Damian+Lubuva_NEC2Waliosoma maandishi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji Mark Bomani, watakubaliana na mawazo yake.
Hoja yake kuu ni kwamba Katiba mpya katika mazingira ya sasa ya nchi yetu, haiwezekani. Kwa maana hiyo hatuwezi kuwa na Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa kutumia Katiba mpya.


Jaji Bomani, mtu mzoefu wa shughuli za Serikali, anashauri Katiba ya sasa iendelee kutumika, lakini baada ya kufanyiwa marekebisho hata kwa kutumia hati ya dharura katika Bunge.
Mtazamo wake ni kama ule wa wanasiasa waliopendekeleza kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba kwa kuruhusu baadhi ya mambo kama Tume Huru ya Uchaguzi, wagombea binafsi, uwiano sawa wa kijinsi kwa madiwani na wabunge, na kadhalika.
Kwa hakika wale waliosoma mawazo ya Jaji Bomani watakubaliana naye. Hatuna muda wa kufanya mambo mengi ambayo wakubwa wangependa yafanywe ndani ya miezi hii isiyozidi mitano kabla ya Uchaguzi Mkuu.


Tupo tunaomuunga mkono Jaji Bomani kwa sababu anayoyazungumza hayahitaji mtu kuwa na ujuzi mkubwa wa kielimu kuweza kuyaelewa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva anaweza kuiokoa au kuiangamiza Tanzania. Uamuzi wake wowote utakuwa na athari hasi au chanya kwa mustakabali wa Taifa letu.


Uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na uchaguzi wa aina hii wa miaka iliyopita. Mwaka 1995 joto la Uchaguzi Mkuu lilikuwa kubwa. Kulikuwa na viashiria kadhaa vya ujivunjifu wa amani. Sina hakika, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba kuwapo kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kuliweza kusaidia kuivusha Tanzania kwenye kipindi hicho.
Mwalimu aliheshimika mno miongoni mwa wananchi, lakini pamoja na ukweli huo, wapo baadhi ya wananchi waliodiriki kwa wazi kabisa kumpinga kwa hoja na wengine kwa nguvu. Kwa mara ya kwanza wapo wananchi waliodiriki kumpopoa Mwalimu kwa mawe jukwaani kwa sababu tu alimnadi mgombea ambaye kwao hakuwa chaguo lao.


Wapo wanaoamini kuwa ni Mwalimu ndiye aliyeweza kupunguza na hata kufifisha nguvu za Augustine Mrema.
Mwaka 2005 joto la Uchaguzi Mkuu lilipanda, lakini kwa bahati nzuri Rais Benjamin Mkapa, akajitahidi kuivusha nchi kwenye wakati huo. Wapo wanaoamini kuwa Mzee Mkapa hakumtaka Jakaya Kikwete, lakini kwa kusoma alama za nyakati na mwelekeo wa umma, alilazimika kukubaliana na matakwa ya wengi.


Mzee Mkapa, hakutaka kuona Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikimfia.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu una mambo mengi. Demokrasia imeendelea kupanuka. Wananchi wamekuwa wawazi zaidi. Idadi ya wanaojitambua na kutambua haki zao za kidemokrasi imeongezeka. Woga dhidi ya viongozi wa dola umepungua.
Changamoto hizi na nyingine ambazo sikuzitaja, zinaufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uwe wa aina yake. Matarajio ya wananchi wengi ni kuona wanampata kiongozi mkuu wa nchi mwenye uthubutu wa kupambana na hatimaye kuyashinda matatizo mengi yanayowakabili.
Matatizo kama ya ajira, rushwa, upendeleo, ukosefu wa haki katika vyombo vya utoaji haki, dhuluma, unyanyasaji ni baadhi ya mambo yanayowakera wananchi.


Wapigakura wanataka wampate kiongozi mkuu atakayerejesha umoja wa Watanzania kutoka kwenye mgawanyiko na ubaguzi wa rangi, dini, kabila, kanda, jinsi na tofauti ya kipato kati ya walionacho na wasionacho.
Kiu ya Watanzania ni kuona utawala wa sheria unarejeshwa ili kuondoa hali hii ya sasa ya kila mtu kujiamulia kufanya jambo kadri ya utashi wake.


Ukosefu wa huduma za kijamii kama elimu, maji safi na salama, afya na nyingine, unawasukuma Watanzania wengi wenye sifa sasa kuwa na kiu ya kushiriki Uchaguzi Mkuu.
Kwa mara ya kwanza tunasikia na kushuhudia taarifa za Watanzania wanaojihimu alfajiri kwenda kupanga foleni kwa ajili ya kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura. Haya ni mabadiliko makubwa.


Ukosefu wa huduma za afya, uonevu katika vituo vya Polisi na rushwa katika Mahakama zetu ni mambo ambayo wapigakura wa Tanzania wanaamini kuwa sasa yanaweza kukomeshwa kwa kutumia sanduku la kura.
Foleni za magari katika majiji makubwa kama Dar es Salaam ni mambo mengine ambayo wapigakura katika maeneo hayo wangependa kuona wanapata Serikali yenye kuwaondolea kero hiyo.


