sababu za athari za kukwea Mlima Kilimanjaro zinajulikana. Lakini labda kwa umashuhuri wa Gugu Zulu tunaweza kuona mabadiliko ambayo yataongeza usalama wa wengine wanaovutiwa kukwea Mlima Kilimanjaro.

1462 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!