Kuanzia kitongoji hadi
Ikulu wote wanalalamika

Siku kadhaa zilizopita nilikutana na mwanahabari mwenzangu, Khalfan Said. Aliniuliza swali hili; “Huu uamuzi wa Rwanda na Uganda kususa bandari zetu utakuwa na athari gani kwa uchumi wetu.” Khalfan aliniuliza swali hili akitambua kuwa mimi si mchumi. Hilo analitambua vema. Mara moja nikatambua kuwa tunao kina Khalfan wengi wanaotaabishwa na jambo hili, kiasi kwamba wapo radhi kumuuliza yeyote wanayemwona hata kama wanajua si mtaalamu wa masuala ya uchumi.

Nilijaribu kutumia akili ya kawaida kumjibu. Nikasema kuwa serikali za Uganda na Rwanda ni sehemu tu ya wateja kati ya wateja wengi wa bandari zetu katika mataifa hayo. Hili ni suala la biashara, kwa hiyo sidhani kama mataifa hayo yanaweza kutoa amri ya kuwazuia wafanyabiashara wao kuzitumia bandari zetu.

Kinachoweza kuwaondoa ni uduni wa huduma kwenye bandari zetu na uchovu wa miundombinu, hasa reli. Kinachoweza kuwapeleka Mombasa ni kukwepa kadhia za urasimu, rushwa, wizi wa mizigo na kadhia ya mapolisi barabarani ambao ni wengi mno.

 

Nilimweleza Khalfan kuwa kitakachotukwaza hata uchumi wetu uweze kutetereka ni hayo niliyojaribu kuyasema. Kinyume cha hayo, sioni kama kuna jingine la hatari.

 

Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba Tanzania ni kama familia ambayo ina vyakula vyote ndani ya nyumba, lakini inahemea. Inashinda kutwa bila kula. Inatokewa na hali hiyo kwa sababu, ama wenye nyumba wenyewe ni wavivu, au hawana maarifa ya mapishi! Unapowakuta watu ndani ya familia hiyo wakilia njaa, wewe unayewashuhudia unapaswa kutilia shaka uwezo wa kiakili wa watu hao.

 

Tanzania tuna kila kitu kinachopaswa kututoa kwenye udhaifu huu wa kulialia kwamba tuna maisha magumu. Kijiografia tupo mahali mazuri mno. Nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Zambia, Malawi na sehemu kadhaa za Msumbiji, wanaitegemea sana Tanzania katika masuala mengi. Kama tungekuwa makini, bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara zingetosha kabisa kuifanya Tanzania iwe paradiso. Bandari hizo pekee zingeweza kuuendesha uchumi wetu.

Kila Mtanzania analalamika. Kuanzia Ofisi ya Rais hadi kwa mtendaji wa kitongoji, kote ni malalamiko tu. Watu wamekata tamaa. Watunga sera wanalalamika kama watekeleza sera! Mpigakura na mpigiwa kura – wote wanalalamika.

 

Desemba 30, 2005 Rais Jakaya Kikwete akifungua rasmi Bunge jipya, alizungumzia utendaji serikalini. Alisema, “Mheshimiwa Spika, dhana ya utawala bora ni pana sana; ni zaidi ya vita dhidi ya rushwa. Tutahimiza utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ustadi, kwa haraka na kwa ufanisi.  Tunataka watendaji wa Serikali wawe waadilifu, na wanaowajibika; wawe na ari, moyo, na msimamo wa dhati kuhusu utumishi wa umma na huduma bora kwa umma.  Tabia ya “njoo kesho” na nenda rudi, tuache. Mwalimu alituasa linalowezekana leo lisingoje kesho.  Napenda huo uwe moyo wa utendaji serikalini.”

 

Kuhusu kasi ya maendeleo, alisema, “Mbali ya kusukumwa na hoja ya kukuza uchumi haraka ili kupiga vita umaskini, tunasukumwa pia na ukweli wa nguvu za utandawazi na ushindani mkubwa katika masoko ya kanda na ya kimataifa.  Hivyo basi, sote tuunganishe nguvu zetu ili tuongeze uzalishaji, tuongeze uwekezaji, tuongeze mauzo nje, tuongeze ubora wa mazao na huduma zetu na tuongeze kasi ya ukuaji wa uchumi wetu ili upae.”

 

Ndugu zangu, nukuu hii kutoka kwenye hotuba ya Rais Kikwete ni muhimu sana. Kasi ya maendeleo duniani hailisubiri taifa wala mtu mmoja mmoja. Maendeleo duniani yanakwenda kwa kasi ambayo si rahisi kuieleza.

 

Kwa miaka mingi tunazungumza ujenzi wa Reli ya Kati ili iwe ya kisasa zaidi. Mipango ilishabuniwa ili reli hiyo ianzie Dar es Salaam hadi Rwanda. Miaka 10 sasa baada ya mpango huo, tujiulize tumefanya nini? Wakati sisi hapa tukiwa mabingwa wa upembuzi, upembuzi yakinifu, semina, makongamano, warsha na mikutano iliyojaa ulaji, wenzetu Kenya wameamua kuingia kazini kweli kweli ili wamudu kasi ya dunia ya leo.

 

Tunachojua ni kama kile tulichoambiwa kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) wametumia Sh bilioni 9 kwa ajili ya kulipana posho za vikao! Haya ndiyo tunayoyaweza.

 

Wakati kupata kiwanja Rwanda kwa mwekezaji ni siku tatu na hati ni siku saba; sisi Tanzania ni kazi ya kutungwa mimba – mtoto kuzaliwa – anakuwa kijana – anaanza kazi, hadi anang’atuka; huku yule aliyeomba kibali cha uwekezaji akiwa hajakipata! Tumekuwa nchi ya urasimu, rushwa, njoo kesho, niko kwenye kikao, niko likizo, na majibu ya kipuuzi mengi tu ya aina hiyo.

 

Kila jambo kwetu ni gumu kutekelezeka. Tunachowapiku wenzetu ni porojo na kulalama. Mfano mzuri ni wa hivi sasa ambako Rwanda kumeibuka propaganda nyingi za kuichafua Tanzania. Hapa kwetu husikii Ikulu, Wizara ya Habari wala Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakikanusha uongo huo. Tumejisahau ilhali wenzetu wakiendelea kuwalisha uongo walimwengu.

 

Kwa kuwa leo sina nafasi ya kutosha kwenye safu hii, niombe tu mniruhusu niendelee na mada hii kwenye matoleo yanayofuata. Lililo muhimu ni kuhakikisha tunabadilika kuanzia mtu mmoja mmoja hadi kwenye ngazi ya taifa.

1184 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!