Sasa kwetu Tanzania ni mauaji tu kila mahali. Na kama hakuna mauaji basi utasikia vurugu bungeni, vyuoni na maeneo mengine. Ile sifa kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani haiko tena. Kila mtu anaishi kwa hofu na wasiwasi.

Mchungaji wa wanyama anahofia wakulima, naye mkulima anamuhofia mchungaji. Spika wa Bunge anawahofia wabunge, nao wabunge wanamuhofia Spika.

Mwenyeji anamuhofia mgeni, naye mgeni anamuhofia mwenyeji. Polisi anamuhofia raia, nao raia wanahofia polisi. Hiyo ndiyo hali halisi ya leo. Ni mapinduzi makubwa ya maisha, hatuna tena kisiwa cha amani.

Viongozi wa dini hawalali, wanaombea amani Tanzania. Lakini amani inaendelea kutoweka, inawezekana kwamba Mungu amejitenga na Tanzania. 

Maana hakuna mmoja wetu anayeweza kujitapa kwamba ndiye mwenye uwezo wa kudumisha Tanzania. Amani ya Tanzania itadumishwa na Mungu. Na katika hili, mtunga Zaburi amesema “Bwana asipoilinda nyumba yeye ailindaye akesha bure.” Kadhalika na mji na nchi bila ulinzi wa Mungu hakuna kitu.

Kama leo lingefanyika kongamano la Taifa kuzungumzia sababu ya Tanzania kutoweka amani, hapana shaka zitatolewa sababu nyingi, hakuna sababu moja. Ningekuwapo kwenye kongamano hilo, ningetoa sababu za kutoweka amani Tanzania. 

Kwanza, watu wengi hawana hofu ya Mungu. Kwa hiyo, hawaamini tena kwamba siku moja watahukumiwa na Mungu kutokana na yale wanayoyatenda wakati huu. Kwa kweli ile amri kuu inayomtaka binadamu ampende mwenzake kama nafsi yake au anavyojipenda mwenyewe inaonekana haina nguvu tena. Hakuna anayempenda jirani yake kwa moyo, majirani wamebaki kudhulumiana.

Pili, maadili hayapo tena Tanzania. Kila mtu anamsema mwenzake vibaya. Hata mtu anapomtaka mwenzake kufanya jambo baya analofanya atamuuliza yeye ni nani – ni polisi? Na wataishia kutukana. Hakuna tena upendo katikati ya Watanzania, wamebaki tu wachungaji na maaskofu kuhubiri upendo makanisani, lakini nani anawasikiliza?

Inawezekana usikute maadili mahali pengine lakini ungetazamia kukuta maadili mashuleni, lakini wapi! Leo nani atanitajia shule ambayo wanafunzi wanaishi kwa amani na hawapigani? Wanafunzi wengi wanachokozana wakati wa masomo. Kwa maneno mengine ugomvi huandaliwa wakati wa masomo. Saa za masomo zikimalizika wanafunzi huwa na ugomvi. Hii ndiyo hali halisi ya shule zetu za leo; walimu wakuu wana kazi.

Kwa kweli kuna haja viongozi wa shule kuhubiri maadili. Tanzania ya leo haina maadili, nani anabisha? 

Tatu, kufutwa kwa Azimio la Arusha kumechangia sana kuvunjika kwa amani Tanzania. Kwa upande mmoja watu wanashindana katika kujipatia mali kwa njia yoyote ile ikiwa ni pamoja na mauaji ya albino, ujambazi na kadhalika.

Kwa upande mwingine kutoweka kwa Azimio la Arusha kumeendana na kutoweka kwa upendo na tabia ya kuheshimiana. Kama tujuavyo, Azimio la Arusha lilikuwa tamko rasmi la Chama cha TANU juu ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Siasa ya Ujamaa ilihubiri upendo, usawa na kuheshimiana.

Lakini wakati huo huo ujamaa ni umoja. Baada ya kutoweka Azimio la Arusha pia umoja umepungua nguvu yake. Kwa kweli Siasa ya Ujamaa iliwaweka Watanzania karibu. Kwa mfano, ule utaratibu wa kuitana ‘ndugu’ badala ya kuitana ‘mheshimiwa’ Watanzania walikuwa kitu kimoja.

Leo si wamoja tena, tofauti kubwa za mapato hazikuwatenganisha tu Watanzania bali pia zimesababisha Watanzania kuishi kwa matabaka. Huwezi kutegemea kukuta amani mahali ambapo watu huishi kwa makundi na matabaka. Kwa kweli waliofuta Azimio la Arusha wameifikisha pabaya Tanzania.

Nne, wanasiasa wamechezea amani. Katika Tanzania ya leo amani imechezewa wakati wote na hasa wakati wa uchaguzi yanafanyika mambo yanayovuruga amani Tanzania. Unakuta mtu hatangazwi kuwa mshindi wa uchaguzi mpaka yeye na wafuasi wake walete machafuko. Ubinafsi umesababisha watu wachache kukiuka misingi ya haki, na bila haki hakuna amani.

Leo Bunge la Tanzania limepoteza heshima yake. Wale wasiotaka ukweli wamebaki wanalaumu upinzani. Lakini ukweli ni kwamba wapinzani hawatendewi haki, katika mazingira hayo unakuta wapinzani wanapiga kelele bungeni au wanatoka nje. Wanasiasa wanachezea amani.

Ukitaka kusema ukweli, watu wa chama tawala wanawaona wapinzani kama si Watanzania kamili ila ni wageni katika nchi yao wenyewe. Kwa hiyo, unakuta mawazo ambayo yangesaidia kujenga nchi au amani yanapuuzwa na kupigwa vita eti kwa sababu yametokea kambi ya upinzani.

Ukweli ni kwamba amani ya Tanzania yetu iko mikononi mwa wanasiasa. Wakitaka wanaweza kuimarisha amani yetu, na wakitaka wanaweza kuchochea chuki na vita.

Lakini wakati huo huo tunapozungumzia kutoweka kwa amani, upendo na maadili katikati yetu hatuwezi kuepuka kuhusika na mambo yanayotokea wakati huu na yale yaliyotajwa kwamba yataonekana wakati wa mwisho wa dunia. 

Kama ndiyo mambo hayo ya mwisho wa dunia, kwa kweli tuna kazi pevu ya kupambana nayo. Hebu tuangalie maandiko. Waraka wa 2 wa Paulo Mtume kwa Timotheo 3: 1-4, tunasoma hivi; “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu.”

Huenda siku zenyewe za mwisho ndizo hizi. Basi ni vigumu kuzuia maandiko yasitimie.

By Jamhuri