Mgogoro baina ya Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mstahiki Henry Matata, na Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, unaendelea kufukuta na kujenga makundi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mgogoro huo ulianza mwaka jana muda mfupi baada kufanyika kwa uchaguzi wa kumpata  meya, naibu wake pamoja na wenyeviti wa kamati za kudumu za manispaa hiyo.

 

Mgogoro ulianza baada ya mbunge huyo na baadhi ya madiwani wanachama wa Chadema katika manispaa hiyo, kupinga uchaguzi uliompatia Matata umeya, kwa  madai kwamba haukufuata kanuni na taratibu za uchaguzi.

 

Inaelezwa kwamba idadi ya madiwani walioshiriki uchaguzi huo ilikuwa ndogo kinyume cha taratibu za uchaguzi.

 

Hali hiyo ilitokea baada ya baadhi ya madiwani wanachama wa Chadema kususia kushiriki uchaguzi huo uliofanyika chini ya uangalizi wa askari polisi zaidi ya 20. Kiwia na Mbunge wa Viti Maalumu, Mkiwa Kimwaga (Chadema) na madiwani walisusia uchaguzi huo.

 

Jimbo la Ilemela linaundwa na kata tisa, kati ya hizo, tano zinaongozwa na madiwani kupitia Chadema na nne zinaongozwa na  madiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Jimbo la Ilemela pia lina diwani mmoja wa Viti Maalumu  kupitia Chadema na mwingine kupitia CCM.

 

Kutokana na mkanganyiko huo, Kiwia na madiwani waliogoma kushiriki uchaguzi huo waliwasilisha  malalamiko yao Chadema makao makuu.

 

Ili kunusuru chama, mwanzoni mwa Septemba 2012 Kamati Kuu ya Chadema ilimvua Matata uanachama kwa madai ya kukiuka taratibu, kusaliti chama hicho, kula njama za kumng’oa  aliyekuwa  Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza (kabla Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela haijazaliwa), Josephat Manyerere (Chadema) kinyume cha katiba ya Chadema.

 

Hata hivyo, Matata alipinga tuhuma hizo kwa kufungua kesi mahakamani kwa kushirikiana  na Diwani wa Kata ya Igoma katika Jimbo  la Nyamagana, Adams Chagulani (Chadema), ambaye pia alivuliwa uanachama kwa tuhuma kama zinazomkabili Matata.

 

Huku akijiita ‘diwani wa mahakama’, Matata alifungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza.

 

Miezi michache baadaye, Matata kupitia mawakili wake, Salum Magongo na Chacha, aliiondoa  kesi hiyo mahakamani kwa madai kuwa ataendelea kuishtaki Chadema kupitia kesi nyingine aliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza.

 

Kwa ujumla, mgogoro huo umeendelea huku  ukidaiwa kuathiri Chadema na shughuli za maendeleo  kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, kutokana na kukwama kwa baadhi ya vikao muhimu vya madiwani.

 

Mgogoro huo ndiyo chanzo cha maandamano ya wafuasi wa Chadema yaliyofanyika Agosti 19,  mwaka huu kwa kuratibiwa na Mbunge wa Ilemela,  Highness Kiwia.

Maandamano hayo ndiyo yamesababisha kukamatwa kwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema), akituhumiwa kuyachochea.

Kwa jumla, bado hali si shwari katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

By Jamhuri