Ishi na watu vizuri. Ishi na majirani zako vizuri. Kumbuka: Unaishi na watu. Kuzaliwa kwako kumefanywa na watu. Jina lako unalotumia umepewa na watu. Umepata elimu kutoka kwa watu. Kipato chako unachopata kinatoka kwa watu. Heshima uliyonayo inatoka kwa watu. Ulipozaliwa uliogeshwa na watu. Wa mwisho kukuogesha watakuwa watu. Mazishi yako yatasimamiwa na watu. Utapelekwa makaburini na watu. Kila unachomiliki kitarithiwa na watu. Ishi na watu vizuri.

Maisha ni kama sarafu  iliyotupwa angani. Huwezi kutabiri itadondokea upande gani. Mtu unayemdhihaki leo na kumwona kama takataka, inawezekana ndiye atakayeamua hatima ya maisha yako kesho. Mwanzoni mwa mwaka 1980 meneja wa hoteli moja ya kitalii huko Hanzghou nchini China alimnyima kazi bilionea Jack Ma (kwa wakati huo Jack Ma alikuwa hana utajiri wa aina yoyote).  Baadaye Jack Ma alianzisha Kampuni ya Alibaba na kumwajiri mtu  yule aliyemnyima kazi.  Maisha ni mzunguko. Ishi katika mzunguko wa kumheshimu kila  mtu.

Wema ni akiba. Wema unaishi. Tenda wema katika maisha yako. Siku moja tajiri namba moja duniani bilionea Bill Gates aliulizwa swali na mwandishi wa habari kuwa anajisikiaje kuwa tajiri mkubwa zaidi duniani. Bill Gates akajibu: “Sidhani kama mimi ni tajiri namba moja duniani.” Mwandishi akamuuliza tena: “Kwa nini unadhani kuwa wewe si tajiri namba moja duniani?” Bill Gates akajibu: “Nadhani yupo mmoja.” Akaulizwa mtu huyo ni nani?

Akajibu: “Nilipokuwa shuleni sikuwa na fedha. Kuna wakati nilienda kwenye ‘vijiwe’ vya  kuuza  magazeti ili nisome tu japo vichwa vya habari. Kijana mmoja mweusi ambaye alikuwa ombaomba eneo lile aliniona.  Alijua nilihitaji gazeti lakini sikuwa na uwezo wa kununua. Akatoa kiasi cha pesa katika zile alizokuwa akiombaomba akaninunulia gazeti. Nilijaribu kukataa kwa sababu nilijua anaweza kulala njaa kwa sababu yangu, lakini akanisihi nichukue.

“Siku nyingine tena nilikwenda kijiwe kile na sikuwa na fedha. Sikutaka mtu yule anione. Hivyo nikapitia vichwa vya habari kimyakimya, na wakati ninaondoka nikaletewa gazeti, nimelipiwa na yule ombaomba. Akanitizama, akafurahi. Nikamtazama. Nikalia. Nikaondoka.” 

Mwandishi akamuuliza: “Sasa huyo aweza kuwa tajiri kuliko wewe wakati umesema ni ombaomba?” Bill Gates akajibu: “Mtu yule alitoa  hata kile kidogo alichokuwa nacho ili kunisaidia. Hakujali kuwa anaweza kulala njaa, kukosa malazi, kukosa mavazi, hakujali kupoteza akiba yake yote ndogo aliyokuwa nayo ili kunisaidia. Nadhani mtu yule ni tajiri kuliko mimi.”

Mwandishi akamuuliza: “Kwa nini usimtafute umlipe?” Bill Gates akajibu: “Nimemtafuta tayari nimemnunulia nyumba, na kumpa dola milioni moja lakini sijaweza kulipa hata robo ya alichonipa.” Mwandishi akamuuliza: “Kwa nini?” Bill Gates akajibu: “Kwa sababu mimi nimetoa sehemu ndogo katika kikubwa nilichonacho, lakini yeye alitoa sehemu yote katika kidogo alichokuwa nacho. Nadhani mtu yule ni tajiri kuliko mimi.”

Kataa roho ya uchoyo inayokufanya usiyafurahie mafanikio ya mwenzako. Watakie wengine mema. Kuanzia leo jifunze kuwasema watu vizuri. Mseme vizuri mke/mume wako. Mseme vizuri jirani yako. Mseme vizuri rafiki yako. Mseme vizuri mfanyakazi wako. Mseme vizuri mtoto wako. Mseme vizuri kiongozi wako wa nchi. Mseme vizuri kiongozi wako wa kiroho. Mseme vizuri Mungu.

Papa Fransisko anasema: “Kuongea vibaya kuhusu watu wengine ni sawa na kuwauza. Hakuna tofouti na kile alichokifanya Yuda ambaye alimuuza Yesu kwa vipande thelathini vya fedha. Kamwe usiwazungumzie wengine vibaya.” Kuna watu wana uchoyo ambao kwa muda fulani unakuja kugharimu maisha yao. Wivu ni msalaba wa  kujitengenezea.

Askofu Mkuu Fulton J. Sheen alipata kuwaasa waumini wake kwa maneno haya: “Misalaba mingi tunayobeba ni ya kujitengenezea wenyewe, tumeitengeneza kwa dhambi zetu.” Acha wivu. Wivu ni msalaba wa kujitengenezea.

By Jamhuri