Haya nayo yana mwisho

Ninapotafakari mwenendo wa kiti cha Spika, sioni kama kuna umuhimu wa kuwa na Bunge.

Kumbe basi, Tanzania tunaweza kuendesha mambo bila kuwa na hiki chombo ambacho katika nchi nyingine, ni chombo kitakatifu.

Spika Makinda, pengine kwa kutambua, au kutotambua, ameamua kuiumiza Serikali iliyotokana na chama chake-Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaonesha upendeleo wa wazi wazi. Anadhani anaisaidia, kumbe anaiumiza.


Kutoiweka ripoti ya CAG kwenye ratiba ili ijadiliwe na wabunge, si kuisaidia Serikali ya CCM, bali ni kuiumiza. Kama yupo aliyemshauri, na yeye akaupokea ushauri huo, wote wamefanya makosa.


Kuwaruhusu wabunge wa CCM wawashambulie wenzao wa Upinzani, na wakati huo huo kuwazuia wapinzani kujibu mapigo kwa hoja hiyo hiyo, ni udhaifu uliopindukia. Ndiyo maana sikushangaa mwishoni mwa wiki wabunge walipoamua kumpinga, tena wengine wakitoa sauti za kuashiria kumzomea. Hadi hapo sioni faida ya kuwa na Bunge kama mambo yenyewe ndiyo haya.


Bunge kufanywa kuwa ni chombo cha mijadala inayotoka kwa wabunge kwa uwiano, ni udhaifu mwingine. Uamuzi huu wa kikanuni una maana kwamba hata kama kinachojadiliwa ni sheria, na kuna wabunge wataalamu wa sheria, alimradi uwiano hauwapi nafasi, hawawezi kupewa fursa ya kuboresha muswada kwa sababu kuna wabunge wengine wachuuzi ambao nao wanastahili nafasi ya kuchangia kwenye sheria hata kama hawaijui!


Weledi walidhani kwamba ni vema kwenye mijadala kama hii, mbunge mwenye ujuzi kwenye jambo fulani, akapewa nafasi hata mara 10 kujadili muswada au hoja kadri inavyowezekana kwa lengo la hatimaye kuwa na kitu bora kilichopitishwa na Bunge.


Kuwa na mbunge mtaalamu wa uvuvi, akapewa nafasi ya kujadili masuala ya kivita ilhali wajuzi wa vita wapo lakini wameachwa kwa sababu ya kubanwa na uwiano, hili si jambo la mbolea kwenye mijadala na hatima ya nchi yetu.


Spika Makinda na wenzake waliotokana na CCM wana mifano mingi ya kuwawezesha kujiepusha na athari za ubabe huu wanaoufanya sasa. Rais Frederick Chiluba alipopitisha sheria za kibabe za kumbana mtangulizi wake, Baba wa Taifa la Zambia , Kenneth Kaunda, ni sheria hizo hizo zilizokuja kutumika baadaye kumweka kizuizini.


Hii ina maana gani? Maana yake ni kwamba Mama Makinda na wana CCM wenzake wanapoamua kuwakomoa wenzao kwa kutumia nguvu zao za kushika dola, watambue kuwa haya nayo yana mwisho. Kitanzi hiki hiki wanachokitumia kuwaumiza wenzao, kitatumika kuwabana wao pia. Wanachokifanya sasa ni sawa na mhudumu wa mochwari anayemcheka maiti, akidhani kwamba yeye hatakufa! Mhudumu wa aina hiyo ni juha.


Kuwapo madarakani na kuondoka ni kitu kilicho wazi. Tena basi, katika nchi kama yetu ambayo tumeamua kutokuwa na utawala wa kifalme, jambo hilo halipo mbali. Kila ninapowaona vijana hawa wanaohitimu elimu ya sekondari-japo ni kutoka shule za kata, kila ninaposikiliza mijadala ya watu mbalimbali, na kwa kurejea tu kwenye historia, sioni ni kitu gani kitaifanya CCM itawale milele. Sikioni.


Mama Makinda na wenzake waache kuwabana wenzao kwa matarajio kwamba ubabe utawasaidia kudumu madarakani milele. Watambue kuwa CCM, Chadema, CUF, UDP na wengine wengi watapita, lakini Tanzania itabaki kuwa Tanzania.


Wao na sisi tutapita, lakini Watanzania wengine watakuja. Kama hayo tunayaamini, basi tuweke uwanja sawa wa kuendesha siasa. Tuwe na mazingira ambayo leo CCM wakiondolewa madarakani, hawatataka kuingia vitani; hivyo hivyo, chama kingine cha upinzani kinapokosa fursa ya kuongoza serikali, kijione kuwa kina fursa ya kujipanga upya. Haki ndiyo maji na mbolea ya amani mahali popote duniani.


Kuendelea kufinyanga mambo kwa matarajio ya kubaki madarakani hakusaidii kuiepusha jamii na mageuzi yaliyo mbele.


Tukiitazama Tanzania kuwa ni ya Watanzania wote, kamwe hatuwezi kuzuia mijadala yenye tija, hatuwezi kuwabana wabunge wa upinzani ambao ni glisi ya uwajibikaji wa serikali, hatuwezi kuruhusu upande mmoja uutukane upande mwingine; na kamwe hatuwezi kugombea fito ilhali tukitambua kuwa sote tunajenga nyumba (Taifa) moja.


Kina Paul Kagame, Yoweri Museveni na wengine wengi waliitwa waasi. Sijui kama baada ya kuingia madarakani wanaendelea kuitwa kwa jina hilo! Muhimu zaidi ni kwa Mama Makinda na wenye fikra kama zake kutambua kuwa “Haya Nayo Yana Mwisho”.