Mara nyingi tumekuwa tukidharau mambo madogo madogo sana ambayo yapo ndani ya uwezo wetu kuyatekeleza ambayo kupitia hayo, tungeweza kuzinufaisha afya zetu kwa kiasi kikubwa sana na kujiepusha na magonjwa hasa yasiyo ya kuambukiza.
Wengi wetu tumejikuta tukipata maradhi mbali mbali na kulazimika kubeba mzigo mkubwa wa matibabu, lakini huenda kinga yake ni kufuata tu masharti madogo madogo sana ya kiafya ambayo kwa udogo wake hayalingani na ukubwa wa matibabu unaolazimika kujitwika baada ya homa.
Leo nitakueleza msomaji mambo hayo madogo madogo na utayashangaa kwa udogo wake na namna yanavyoweza kuleta manufaa makubwa sana kiafya na kisaikolojia pia.
Kula chakula taratibu

Hii ni changamoto hususani kwa jamii zetu za Kiafrika, huenda kutokana na asili ya malezi tunayopewa tangu tukiwa utotoni.  Tafiti mbali mbali za kijamii zimethibitisha kuwa familia nyingi za Kiafrika ni zile zinazohusisha idadi kubwa ya watu katika familia moja na mara zote zinakuwa na utamaduni wa kutumia sahani moja ya chakula kwa idadi kubwa ya watu, hii inawajengea watoto ile dhana kula kwa kasi kwani usipofanya hivyo huenda usishibe.
Kisaikolojia tabia hii inakuwa sugu hadi ukubwani na mtu anaweza kujikuta anaendeleza tabia hii hadi ukubwani na hata kama akiwa anakula peke yake. Kiafya hii ina madhara, kwa kuwa unaunyima nafasi mfumo wako wa umeng’enyaji wa chakula kufanya kazi yake kwa usahihi. Aidha, ulaji wa chakula taratibu unaupa ubongo wako nafasi ya kupokea taarifa kutoka kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kuashiria kuwa umeshiba, na hivyo utaepukana na ulaji uliopitiliza.

Lakini pia ulaji wa chakula taratibu unasaidia kumpa mlaji nafasi ya kukitafakari chakula anachokula, kuanzia ladha yake na ubora wake na hivyo kufanya uamuzi sahihi wa aina ya chakula ili kuepukana na madhara ya kiafya yatokanayo na ulaji wa vyakula ambavyo si salama.
Jumuika na wengine
Jenga tabia ya kuondokana na upweke mara kwa mara na ujumuike na watu wanaokuzunguka. Kwa kufanya hivi, utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuepukana na na matatizo ya kisaikolojia kama vile sonona (depression) na hata msongo wa mawazo. Lakini kwa kufanya hivi itakusaidia kuyamudu matatizo mengine ya kiafya kama vile shinikizo la damu na magonjwa mengine ya kiakili.
Siyo lazima uwe na watu wengi sana wa kujumuika nao, hata wachache tu ambao upo karibu nao wanaweza kuleta mabadiliko makubwa kwako zaidi ya ujuavyo. Kujumuika na watu hata kwa saa chache kunaongeza furaha, na kisayansi pia imethibitika kuna kuongeza utendaji kazi wa vichocheo vinavyoleta hisia mwilini na hivyo kukufanya uwe na ari ya kufanya jambo husika. Hivyo ita marafiki na ujumuike nao kwenye chakula cha jioni na hata sehemu yoyote ya kupumzisha akili angalau mara moja kwa wiki.

Kabili msongo wa mawazo na kila kitu kinachoingilia furaha yako. Moja ya vitu muhimu tunavyowahimiza sana watu ni kujitahidi kuishi maisha yenye afya bora. Lakini ukweli ni kwamba hamna maisha yenye afya bora pasipokuwa na furaha. Naomba ieleweke kuwa kukosa furaha kunaweza kusababisha matatizo mengi na makubwa sana kiafya zaidi ya vile unavyoweza kufikiria.
Hata sisi wahudumu wa afya huwa tunakutana na changamoto kubwa sana kuwatibu wagonjwa wenye matatizo ya kisaikolojia na hasa waliokosa furaha kuliko wagonjwa wa aina nyingine yoyote ile. Kila mmoja amewahi kupitia hali hii. Lakini msongo wa mawazo ukizidi unaweza kusababisha kukaza kwa misuli na kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo, ambayo yakidumu sasa husababisha matatizo kama vile magonjwa ya moyo na hata shinikizo la damu.
Hivyo, ni vyema kuyatamua mambo yanayokatisha furaha yako mara kwa mara na uweze kukabiliana nayo.

Na Dr Chris

2433 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!