Tunajaribu kutabiri yasiyotabirika

Baada ya uchaguzi wa Rais John Magufuli, mada iliyotawala mazungumzo maeneo mengi ya Tanzania ilikuwa nani atateuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Juma lililopita nilikaa kwenye mazungumzo ya aina hiyo na wanakijiji wenzangu na majina mengi yalitajwa. Majina mengi hayakupewa nafasi hata kidogo. Wengine walipendekeza hata Watanzania ambao si wabunge. Na kama walivyo Watanzania wengi, nami nilichangia mawazo yangu. Nikasema inawezekana atatajwa mtu ambaye hatujawahi kumsikia sana.

Muda ulipowadia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano alisoma barua ya Rais Magufuli na kutamka: “…Rais Magufuli amemteua…Mbunge wa Ruangwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuwa ndiye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Kuacha wale wanaofuatilia kwa karibu masuala ya kisiasa, na kuacha wapiga kura wake wa jimbo la uchaguzi, naamini Watanzania wengi walianza kuuliza maswali. Mbunge wa wapi? Kassim nani? Na Rais Magufuli naye alifanikisha kujitokeza kwa maswali mengi mpaka dakika ya mwisho kwa kuandika barua yake kwa mkono na kuifunga kwenye bahasha tatu na kwa kumtuma mpambe wake aiwasilishe bungeni. Yalijitokeza maneno ya mtaani kuwa inawezekana Rais Magufuli alimsindikiza mpambe wake mpaka bungeni na akawa anamsubiri nje ili awe na uhakika kuwa jina lile litabaki siri hadi dakika ya mwisho.

Kabla ya jina kufahamika, taarifa za baadhi ya vyombo vya habari zilimworodhesha Waziri Mkuu Majaliwa kwenye orodha ya majina ya wengine wengi ambao walionekana kuwa na sifa za kuteuliwa. Ni mwandishi mmoja tu, akiandika kwenye mtandao mmoja wa jamii, aliyemtaja Mheshimiwa Majaliwa.

Hulka ya kubashiri yasiyobashirika sasa imekuwa sifa mojawapo ya wengi. Lakini haitakuwa sahihi kusema kuwa ni tatizo la Watanzania pekee. Haja ya kufahamu yatakayotokea kesho, wiki ijayo, au mwaka kesho, ndiyo kielelezo cha msingi cha sifa za mwanadamu. Tunapoweza kutabiri yale yanayoweza kutokea, tunaamini kuwa na uwezo wa kukabiliana vyema na hayo yatakayotokea, na kupanga maisha yetu ipasavyo. Lakini hayo yangekuwa kweli zaidi kwa mkulima ambaye anabashiri kuwapo mvua za kutosha za kustawishia mazao yake kuliko kutabiri nani atakuwa waziri mkuu.

Kweli, waziri mkuu asiye bora anaweza kudhoofisha nia ya Serikali ya kutekeleza mipango yake na kuathiri hali ya maisha ya wananchi wote. Tunapotaja majina ya wale tunoatarajia kushika uongozi wa juu serikalini tunachagua mtu ambaye tunaamini ataleta neema, siyo mtu ambaye kila siku atakuwa mada ya ubovu wa uongozi na msukumo wa mawazo mapya kwa wachora vibonzo.

Tunapounganisha “Hapa Kazi Tu” na kupokea kauli mpya ya “Sasa Kazi Tu” na hayo mawili yakaleta mabadiliko chanya, tuajenga msingi kwenye kumbukumbu zetu kuwa tuyaoyatabiri leo yanaweza kuleta matokeo ambayo tunayataka na tunayatarajia baada ya miaka kadhaa.

Lakini imani kwamba, leo hii, tunafahamu kuwa Waziri Mkuu Majaliwa ndiye chaguo bora kuliko wote inabaki kuwa imani. Kama alivyotamka Rais Magufuli kwenye hotuba yake ya bungeni Novemba 20, mwaka huu, ni baada ya miaka mitano ndiyo tutawapima viongozi wetu kuona kama tulifanya uamuzi mzuri.

Nchini Tanzania wapiga kura waliyo wengi si wanachama hai wa vyama vya siasa. Lakini wote hao, pamoja na wale wa vyama vya siasa ambao walikuwa wana uhakika kuwa chama chao kitashinda uchaguzi mkuu, bado hufanya utabiri kwa misingi ya imani na matumaini, lakini bila kufanya hivyo kwa misingi ya ukweli.

Na mara nyingi tabiri zetu tunazikosea, kama ambavyo haya ya uchaguzi wa Majaliwa Kassim yalivyothibitisha. Na hapa ni mwanzo tu wa mapambano, kwa kuwa upo muda mrefu wa kupima iwapo hilo ni chaguo sahihi. Mashabiki wa soka wanasema mechi inaisha baada ya dakika tisini pamoja na zile dakika za ziada.

Hivi karibuni Taifa Stars ilipoongeza bao la pili dhidi ya timu ya taifa ya Algeria nilianza, hata kabla ya mechi kwisha, kutabiri kuwa mambo yanaelekea kuwa mazuri huko mbele. Dakika tisini baadaye, nikabaki najiuliza sababu ya kukaa muda wote ule kutazama ile mechi.

Matokeo ya mechi ya marudiano ambako Taifa Stars ilifungwa mabao saba bila majibu, ndiyo ikathibitisha kuwa masuala ya utabiri hayana uhusiano mkubwa sana na yatakayotokea. Ukweli huo upo kwenye michezo, na ukweli huo upo pia kwenye siasa.

Katika siasa tabiri zetu na matokeo yake yanapooana hatuna budi kujipongeza hadharani. Matokeo ya uchaguzi mkuu yalipomdhihirisha Rais Mteule John Pombe Magufuli nilisikia wengi wakisema kuwa ndiye waliyempigia kura. Tunajitokeza hadharani kuthibitisha kuwa yale tuliyotarajia yametokea, lakini hatutaji hadharani uwezo wetu hafifu wa kutabiri yasiyotabirika.

Jambo jema ni kuwa fursa za kutabiri tena na tena haziishi. Tunapokosea tunayo fursa ya kumfukuza kocha na timu yake ya ufundi ifikapo Oktoba 2020, kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Lakini jambo la msingi ni kuwa tunapokosea katika tabiri zetu juu ya safu ya uongozi na matarajio mema ambayo tunayasubiri kutokana na uongozi wao tunaumia wote – kuanzia wale wasio wanachama wa vyama vya siasa, hadi kwa wale ambao ni wanachama.

Na makosa hayo tunaweza kuyabeba kwa miongo kadhaa, hata kwa wale ambao leo hii hawajazaliwa. Tunapopatia inakuwa neema kwa wote, hata kwa wale waliopinga yanayotokea sasa.

Kwa sasa natafuta fursa ya kukaa tena na wanakijiji wenzangu kuwaambia: “Si niliwaambia?”