Tanzania ni nchi yangu ninayoipenda kwa moyo wote, ni kisiwa cha amani, upendo na utulivu, ni nchi yenye watu wakarimu na wenye upendo na mahaba yasiyopimika. Watanzania wanaishi kwa kupendana kuthaminiana na kuheshimiana bila kujali matatizo au changamoto zinazowakabili, kila mmoja akimuita mwenzake ndugu.

Naamini maji ya mabonde na mito mikubwa ndani ya nchi hii ndiyo yaliyoosha nongo za nyota zetu ambazo baadaye zimeng’aa kabla hata ya kupandishwa kwenye kilele kirefu cha Mlima Kilimanjaro; mlima ambao Mwenge wa Uhuru ulipandishwa uweze kuleta matumaini pasipokuwa na tumaini, kuleta amani pasipokuwa na amani, kumulika wahujumu uchumi, uwamulike maadui wa maendeleo – ujinga, maradhi na umaskini – kila mtu aweze kupamabana nao.

 

Tanzania nchi yangu imekuwa ngome imara ya kuigwa kama si kupigiwa mfano kwenye nchi majirani tangu enzi za dahari. Mara kadhaa viongozi wa Tanzania wameshiriki kuleta amani na upatanisho kwenye nchi majirani kwa kipindi ambacho nchi majirani zetu walipokuwa kwenye mitanziko na mihemuko ya kisiasa ambayo kwa namna moja au nyingine ilihatarisha afya ya amani kwenye nchi zao.

 

Tanzania imekuwa nyumba ya kuhifadhi wakimbizi waliokimbia kwao kwa matatizo ya kivita au matatizo mengine ya kibinadamu, ambayo wahanga waliona kuwa Tanzania itakuwa sehemu salama kwao kupakimbilia.

 

 

Tanzania imejaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na ardhi yenye rutuba inayokubali mazao ya aina mbalimbali. Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yake akaweka kwenye ardhi hiyo madini ya thamani kubwa ambayo mengine yanapatikana Tanzania pekee.

 

Kwenye ardhi hiyo hiyo, Mwenyezi Mungu akaweka tena wanyama wa aina mbalimbali ili Watanzania wawatumie kwa faida ya maisha yao. Ni kwenye ardhi hiyo hiyo Mwenyezi Mungu aliweka na gesi inufaishe Watanzania kwa kuboresha maisha yao.

 

Mwenyezi Mungu akatupendelea tena, akaweka maziwa makubwa na bahari tuvue samaki kama kitoweo kwa ajili yetu lakini pia kwa ajili ya biashara. Naamini haya yote Mwenyezi Mungu ameyafanya akiwa na mapenzi ya dhati, malengo, na upendo mkuu uliopitiliza kwa Watanzania.

 

Ni Tanzania hii hii ambayo leo ukikosoa kwa nia njema ‘kwanini vitu alivyotupa Mwenyezi Mungu bure kwa mapenzi yake na ridhaa yake’ havimnufaishi Mtanzania kwa kiwango anachostahili, baadhi ya watawala hukubatiza jina na kukuita mchochezi, tena wengine wakitoa kauli hizo huku duru zikionesha kuwa wanatuhumiwa kwa ufisadi.

 

Ni Tanzania hii hii ambayo haki za kiraia zikikandamizwa, wenye jicho la kuona na kuthubutu wakikemea hutekwa nyara, hung’olewa kucha na meno.

 

Ni Tanzania hii hii ambayo baadhi ya viongozi wetu wanadiriki kuacha miiko ya uongozi na kuanza kutoa kauli tata zinazokiuka hata viapo vyao mara baada ya kukabidhiwa madaraka.

 

Majuzi, Waziri Mkuu amesema wanao kaidi kutii amri wapigwe. Alishasema pia kwamba wanaoua albino nao wauawe wakati sheria inasema wahukumiwe na vyombo vinavyohusika.

 

Bila kujiuliza na kupata sababu za kina kwanini wadogo wetu wanapata mimba kwenye shule za ukata, eti nasikia mheshimiwa wa Magogoni naye alishawahi kusema, “Wanafunzi wanaopata mimba wana viherehere.”

 

Waziri mmoja naye akatoa kauli ya kijeuri kwa sisi kina kajamba nani, ambao tusingemudu nauli ya kivuko eti akasema, “Wasioweza kulipa nauli wapige mbizi.” Yaani kama hatuwezi kulipa nauli tupige mbizi kutoka Kigamboni hadi Posta, tukizama!

 

Nikakumbuka kuna waziri mwingine wa fedha naye katwambia kuwa rais anahitaji ndege, na kwa kuwa ndege lazima inunuliwe tutakula hata nyasi kama mbuzi lakini lazima ndege inunuliwe. Yeye kwake kipaumbele kikawa ndege huku wadogo zetu wakiwa hawana hata madawati ya kukalia.

 

Nikakumbuka na wale wanaohamishwa kwenye makazi bila kulipwa fidia, au kujua wanakwenda wapi, nikakumbuka nyumba za wahanga wa mabomu kule Mabwepande!

 

Nikaishiwa nguvu nilipokumbuka kuwa kuna mjomba wangu alinipigia simu ili nimtumie fedha ya kununulia dawati, nikawakumbuka na wale wanafunzi waliofaulu huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

 

Nikakumbuka na wale mamia waliopata daraja sifuri halafu ikaundwa tume ya kupoza wazazi machungu. Nikakumbuka kuwa viongozi wetu wengi watoto wao hawasomi kwenye hizi shule wanazozitungia sera.

 

Nikamkumbuka sana Mwalimu Nyerere aliyetengeneza mazingira ya kupata elimu bila matabaka. Natamani ningekuwa na anuani yake nimwambie: Navumilia kuwa Mtanzania.

By Jamhuri