Hati ya nyumba yako inapoharibika au kuchakaa

Hati kwa maana ya hapa ni hati za nyumba na viwanja, kwa ufupi ni hati za ardhi. Kwa kuwa hati ni karatasi sawa na karatasi nyingine basi huweza kuharibka au kuchakaa.

Huweza kuchakaa kwa sababu mbalimbali za kibinadamu. Inaweza kunyeshewa na mvua au kumwagikiwa na maji kwa namna yoyote ile, inaweza kuungua moto na wakati mwingine inaweza kuharibika kutokana na majanga ya ajali za barabarani n.k. Muhimu ni kujua tu kuwa hati huharibika na ziko sababu nyingi za msingi.

 

1. Sheria ya usajili wa hati

Ofisi ya msajili wa hati hutekeleza shughuli zake chini ya Sheria ya Usajili wa Ardhi sura ya 334, (The land registration Act Cap 334). Ni katika sheria hii ambamo habari zote kuhusu usajili wa hati hutolewa. Sheria hii hueleza namna na nyaraka mbalimbali zinazohitajika katika kusajili hati. Sheria hii ndiyo mwongozo wa jumla katika masuala mazima ya hati.

 

2. Faida unazopata kupitia ofisi ya usajili wa hati na haraka

Ofisi ya usajili wa hati haishughuliki na usajili wa hati pekee bali pia kupitia ofisi hii nyaraka mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi nazo husajiliwa. Unaweza kusajili maombi ya zuio kwa kuzuia hati kubadilishwa. Hii hutokea iwapo una wasiwasi kuwa kuna mtu anataka kuuza eneo lako au pengine mmoja wa wanafamilia anataka kuuza bila ridhaa ya mwingine/wengine. 

Pili, kupitiaofisi hizi unaweza kusajili jina jipya. Kwa wale wanaobadilisha majina na kupata majina mapya basi majina hayo husajiliwa ofisi hizi. Jina jipya haliwezi kuanza kutambulika rasmi bila kusajiliwa katika ofisi hizi. Majina ni haya ya John kuitwa Rashid n.k.

Tatu, kwa wale wenye taasisi  ndogo za kutoa mikopo hata wale wa vicoba, basi huweza kusajili mikopo kupitia ofisi hizi. Nasema wenye taasisi ndogo kwa kuwa wale wenye taasisi kubwa wanalijua hili. Ili mkopo uwe salama zaidi huwa unasajiliwa, na hivyo ofisi zinazohusika na kusajili mikopo ni hizi. Mkopo husajiliwa chini ya sheria ya mikopo (Mortgage Financing Special Provision) Act No. 18/2008).

Nne, ofisi hizi hutunza kumbukumbu za masuala yote ya ardhi na hivyo kwa wanaotaka rejea ya kumbukumbu huweza kufika ofisi hizi na kupata rejea hiyo. Ni vyema ukitaka kununua ardhi kupata rejea ya ardhi unayotaka kununua kupitia ofisi hizi.  Hatua hii huepusha mgogoro.

Kwa kutaja ni machache lakini yapo mengi ambayo unaweza kupata kupitia ofisi za usajili wa hati na nyaraka.

 

3. Ninini ufanye iwapo hati imeharibika/kuchakaa

Hati inapoharibika katika mazingira niliyoeleza hapo juu basi unayo hiari ya kufuatilia na kupata hati nyingine. Mamlaka za ardhi zilizokuwa zimetoa ile hati ya mwanzo iliyoharibika ndizo hizo hizo zitakazotoa hati nyingine mpya. Ili usipate usumbufu katika kukamilisha muamala huu ni vema ukaandaa nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kazi hiyo.

(a) Andaa picha nne kwa maana ya saizi ya pasipoti. Picha hizo ziwe za mtu yuleyule aliyekuwa kwenye ile hati iliyoharibika. 

(b) Ikiwa hati imeharibika pamoja na nyaraka nyingine ulizokuwa umetumia awali kuombea hiyo hati, basi ni vema nyaraka hizo nazo ukaziambatanisha na ukaenda nazo katika mamlaka ya ardhi. Nyaraka hizi ni zile ambazo huitwa fomu za maombi.

(c) Hati iliyoharibika ni lazima nayo uiambatanishe. Bila kujali imeharibika kiasi gani lakini la muhimu ni kuwa unapoenda kuomba hiyo nyingine basi ambatanisha na hiyo iliyoharibika.

(d) Ni lazima uwe na risiti za malipo ya kodi ya ardhi. Hata kama wakati hati inaharibika ulikuwa hujalipia kodi ya ardhi, basi ni bora kabla ya kuanza kufuatilia hati mpya ukahakikisha umelipa kodi ya ardhi na hudaiwi. Mchakato hauwezi kufanyika iwapo unadaiwa kodi ya ardhi.

(e) Pia ipo ada maalum ya usajili mpya ambayo utatakiwa kulipia. Ada hizi hubadilikabadilika na hivyo si vema makala kutaja kiwango. Hata hivyo, malipo ya ada ni hatua ya mwisho kabisa unapokuwa umekamilisha maandalizi ya hapo juu. Ukiwa kwa msajili utaelezwa ni kiasi gani utatakiwa kulipia ambapo risiti ya Serikali hutolewa. 

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.