Ni kwa kuzingatia haya na mengine mengi, ndiyo maana nasema Jaji Lubuva atambue dhima aliyonayo kwa Taifa letu. Namna yoyote ya kuwafanya Watanzania wasijiandikishe kwenye kwenye Daftari kwa sababu yoyote ile, iwe ya BVR au nyingineyo, haitakubalika kwa Watanzania hawa.
Namna yoyote ya kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni kama kujaribu kuwasha moto kwenye debe lenye petroli.


Wananchi wanahitaji mabadiliko ambayo kama nilivyokwishasema, wametambua kuwa yatapatikana kupitia kwenye sanduku la kura.
Sisi tulio mitaani tunaziona na kuzisikia hasira za wananchi dhidi ya Serikali ya sasa. Wanalalamika kweli kweli juu ya ufisadi. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyotolewa wiki iliyopita imezidi kuwatia hasira. Wimbo wa wizi fedha za umma umewachosha. Kila mwaka ripoti ya mwaka huo inakuwa mbaya kuliko ya mwaka uliopita.


Wanasoma na kuona namna Serikali hii ‘sikivu’ ilivyotia nta kwenye masikio kwa kukataa kuwaondoa wabunge kwenye bodi za mashirika na taasisi za umma.
Wanasoma na kuona namna kila mwaka marehemu wanavyoendelea kupokea mishahara kupitia Hazina.
Wanasoma namna wakubwa wanavyotafuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Wanaonyeshwa kila aina ya vielelezo vya namna wakubwa wanavyofuja mabilioni ya shilingi za walipakodi.


Mbaya zaidi, wanaendelea kusikia wimbo ule ule wa Serikali wa “Tutawashughulikia wala rushwa wote”. Badala yake wanachoshuhudia ni kukamatwa kwa dagaa ilhali wale mapapa wenyewe wakiachwa watambe.
Wananchi wanaambiwa wahame sehemu zisizoruhusiwa kujengwa, lakini hapo hapo wanaona mahekalu ya wabunge na wakubwa wengine yakijengwa kwenye mikondo ya mito na bahari.


Haya yanawatia hasira. Yanawafanya wakasirike kila wanaposikia uvumi wa kwamba Awamu ya Nne ina mpango wa kuongeza muda wa kuwapo madarakani. Hawataki kusikia kitu cha aina hiyo. Ndio maana Jaji Lubuva sasa anatazamwa na wengi. Anatazamwa kwa kutambuliwa kuwa ndiye anayeweza kuokoa au kuharibu mambo.
Kama BVR itaendelea kusumbua, na endapo wapigakura wenye uchu wa kupata mabadiliko wataona wanakosa kufikia kile wanachokitaka (kupiga kura), wanaweza kusababisha usumbufu katika Taifa letu.


Jaji Lubuva na wakubwa wenzake hawapaswi kulala. Hawana cha kuwafanya wanywe mvinyo kwa sasa. Alimradi waliikubali kazi hiyo, hawana budi kuhakikisha wanaitekeleza. Kama kweli Jaji Lubuva ana hakika ya kwamba uandikishaji wapigakura utafanikishwa, ahakikishe hilo linafanyika. Kama anajua kazi hiyo haiwezekani, ni heri akawa muwazi sasa badala ya kusubiri dakika za lala salama. Kwenye kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa wananchi walisema haiwezekani. Wanasiasa wakaapa kuwa inawezekana. Matokeo yake sote tumeyaona. Imeshindikana.
Kwa hiyo hata hili la kufanyika au kutofanyika kwa Uchaguzi Mkuu ni vema wananchi wakapata hakika ya mambo mapema.


Kwa ufupi ni kwamba Watanzania wana kiu ya kupata mabadiliko ya kweli. Mabadiliko yatakayoitoa Tanzania hapa ilipo kuelekea kwenye Tanzania yenye neema zaidi, Tanzania yenye kuwafaidisha Watanzania wote.
Narejea,  Jaji Lubuva atambue kwenye suala hili la Uchaguzi Mkuu liko mikononi mwake. Aliyempa nafasi hiyo keshawahakikishia Watanzania na walimwengu kwamba ameshachoka, na kwamba anachosubiri ni kustaafu na kwenda kuhangaika na maisha ya ustaafu. Jemedari anaposema kachoka, hapo hatuhitaji kuweka akili na nguvu nyingi kwake maana keshachoka! Kwa sababu hiyo, ni wajibu wa wasaidizi wa jemedari kuhakikisha wanaivusha nchi katika hali ya salama.


Sisi tulio mitaani tunayasikia mengi. Tunasikia namna vijana wanavyonung’unika. Tunawashuhudia maskini wanavyotaabika. Tunaona namna nchi yetu ilivyofikia hatua ya kila mmoja kufanya anachojisikia kukifanya. Tunahitaji uongozi mpya wa kurejesha matumaini ya Watanzania. Tunapaswa kuwa na dira ya kutuwezesha kuwa na malengo ya kutufikisha kwenye aina ya Taifa tunalotaka kulijenga.
Jaji Lubuva huu ndio muda wako wa kuthibitisha kuwa kuteuliwa kwako hakukuwa kwa bahati mbaya. Ukivurunda Uchaguzi Mkuu Watanzania watakulilia.

By Jamhuri