Tumechezewa, tumechakachuliwa, sasa yatosha

“Mmetuchezea vya kutosha, muda sasa umekwisha. Mmetuchakachua vya kutosha, muda wa kuchakachuana umekwisha. Nataka iwe kazi tu…”

Ni baadhi ya maneno yaliyotamkwa na Rais John Pombe Magufuli, alipokuwa anazindua Bunge la Muungano la Tanzania la 11 Ijumaa, Novemba 20, 2015, mjini Dodoma.

Maneno hayo kwa ujumla wake ni makali mithili ya upanga na mazito mfano wa mchanga uliyolowana maji na ni muhari kwa Mtanzania ye yote mpenda nchi yake Tanzania. Maneno hayo yametamkwa na binadamu na yanakwenda kwa binadamu.

Kwa desturi binadamu ni kiumbe hai chenye uwezo wa kufikiri, kupima fikra nzuri na mbaya na kutenda mambo mema pia na maovu. Lakini lenye asilimia kubwa ni matendo mema miongoni mwa binadamu. Kinyume cha hivyo ni unyama wenye asili ya wanyama.

Kauli “Mmetuchezea na mmetuchakachua vya kutosha…” si ya kupuuzwa hata kidogo kwa binadamu mpenda maendeleo na mtaka haki, amani na utulivu. Sina uhakika Watanzania wangapi tumemsoma na kumuelewa Rais John Pombe Magufuli! 

Naomba samahani kutamka yafuatayo kwako msomaji wa makala haya, iwapo ni kweli wanaCCM wanataka mabadiliko ya kweli; Wapinzani na UKAWA wanataka mabadiliko; Vijana wanahitaji maisha nadhifu na Wazee wanahitaji maisha ya matumaini na bora, kauli hiyo ya rais ni mwongozo wa kuelekea kwenye mabadiliko ya mahitaji yetu.

Tumesema na tumeimba sana kwa muda mrefu kuhusu utajiri wa nchi yetu na umaskini tuliyonao uanavyisigana na uhalisia ya mali zilizopo nchini. Umaskini huu tumeuleta wenyewe kwa kukubali kuchezewa kama mwanasesere na kuchakachuliwa kama mafuta ya taa na dizeli katika soko la magendo.

Sasa lazima tubadilike madhali tumempata kiongozi mkohozi wa pumu na mwenye kucha za kukuna upele. Lakini haitoshi kuwa na mtu mwenye sifa hizo iwapo sisi Watanzania hatutakuwa pia wakohozi wa vikohozi wala wakunaji upele. Bila ya hivyo kamwe hatuwezi kuwashinda maadui wetu umaskini ujinga na maradhi.

Ukweli Rais Magufuli ametoa dira ya nchi. Ameahidi kupambana na rushwa, ufisadi, dawa za kulevya, uzembe na kufuta warsha makongamanona safari za nje ya nchi n.k. kwa lengo la kutaka kulinda mali na hazina ya nchi na kukuza pato la mtu pamoja na kukuza uchumi wa taifa ili serikali iwe na uwezo wa kutoa huduma bora katka afya, elimu, maji na miundombinu ya usafiri na usafirishaji nchini.

Yote hayo yanawezekana iwapo tu sisi walalahoi na wale wenye afueni tukiwa kundi moja na kutumia vyema ndimi zetu na vitendo vyetu vikiwa havina mashaka tutawashinda maadui zetu watatu na watatoweka nchini. Na hiyo ndiyo tafasiri nyepesi ya “ Nataka iwe kazi tu” ya Rais Magufuli.

Kasi anayokwenda nayo Rais John Magufuli katika serikali yake haina dalili ya nguvu ya soda, moto wa mabua au vifuu, kama baadhi ya Watanzania wanavyosema na kuamini au wanavyokejeli. Ukweli tumekwisha uona katika kauli na vitendo vyake. Hili halina ubishi.

Utendaji wake umejichomoza na kuonekana katika maeneo ya mapato, matumizi ya hazina yetu na katika usimamizi wa utoaji huduma za jamii hospitalini, shuleni, vyuoni, viwandani na mashambani. Watu wameshaona hali na mwendo huu si wa kawaida.

Kwa mtaji huu anaokwenda nao heshima na usiri wa serikali katika kazi zake unaonekana. Wapambe na wale pangu pakavu tia mchuzi hawana chao, wamekwendakapa. Serikali lazima iheshimike.

Serikali lazima iwe na kauli ya muungurumo wa kusitua na kutetemesha wapuuzi na hapo ndipo inapoogopwa. Haiwezi kuchezewa kama pusi na mkia wake. Duniani kote serikali zinaheshimika na kuogopwa. Serikali inayotiwa mfukoni na mafisadi na wala rushwa si serikali ni asali. Na mwisho wa kuramba asali ni kufilisi mali ya nchi.

Rais Magufuli anasema,” Yatosha na muda sasa umekwisha, hapa kazi tu.”  Kauli hiyo naona ni pacha ya kauli ya serikali ya awamu ya kwanza ya Rais, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  chini ya Azimio la Arusha isemayo kwamba, “ Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndiyo uliyotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi…”

Kumbuka msomaji, mapinduzi ni mageuzi na ni mabadiliko. Leo tunahitaji mabadiliko ya kweli. Mabadiliko ya kweli hayana ubaguzi wa itikadi ya chama, udini, ukabila wala ukanda. Na zaidi hayana ujinsi, rangi wala rika. Tanzania ni moja inahitaji nia moja ya kuleta na kujenga mabadiliko ya kweli. Hili limo ndani ya uwezo wetu na linawezekana pasi na figisufigisu.