Baada ya kuona kuwa wameboronga elimu na wameendelea kusemwa vibaya, sasa Waziri wa Elimu na wasaidizi wake wamekuja na  jambo jipya kwa lengo la kujikosha. Wamekuja na mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN).

Mpango wa BRN ulizinduliwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, jijini Dar es Salaam, Agosti 15, mwaka huu. Utekelezaji wa mpango huo ulianza mwezi Aprili.

 

Wakati wa uzinduzi wa mpango huo, wakurugenzi wa taasisi mbalimbali za elimu za Serikali na maofisa elimu wa mikoa yote nchini, walikula kiapo cha kuhakikisha kuwa wanasimamia mpango huo kikamilifu. Wakashangaliwa sana. Tuanzie hapo.

 

Watu waliotakiwa kula kiapo pale ni walimu ambao ndiyo watekelezaji wakubwa wa mpango huo, si watu watakaosimamia utekelezaji wake.

 

Kasoro yetu kubwa Watanzania katika mipango yetu yote ni kutoshirikisha watekelezaji. Wakubwa watakutana, watapeana posho, na watajiridhisha kuwa wameanza vizuri bila kushirikisha watekelezaji.

 

Kilichotakiwa pale ni kila mkoa kuleta angalau walimu wawili; mmoja wa shule msingi na mwingine wa shule ya sekondari. Hao wangepewa nafasi angalau ya dakika tano tano za kuzungumzia changamoto (matatizo) zinazokabili sekta ya elimu shuleni.

 

Ni hao ambao wangekula kiapo kwa niaba ya wenzao – kiapo cha kutekeleza na wala si hiki cha kusimamia. Naweza kutamka bila kusita kuwa mpango wa BRN hautafanikiwa kama Wizara ya Elimu haitabadilika kimtazamo.

 

Lazima Wizara ya Elimu iheshimu walimu na iwasikilize. Usimamizi utakaofanywa na wakubwa hata kama utakuwa mzuri kiasi gani, hautafanikiwa kuleta Matokeo Makubwa Sasa.

 

Si usimamizi wa mpango huo utakaoleta mafanikio bali mambo wawili. La kwanza, wizara iweke utaratibu utakaotoa nafasi na uhuru kwa walimu kueleza matatizo ya elimu. Kwa sasa kuna mikutano ya kila mwezi ya walimu wakuu inayotumiwa kuwapa maagizo ya kutekeleza hiki na kile. Hawapewi nafasi ya kuuliza maswali wala kushauri.

 

Wakati umefika kwa wizara kuanzisha vikao vya kila mwezi vya walimu wa taaluma. Ni vikao vya kuzungumzia taaluma na elimu kwa jumla vitakavyofanikisha mpango huo wa Matokeo Makubwa Sasa na wala si vikao vya walimu wakuu vinavyoishia kupewa maagizo yanayohusu zaidi masuala ya utawala kuliko taaluma.

 

Jambo la pili linalotakiwa katika kufanikisha mpango huo, ni Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa walimu wanatimiziwa haki zao, ndipo watakapoweza kutekeleza mpango huo kikamilifu.

 

Leo, maelfu ya walimu wamepandishwa madaraja wengine tangu mwaka 2009, lakini hawajapandishiwa mishahara, watakuwa na furaha gani ya kutekeleza mpango huo wa Matokeo Makubwa Sasa?

 

Kwa kifupi, ni muhimu Wizara ya Elimu ichukue hatua sasa ya kumaliza uhasama uliopo kati ya walimu na Serikali. Lakini pia mipango mizuri ya wizara katika utekelezaji wa mpango huo, itasaidia kufanikisha mpango huo. Kwa sasa Wizara ya Elimu imekosa kabisa mipango vizuri.

 

Tazama! Wizara ya Elimu imepanga kuona Matokeo Makubwa Sasa katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba unaofanyika wiki mbili zijazo! Ni jambo ambalo halitawezekana.

 

Lakini pia tumeshuhudia mtihani uliotungwa na Baraza la Mitihani la Taifa kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la saba ukifanyika siku ya kufungua shule! Siku ya kufungua shule kwa vyovyote si siku nzuri ya kufanya mtihani.

 

Kwa hiyo, wanafunzi wengi hawakufanya mtihani huo ambao si kama tu haukutungwa vizuri bali pia haukusimamiwa vizuri. Katika mazingira hayo Matokeo Makubwa Sasa yatawezekana?

 

Mbali ya wananfunzi wa darasa la saba wanaotazamiwa kuleta Matokeo Makubwa Sasa katika mtihani wao wiki mbili zijazo, nao wanafunzi wa kidato cha nne wanatazamiwa kuleta Matokeo Makubwa Sasa katika mtihani watakaoufanya miezi miwili ijayo!

 

Kwa kweli ni ndoto kwa wanafunzi hao kufanya vyema mitihani hiyo katika muda uliobaki. Watanzania wanakubali kuwa si Wizara ya Elimu tu bali Serikali kwa ujumla imekuwa na mipango mizuri sana ambayo haikuzaa matunda yaliyotarajiwa kutokana na utekelezaji mbovu.

 

Chukua, kwa mfano, somo la stadi za kazi lilikusudiwa kuwasaidia wanafunzi wanaorudi nyumbani kujiajiri wenyewe. Lakini wanafunzi wanaorudi nyumbani hawajiajiri.

 

Wanashinda vijiweni kwa sababu walimu hawakupewa semina ya kuwasaidia kufundisha vizuri somo hilo, na ni somo ambalo halina vifaa vya kufundishia. Basi kama ni Matokeo Makubwa Sasa tuanze na somo la stadi za kazi.

By Jamhuri