Kama siyo sisi ni nani?

Sisi ni daraja kati ya kizazi kilichopita na kizazi kijacho. Tunakiachia nini kizazi kijacho? Tunaacha alama gani? Namna gani tunakabidhi kijiti? Tutakumbukwa kwa mambo gani? Methali ya Kiyahudi inasema yote: “Kama siyo sasa ni lini? Na kama siyo sisi ni nani?” 

Kama siyo wewe ni nani? Kuwa upinde wa matumaini katika wingu la kukata tamaa la mwingine. Kuwa malaika wa ufufuko kwa ambaye ndoto zake zimekufa. Fanya kitu kizuri cha kusukuma gurudumu la maendeleo mbele. John W. Newbern alisema: “Watu tunaweza kuwaweka katika makundi matatu: Wale ambao wanafanya mambo yatokee, wale ambao wanatazama tu mambo yakitokea, na wale ambao wanayashangaa yale yanayotokea.” 

Unaalikwa kuwa kundi la kwanza kama hujaingia. Ni kundi la watendaji na si watazamaji. Ni kundi la wawezeshaji na si wakwamishaji. “Swali ambalo linajirudia sana maishani na linalohitaji jibu haraka sana ni ‘Unafanya nini kwa ajili ya wengine?’ Anatutafakarisha Martin Luther King, Jr. Mungu alikuumba uache alama. Fanya kitu kwa ajili ya wengine. Tunakula maembe kutoka miembe iliyopandwa na watu wengine. Tunakaa kwenye majengo yaliyojengwa na watu wengine. Tunasoma vitabu vilivyoandikwa na watu wengine. Fanya kitu fulani. Usiiache dunia ulivyoikuta. “Kama hupendi jambo fulani, libadili. Kama huwezi kulibadili, badili mtazamo wako juu ya jambo hilo,” alisema Maya Angelou. Kuwa wewe na fanya mambo kama wewe. “Kama Mungu angetaka uwe vinginevyo, angekuumba vinginevyo,” anatukumbusha Johann von Goethe. 

Tuna mifano mingi ya watu wengi walioacha alama. Mfano mmojawapo ni wa Henry Ford (1863-1947). Huyu alikuwa mfanyabiashara na mwanaviwanda mzaliwa wa Marekani. Alianzisha kampuni iliyoitwa Ford Motor Company.  Gari la modeli ya T ya Henry Ford lilitengenezwa mwaka 1908. Mwaka 1914 alizalisha magari 250,000. Hili lilikuwa ni pigo kwa watengeneza magari ya kukokotwa na farasi. Mwaka 1900 watu karibu 110, 000 walikuwa wameajiriwa kutengeneza lijamu na hatamu, magari ya farasi na mabehewa. Kuingia kwa gari modeli T ya Henry Ford waliokuwa wanafagia barabara kuondoa mbolea iliyosambazwa na farasi barabarani walipoteza kazi. 

Lakini jambo jipya lilizaliwa lililosaidia watu kusafiri kwa urahisi. Mabadiliko haya yalitupeleka mbali. Kizazi cha magari ya farasi kilitengeneza magari ya farasi. Kizazi cha Henry Ford kiliacha modeli ya gari la T. “Kila kizazi kinakwenda mbele zaidi ya kizazi kilichotangulia kwa sababu kinasimama kwenye mabega ya kizazi hicho. (Ronald Reagan).

Mambo hayakuwa rahisi kwa Henry Ford. Tuzingatie ushauri wake. Alisema: “Vikwazo ni mambo yanayoogofya unayoyaona unapotoa macho yako kwenye malengo yako.” Usitazame dhoruba, tazama malengo. Usitazame viunzi, tazama malengo. Henry Ford anashauri tusiache kujifunza. “Yeyote anayeacha kujifunza ni mzee, hata kama ana miaka ishirini au themanini. Yeyote ambaye anaendelea kusoma anabaki kijana. Jambo kubwa sana katika maisha ni kufanya akili yako ibaki ya kijana.” Elimu haina mwisho.

Umiza kichwa kuleta jambo jipya. Kuna kitengo cha uhandisi ambacho kilitoa orodha ya maswali tisa ya kusaidia kuleta jambo jipya. Unganisha? Kwa kujibu swali hili makampuni ya simu yamekuja na kifurushi cha kupiga mitandao mingine. Zidisha? Makampuni ya simu yanazungumzia kuongeza spidi 4G na 5G badala ya 3G au 2G. Punguza? Tunazungumzia kwa sasa tairi za magari zisizo na mpira wa ndani. Matumizi mengine? Kutumia unga wa mbao kutengeneza mkaa au kuni. Kinyume? Elias Howe alikamilisha mashini ya kushona kwa kutengeneza sindano ikiwa na tundu chini badala ya juu. Mwonekano mpya? Simu za zamani zilikuwa ndefu mno kuna ambazo ziliitwa mche wa sabuni. Sasa kuna mwonekano mpya. Mbadala au chukua nafasi ya kitu? Barua pepe kwa kiwango kikubwa zimechukua nafasi ya kutuma barua kwa njia ya posta. Iga au azima? Ndege inaruka dhidi ya upepo kama tiara. Panga upya? Badili mpangilio. Hayo yote ni matunda ya kufikiria. Kama siyo sisi ni nani?

By Jamhuri